2013-06-03 07:24:25

Taasisi ya Mafunzo ya Afya ya Mtakatifu Bakhita, Jimbo Katoliki Sumbawanga, kugharimu kiasi cha Billioni 6.6


Waziri mkuu Mizengo Pinda amesema Serikali itasaidia kadri itakavyoweza kwenye ujenzi wa Taasisi ya Mafunzo ya Afya ya Mtakatifu Bakhita iliyopo Namanyere, wilayani Nkasi, mkoani Rukwa, nchini Tanzania. Chuo cha Mtakatifu Bakhita kinamilikiwa na kuendeshwa na Jimbo Katoliki la Sumbawanga.

Alikuwa akijibu risala ya taasisi hiyo wakati alipoitembelea ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yaliyoanza Juni Mosi, 2013 kwenye mji mdogo wa Namanyere, wilayani Nkasi mkoani Rukwa.

Ujenzi wa taasisi hiyo unaochangiwa na wafadhili mbalimbali unatarajia kugharimu sh. Bilioni 6.6 ambapo mabweni matatu yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 576 yanatarajiwa kujengwa. Pia madarasa manne yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 400 yanatarajiwa kukamilika chini ya mradi huo.

Maeneo mengine ni vyumba vya kujisomea, ukarabati wa madarasa mawili ya zamani ambapo moja litatumika kama maabara ya kufundishia na jingine litatumika kama chumba cha kompyuta kwa ajili ya wanafunzi.

Akisoma risala mbele ya Waziri Mkuu, Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Sista Helena Katebera alisema taasisi hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo uhaba wa fedha kwa ajili ya uendeshaji wa shughuli za taasisi hiyo ambayo inatoa kozi ya Afya ya Uuguzi na Ukunga pamoja na wasaidizi wa maabara zote zikiwa ni kwa ngazi ya cheti.

“Chuo kinakabiliwa na uchache wa walimu wenye sifa stahiki; upungufu wa vitabu na vifaa vya ufundishaji kwa vitendo kwa kozi zote mbili; ukosefu wa gari la chuo na kutolipwa madeni yanayofikia sh. milioni 80 zikiwa ni ada za wanafunzi waliodhaminiwa masomo na taasisi mbalimbali,” alisema.

Wakati huohuo, Waziri Mkuu pia alitembelea Hospitali teule ya Wilaya ya Nkasi na kukagua baadhi ya majengo ambako pia alielezwa kwamba uongozi wa hospitali hiyo umeanza kufanya upanuzi wa wodi ya wazazi ili iweze kuwahudumia wazazi tisa kwa wakati mmoja badala ya watatu kama ilivyo sasa.

Akisoma taarifa ya hospitali hiyo mbele ya Waziri Mkuu, Mganga Mfawidhi, Dk. Norbert Twamba alisema hospitali hiyo inakabiliwa na upungufu wa watumishi wa kada mbalimbali wakiwemo madaktari sita, madaktari wasaidizi 22, wauguzi 19, matabibu 10, maafisa wauguzi 13 na wahudumu wa afya 42.

“Gari la wagonjwa limechakaa mno kwa lililopo ni la tangu mwaka 2004 ambalo tulipewa na Baba Askofu wa Jimbo Katoliki la Sumbawanga na hadi sasa limetembea zaidi ya km.192,000,” alisema.

Vilevile, Dk. Twamba alisema hospitali hiyo inakabiliwa na upungufu wa madawa, vifaa tiba na vitendanishi na akaomba kusaidiwa ili waweze kutioa huduma kwa ufanisi zaidi.

Waziri Mkuu aliahidi kufuatilia maombi yao ili kuyapatia ufumbuzi.









All the contents on this site are copyrighted ©.