Watoto wagonjwa wana mwomba Papa kusali kwa ajili ya watoto wenzao ambao wanateseka
kwa magonjwa sehemu mbali mbali za dunia!
Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa jioni, tarehe 31 Mei 2013, amekutana na kuzungumza
na watoto ishirini ambao ni wagonjwa wa saratani kutoka Kitengo cha Watoto, Hospitali
ya Agostino Gemelli iliyoko mjini Roma waliosindikizwa na wazazi, madaktari, wauguzi
pamoja na viongozi wao wa kiroho, kwenye Kikanisa cha Domus Sanctae Marthae kilichoko
mjini Vatican.
Watoto hawa wakati wa hija yao kwenda kwenye madhabahu ya Bikira
Maria wa Lourdes walikuwa wamemtumia salam za matashi mema wakimwomba aje kusali pamoja
nao!
Padre Federico Lombardi msemaji mkuu wa Vatican anabainisha kwamba, mkutano
kati ya Baba Mtakatifu na watoto hao wagonjwa umefanyika katika hali ya ibada, furaha
na matumaini makubwa. Watoto hao wamemwomba Baba Mtakatifu Francisko kusali kwa ajili
ya kuwaombea watoto wagonjwa sehemu mbali mbali za dunia pamoja na kuwabariki wazazi
na walezi wao wanaojitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuwahudumia.
Baba
Mtakatifu amewahakikishia watoto hao kwamba, Yesu anawapenda upeo na kwamba, daima
yuko pamoja nao hata katika mahangaiko yao. Baba Mtakatifu amewapatia watoto hao baraka
zake za kitume, wote wakiwa wamefurahi kukutana na kuzungumza naye ana kwa ana na
wala si kama wanavyomwona kwenye Luninga. Watoto hao wamemwahidia Baba Mtakatifu sala
zao katika maisha na utume wake.