2013-06-01 07:57:01

Jifunzeni kutoka katika shule ya Bikira Maria kwa: kusikiliza kwa makini, kuamua kwa busara na kutenda kwa hekima!


Rozari Takatifu ni sala inayomwezesha mwamini kutafakari hija ya maisha ya Yesu Kristo hapa duniani kama sehemu ya utekelezaji wa kazi ya ukombozi na kwamba, Bikira Maria anawaongoza waamini kumwendea Yesu. Bikira Maria katika hija ya maisha yake ya imani alifanikiwa: kusikiliza kwa makini, akatoa uamuzi thabiti na kuutekeleza mpango wa Mungu katika maisha yake.

Ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 31 Mei 2013, katika Maadhimisho ya Kumbu kumbu ya Bikira Maria kumtembelea Elizabeth sanjari na kuufunga mwezi wa Maria. Bikira Maria alikuwa na uwezo mkubwa wa kusikiliza kwa makini; akapokea ujumbe na hatimaye, kujiachilia mikononi mwa Mwenyezi Mungu, changamoto kwa waamini kuwa makini katika kusikiliza sauti ya Mungu katika maisha yao.

Bikira Maria alifaulu kusikiliza na kusoma alama za nyakati katika historia na hija ya maisha yake, akajifunza kuzama katika matukio hayo ili kufahamu mafumbo yaliyokuwa yamefichika ndani mwake, kiasi cha kukiri kwamba, hakuna lisilowezekana mbele ya Mungu.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kujenga ndani mwao utamaduni wa kumsikiliza Mungu, kusoma alama za nyakati kwa matukio mbali mbali yanayowazunguka pamoja na kuwajali jirani, kwani Mwenyezi Mungu anaendelea kuzungumza na waja wake kwa njia mbali mbali, jambo la msingi ni kuwa makini kuweza kutambua na kusoma alama hizi kadiri ya mpango wa Mungu.

Bikira Maria ni mwanamke aliyefanya tafakari ya kina katika maisha yake, kisha akachukua uamuzi, huku akijiachilia mikononi mwa Mwenyezi Mungu ili aweze kuwa ni chombo chake cha huduma. Ni maamuzi ambayo yaliacha chapa ya kudumu katika maisha ya watu, kama ilivyojitokeza kwenye arusi ya Kana. Hapa ubinadamu na utu wake unajionesha kwa hali ya juu kabisa, anatambua na kuonja adha ya wale wanandoa wapya waliokosa divai. Anatambua kwamba, Yesu anaweza kufanya muujiza, anaamua kumwendea.

Baba Mtakatifu anasema kwamba, wakati mwingine waamini wanakosa ujasiri wa kufanya maamuzi katika maisha yao na hata kushindwa kutekeleza wajibu wao. Katika hali kama hizi, Bikira Maria awe ni alama na kielelezo cha kufuata, kiasi cha kujiachilia mikononi mwa Mwenyezi Mungu. Ni mtu wa watu, kwani aliguswa na mahangaiko ya binamu yake Elizabeth aliyekuwa mjamzito, akaamua kwenda kumsaidia katika shida na mahangaiko yake. Uamuzi huu ni kielelezo cha utii unaomwilishwa katika upendo na matokeo yake ni furaha, amani na utulivu wa ndani.

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kusikiliza kwa makini, kuamua na kutenda kwa ajili ya kuwaelewa na kuwasaidia wale wanaohitaji msaada wao. Waamini wakumbuke kwamba, ndani ya mioyo yao wamempokea Kristo na Injili yake, changamoto ya kumshuhudia kwa maneno, lakini zaidi, kwa njia ya ushuhuda wa maisha.

Waamini wanachangamotishwa kujenga utamaduni wa kusikiliza kwa makini Maandiko Matakatifu; Jirani na Matukio ya Maisha. Bikira Maria awawezeshe waamini kuwa watiifu kwa Kristo kwa kujishikamanisha naye! Waamini wawe tayari kwenda kwa haraka sehemu mbali mbali za dunia ili kupeleka Mwanga wa Injili ya Kristo.

Ibada ya Rozari Takatifu imehudhuriwa na umati mkubwa waamini uliokusanyika kwenye uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro. Yote haya ni matukio yanayoendelea kuwaimarisha waamini katika hija ya maisha yao ya imani, changamoto ya kujifunza kutoka katika shule ya Bikira Maria.







All the contents on this site are copyrighted ©.