Uchaguzi Zimbabwe unapaswa kufanyika katika kipindi cha miezi miwili kuanzia sasa!
Mahakama kuu ya Zimbabwe inaitaka Serikali kuhakikisha kwamba, inafanya uchaguzi mkuu
nchini humo katika kipindi cha miezi miwili, kabla ya tarehe 29 Julai 2013 wakati
ambapo Bunge la sasa litakuwa linakamilisha muda wake rasmi. Vyama mbali mbali vya
kisiasa nchini Zimbabwe vinatakiwa kuanza kujipanga kikamilifu ili mchakato wa uchaguzi
mkuu wa Rais na Wabunge uanze mara moja.
Itakumbukwa kwamba, Serikali iliyoko
madarakani kwa sasa ni ile ya kitaifa, baada ya kutokea machafuko ya kisiasa nchini
Zimbabwe kunako mwaka 2008, Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe na Bwana Morgan Tsvangirai
wakalazimika kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Rais Mugabe anataka uchaguzi ufanyike
mara moja!
Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Zimbabwe Bwana Morgan Tsvangirai
anapendelea kwanza kufanyike mageuzi makubwa katika sheria, vyombo vya ulinzi na usalama
pamoja na sheria za uchaguzi. Uchaguzi mkuu wa Zimbabwe unatarajiwa kufanyika chini
ya Kabisa Mpya iliyopitishwa hivi karibuni kwa wananchi wa Zimbabwe kuipigia kura
ya maoni, baada ya vuta nikuvute ya vyama vya kisiasa nchini Zimbabwe.