2013-06-04 07:38:43

Makampuni ya kimataifa yana wajibu wa kulinda na kudumisha haki msingi za binadamu!


Askofu mkuu Silvano Maria Tomasi, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Ofisi za Umoja wa Mataifa zilizoko mjini Geneva, hivi karibuni akichangia mada kwenye Baraza la Haki Msingi la Umoja wa Mataifa anabainisha kwamba, Mashirika ya Kimataifa na Haki msingi za binadamu ni ajenda inayopaswa kupewa kipaumbele cha pekee kutokana na matukio hatarishi ambayo yamepelekea watu wengi kupoteza maisha na mali zao, wakati wakifanya kazi kwa ujira mdogo, kama ilivyotokea hivi karibuni mjini Dhaka. RealAudioMP3

Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni alionya kwamba, kutokana na uchu wa kutafuta utajiri na faida kubwa, maisha, utu na heshima ya mtu vinawekwa rehani na badala yake, wanasiasa na watu wenye nguvu za kiuchumi kwenye Jamii ndio wanaopewa kipaumbele cha kwanza. Kuna watu wanafanya kazi kubwa kwa ujira mdogo usioweza hata kukidhi mahitaji msingi ya binadamu; kuna baadhi ya watu wamegeuzwa kuwa ni watumwa kwa kufanyishwa kazi za suluba; mambo yote haya ni kiyume kabisa cha mapenzi na utashi wa Mungu kwa binadamu.

Jumuiya ya Kimataifa haina budi kujenga na kuimarisha mbinu mkakati itakaoyosaidia kupambana na hali inayopelekea baadhi ya watu kufanya kazi katika mazingira magumu na hatarishi kwa usalama wa maisha yao. Wawekezaji kutoka nje ya nchi wanapaswa kujielekeza zaidi kwa kuwajengea wananchi uwezo wa kupambana na mazingira yao; kwa kulinda na kuthamini: haki zao msingi, utu na maisha yao kama binadamu sanjari na utunzaji bora wa mazingira.

Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, katika Waraka wake “Caritas in Veritate” Upendo katika Ukweli anasema, kuna haja ya kujenga na kuimarisha uhuru wa vyama vya wafanyakazi; kuondoa mifumo yote inayowafanyisha watu kazi za suluba; upendeleo katika ajira; kupinga kwa nguvu zote vitendo vya kuwafanyisha kazi watoto wadogo na kwamba, fursa za ajira na ujira zitekelezwe kadiri ya sheria za nchi na mikataba ya Jumuiya ya Kimataifa.

Mashirika na Makampuni makubwa ya kimataifa kwa sasa yanaendelea kuwekeza kwa ajili ya kupata faida kubwa, lakini wakati mwingine kwa kupindisha sheria na kanuni za nchi husika. Serikali na watunga sera wanapaswa kuwa makini kwa kuhakikisha kwamba, wawekezaji wanachangia kwa ukamilifu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi ili kusaidia mchakato wa kujenga na kudumisha usawa sanjari na kuheshimu haki msingi za binadamu.

Baadhi ya Mashirika na Makampuni haya anasema Askofu mkuu Silvano Maria Tomasi kwamba, yamekuwa yakivunja sheria za nchi na haki msingi za binadamu kwa makusudi bila kuchukuliwa hatua za kisheria. Umefika wakati kwa Mashirika na Makampuni haya kutekeleza wajibu wake kwa kuzingatia misingi ya haki, sheria na kwa ajili ya mafao ya wengi badala ya kuwanufaisha watu wachache katika Jamii. Ukweli na uwazi ni mambo ambayo yanapaswa kutiliwa mkazo wa pekee, ili wananchi wanaoishi katika maeneo husika waweze kufaidika na uwekezaji huo kutoka nje ya nchi.

Makampuni haya yazingatie viwango vya kimataifa na huduma kwa Jamii husika iwe ni kati ya vipaumbele vyao. Wafanyabiashara wanao wajibu wa kulinda na kudumisha haki msingi za binadamu; wasimame kidete kutunza mazingira kwa kuendeleza uchumi rafiki kwa binadamu na mazingira yake.








All the contents on this site are copyrighted ©.