Masista watatu wa Shirika la Misericordia, Dodoma waweka nadhiri za kwanza!
Kwa njia ya nadhiri ya usafi kamili, ufukara na utii, maisha ya kitawa yanakuwa ni
ushuhuda wa kinabii kati ya watu wanaowazunguka na kikolezo kikubwa cha haki, amani,
upendo na upatanisho. Maisha ya kitawa ni ushuhuda wa upendo wa Kristo kwa Kanisa
lake, unaoimarishwa kila siku kwa Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, Sala
za Kanisa na Utume kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.
Mama
Kanisa anaendelea kuwachangamotisha watawa kuishi kwa uaminifu karama na utume wao
ndani ya Kanisa mintarafu miongozo ya waanzilishi wao, kwa njia hii wataendelea kulipamba
Kanisa kwa karama na mapaji waliyokirimiwa na Roho Mtakatifu daima wakijitahidi kusoma
alama za nyakati na kuendelea kushikamana na Maaskofu mahalia katika maisha na utume
wa Kanisa. Nadhiri zinawawezesha watawa kujitoa kwa ajili ya Mungu na jirani zao,
huku wakiendelea kujenga na kuimarisha ufalme wa Mungu kati ya watu wake.
Ni
changamoto iliyotolewa hivi karibuni na Askofu Gervas Nyaisonga wa Jimbo Katoliki
Dodoma wakati wa Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya Masista watatu wa Shirika la
Masista wa Huruma wa Verona (Misericordia) walipokuwa wanaweka nadhiri zao za kwanza,
kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Paulo wa Msalaba, Jimbo Katoliki Dodoma.
Askofu
Nyaisonga anasema, ubatizo ni mlango wa imani, unaomwezesha mwamini kushiriki katika
mafumbo na maisha ya Kanisa, daima akijitahidi kutekeleza mapenzi ya Mungu kadiri
ya wito wake. Nadhiri za kitawa ni kifungo kinachomwimarisha mtawa kuacha yote kwa
ajili ya kumtumikia Mungu na jirani, jambo ambalo linapaswa kufanywa kwa hiyari pasi
na shuruti.
Kwa njia ya Nadhiri za kitawa, watawa wanaweka pembeni haki nyingine
za maisha ya kijamii kama vile haki ya kuwa na mchumba, kumiliki mali na kuamua kadiri
ya mapenzi binafsi, ili kujifunga na Mwenyezi Mungu, ili kutumia nguvu na mapaji yao
kwa ajili ya sifa na utaswi wa Familia ya Mungu inayowazunguka. Hii ni huduma ya upendo
inayopaswa kutolewa pasi na upendeleo. Ni mwaliko wakuwa watii kwa Kristo, Kanisa
na Viongozi halali wa Shirika, huku wakijitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya Shirika
lao.
Wakiishi vyema nadhiri zao, anasema Askofu Nyaisonga watakuwa kwa hakika
"wamempiga bao shetani". Amewakumbusha watawa walioweka nadhiri zao za kwanza kwamba,
kama binadamu watakumbana na vishawishi lakini wanapaswa kusimama kidete kupambana
kufa na kupona kwa kutumia silaha na nyenzo zilizowekwa mbele yao na Mama Kanisa.
Kwa kufanya hivi, watawa hawa watakuwa wepesi katika kutenda, wenye hekima na busara.
Wajitahidi kutekeleza majukumu yao kwa busara, juhudi na maarifa na kamwe wasilegee
katika maisha yao ya kitawa.
Watawa walioweka nadhiri zao za kwanza ni: Sr.
Bridgita Clod, Sr. Delphina Raphael pamoja na Sr. Cecilia Marko. Ibada hii imehudhuriwa
pia na Askofu mstaafu Mathias Josefu Isuja wa Jimbo Katoliki Dodoma.