Ukosefu wa fursa za ajira bado ni tatizo sugu duniani kwa mwaka 2013
Shirika la Kazi Duniani limetoa taarifa ya hali ya fursa za kazi duniani kwa kuonesha
kwamba, ukosefu wa fursa za ajira ni tatizo ambalo linazikumba nchi nyingi duniani.
Kuna dalili za kukua na kuboreka kwa uchumi katika nchi nyingi, lakini hali bado ni
tete sana. Dalili hizi zimejionesha katika nchi zinazoibukia katika uchumi kama vile
Brazil, India na Afrika ya Kusini pamoja na baadhi ya Nchi zinazoendelea.
Lakini
takwimu zinaonesha kwamba, katika nchi tajiri duniani kuna idadi kubwa ya watu wasiokuwa
na fursa ya ajira, jambo ambalo linaendelea kukua na kuongezeka maradufu, ikilinganishwa
na miaka kadhaa iliyopita. Tatizo hili linaendelea kuibua makundi ya watu ndani ya
Jamii: maskini wa kutupwa na kundi dogo la matajiri.
Baadhi ya Makampuni yameaanza
kupata faida baada ya miaka kadhaa ya athari za myumbo wa uchumi kimataifa. Uwekezaji
bado uko katika kiwango cha chini sana, kiasi ambacho si rahisi kufufua uchumi kwa
haraka kama wengi wanavyotarajia.