Katiba ni jambo tete lishughulikiwe kwa umakini mkubwa!
Askofu mkuu Paul Ruzoka , Mwenyekiti wa Tume ya haki na amani ya Baraza la Maaskofu
Katoliki Tanzania katika mahojiano na Radio Vatican anabainisha kwamba, mchakato wa
Katiba Mpya ya Tanzania ni jambo tete linalopaswa kushughulikiwa kwa umakini mkubwa.
Mchakato
huu umekwishapitia hatua mbali mbali na Jumatatu, tarehe 3 Juni 2013, Tume ya Mabadiliko
ya Katiba Tanzania itazindua Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Anasema, mchakato huu bado haujakidhi matakwa ya watanzania walio wengi ndiyo
maana kumekuwepo na manung'uniko kadha wa kadha, kwani masuala ya kidini yameonekana
kutawala zaidi, kinyume cha matarajio ya wengi. Kimsingi watanzania wengi wanataka
Katiba ambayo itajenga na kuimarisha umoja, upendo na mshikamano wa kitaifa. Katiba
ambayo kimsingi ni sheria mama, kamwe isiwe ni chombo cha kuwagawa wananchi wa Tanzania
kwa misingi ya ukabila, udini au mahali anapotoka mtu!
Katiba inapaswa kuzingatia
mafao ya wengi, utu na heshima ya binadamu. Iwe ni Katiba inayoleta tija kwa watanzania
wote na wala si kwa ajili ya masilahi ya kundi fulani miongoni mwa Jamii ya Watanzania.