Watanzania wanahimizwa kutunza mazingira, vyanzo ya maji, usafi na ujenzi wa vyoo
bora!
Waziri Mkuu Mizengo Pinda amesema Tanzania inapoteza kiasi cha hekta 400,000 za misitu
kila mwaka kwa sababu ya ukataji miti unaochochewa na matumizi ya kuni, mkaa, mbao,
ujenzi ama uchomaji moto misitu.
Alikuwa akizungumza na mamia ya wakazi wa
mji mdogo wa Namanyere, wilayani Nkasi mkoani Rukwa wakati akizindua Maadhimisho ya
Siku ya Mazingira Duniani yaliyoanza Jumamosi, Juni Mosi, 2013 ambayo Kitaifa yanafanyika
mkoani Rukwa. Maadhimisho hayo yatahitimishwa Juni 5, mwaka huu.
Alisema utafiti uliofanywa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (Tanzania Forest
Services - TFS) chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Mradi wake wa Tathmini
ya Rasilimali za Misitu Nchi unaonesha kuwa ukataji huo wa misitu unasababishwa kuzalishwa
kwa tani milioni moja za mkaa ambao nusu yake unatumiwa na wakazi wa Jiji la Dar es
Salaam.
“Tanzania inakadiriwa kuzalisha kiasi cha tani milioni moja za mkaa
kila mwaka, nusu yake yaani tani 500,000 zinatumika Dar es Salaam peke yake. Kuni
zinatumika sana vijijini wakati mkaa unatumika sana mijini. Ndiyo sababu tunasisitiza
kwamba, kama tukiwapatia wakazi wa mijini hususan wale wa Dar es Salaam nishati mbadala
kama vile gesi, umeme na nishati itokanayo na jua, tutakuwa tumepunguza kwa kiasi
kikubwa ukataji miti nchini kwa ajili ya kutengeneza mkaa,” alisema.
Aliwasihi
wakazi wa Nkasi na mkoa wa Rukwa kuhakikisha wanajenga nyumba bora zenye vyoo bora
kwani ni njia ya uhakika ya kutunza usafi wa mazingira na kupunguza maradhi ya kuambukiza.
“Watu
wamezoea kujenga nyumba nzuri lakini hawaweki uzito kwenye suala la choo bora...utakuta
choo kidogo tena urefu wake unaishia kifuani tu, unaweza hata kumpungia mtu mkono.
Jenga nyumba nzuri na hakikisha unaweka choo kizuri, chooni lazima pawe ni mahali
pasafi na pa heshima,” alisisitiza.
Alisema kila Halmashauri hapa nchini inapaswa
kulisimamia suala hilo kwani litasaidia kuondoa magonjwa kwa wananchi wake. Alisisitiza
utunzaji wa vyanzo vya maji, upunguzaji wa idadi ya mifugo na kuanzishwa kwa ufugaji
wa nyuki kama njia ya uhakika ya uhifadhi wa misitu na utunzaji wa mazingira.
“Mkuu
wenu wa mkoa kaeleza hapa idadi kubwa ya mifugo iliyomo mkoani mwenu. Suala hapa si
wingi wa mifugo mliyonayo bali eneo linalohitajika kwa ajili ya kulishia mifugo. Fugeni
kisasa kwa kuzingatia idadi ya mifugo inayotakiwa kwa eneo husika,” alisema.
Mapema
akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na wananchi waliohudhuria maadhimisho hayo, Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano) Bi. Samia Suluhu Hassan aliwataka wakazi
hao watunze mazingira, watunze misitu na wasiharibu vyanzo vya maji.
Naye Mkuu
wa Mkoa wa Rukwa, Mhandisi Stella Manyanya akitoa salamu za mkoa huo kwenye uzinduzi
huo alisema uharibifu wa mazingira katika mkoa huo umesababisha kushuka kwa kina cha
maji kwenye Ziwa Tanganyika pamoja na Ziwa Rukwa.
“Misitu kwenye mkoa wetu
imepungua kutokana na uharibifu wa mazingira. Pia kuna uharibifu wa mazingira unaoendelea
kutokana na uzalishaji mkubwa wa taka ngumu pamoja na utupaji hovyo wa takataka...
tuache uharibifu huu na tuhifadhi mazingira yetu,” alisisitiza.