2013-06-04 14:33:37

FAO kusaidia Tanzania kuanzisha Benki ya Kilimo


Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) limesema kuwa litaisaidia Tanzania katika kuanzisha Benki ya Kilimo nchini kama namna bora zaidi ya kusaidia kuboresha kilimo na kuwainua wakulima wa Tanzania. Aidha, FAO limesema kuwa litaendelea kuunga mno jithada kubwa zinazofanywa kwa sasa na Serikali katika kuboresha kilimo na kuwainua wakulima wa Tanzania kutoka kwenye umasikini.

Msimamo huo wa FAO umeelezwa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo, Mheshimiwa Dr. Jose Graziano da Silva wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete kwenye hoteli ya Intercontinental mjini Yokohama, Japan.

Mkurugenzi Mkuu huyo ametoa ahadi hiyo ya FAO kusaidia katika uanzishwaji wa Benki ya Kilimo Tanzania baada ya kuelezwa na Rais Kikwete kuhusu mipango ya Serikali ya Tanzania kuanzisha Benki hiyo kama namna ya uhakika zaidi ya uwezeshaji wa sekta ya kilimo na wakulima nchini.

Dr. Jose Graziano da Silva amemwambia Rais Kikwete: “Hili ni jambo zuri sana, nilikuwa sijapata nafasi nzuri ya kujua mipango hii. Ahadi yangu ni kwamba FAO itawasiliana haraka iwezekanavyo na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) ili kuangalia namna gani ya kusaidia uanzishwaji wa Benki. Ninachoweza kukuhakikishia Mheshimiwa Rais kuwa na sisi tutasaidia jitihada za Serikali yako kuanzisha Benki hii ambalo ni wazo zuri,” amesema Mkurugenzi mkuu huyo na kuongeza:

“Jitihada za Serikali yako ya kutoa ruzuku kwa wakulima ambazo mmekuwa mnazifanya ni jitihada nzuri sana na zimechangia katika kuinua uzalishaji na mapato ya kilimo. Hata hivyo, ruzuku ina mipaka yake kwa sababu haiwezi kutolewa wakati wote na kwa kila mkulima. Jibu sahihi ni kuwa na Benki ya Kilimo ambayo itatoa mikopo nafuu kwa wakulima.”

Mkurugenzi huyo wa FAO pia amemwalika Rais Kikwete kushiriki katika shughuli mbili kubwa za FAO ukiwamo Mkutano Mkuu wa mwaka wa Shirika hilo ambao umepangwa kufanyika makao makuu ya FAO mjini Rome, Italia kati ya Juni 15 hadi 22 mwaka huu. Mkurugenzi huyo pia amemwalika Rais Kikwete kushiriki katika Mkutano Maalum wa Kuanzisha Kampeni ya Kutokomeza Njaa Duniani ifikapo mwaka 2025.

Mkutano huo umepangwa kufanyika mjini Addis Ababa, Ethiopia Julai Mosi, mwaka huu, 2013 na Kampeni hiyo imebuniwa na Rais Mstaafu wa Brazil, Mheshimiwa Lula Silva. Rais Kikwete amekubali mialiko hiyo na akasema kuwa Serikali itaangalia nani ataweza kuiwakilisha Tanzania katika mikutano hiyo muhimu.








All the contents on this site are copyrighted ©.