2013-06-04 11:35:11

Hali ya chakula si shwari, kuna watu billioni mbili wanakabiliwa na baa la njaa duniani


Bwana Josè Graziano da Silva, Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa anasema kwamba, utapiamlo una gharama kubwa katika maisha ya kijamii pamoja na maendeleo ya kiuchumi, kumbe kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kujifunga kibwebwe ili kuhakikisha kwamba, utapiamlo unafutika katika uso wa dunia.

Katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, kumekuwepo na mabadiliko makubwa, lakini bado kuna njia ndefu ambayo Jumuiya ya Kimataifa haina budi kupitia ili kuhakikisha kwamba, tatizo la utapiamlo linatoweka katika uso wa dunia. Katika kipindi cha mwaka 2010 hadi mwaka 2012 kulikuwa na jumla ya watu millioni 870 waliokuwa wanakabiliwa na baa la njaa duniani. Taarifa ya hali ya chakula kwa mwaka 2013 inaonesha kwamba, kuna watu billioni mbili wanaoteseka kutokana na baa la njaa duniani, hali ambayo imepelekea afya ya watu hawa kuwa hatarini.

Bwana Josè Graziano da Silva anasema, hali hii haiwezi kukubalika duniani, kwani gharama na athari zake ni kubwa kwa uchumi wa Kitaifa na Kimataifa. Hali ya maisha ya watu inaendelea kudorora sanjari na kuendelea kushamiri kwa magonjwa nyemelezi yanayotokana na baa la njaa na utapiamlo. Kuna haja kwa wananchi kupata lishe bora inatokana na kilimo cha kisasa kinachozingatia ubora wa mazao toka pale yanapovumwa shambani hadi yanapomfikia mlaji.

Ili kupambana na tatizo la utapiamlo kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuwekeza katika sekta ya kilimo; kudhibiti upotevu wa chakula na kuongeza ubora wa lishe; walaji hawana budi kuwa na ufahamu mpana zaidi wa chakula wanachokula pamoja na kuhakikisha kwamba, wanawake na watoto wanapata chakula kwa wakati muafaka.







All the contents on this site are copyrighted ©.