Japan na Tanzania zatiliana sahihi kwenye mikataba ya sekta ya umma na sekta binafsi!
Tanzania imetiliana mkataba wa ujenzi wa kituo cha kuzalisha umeme wa mabilioni
ya fedha na Kampuni ya Sumitomo Corporation ya Japan ikiwa ni moja ya miradi ya kwanza
na mikubwa kutekelezwa chini ya Ushirikiano wa Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP).
Sherehe za utiaji saini huo zimefanyika Ijumaa, Mei 31, 2013 mjini Tokyo, Japan na
kushuhudiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete ambaye
anatembelea Japan.
Katika sherehe hizo zilizofanyika kwenye Makao Makuu ya
Sumitomo Corporation yenye ghorofa 39, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt.
Servacius Likwelile ametia saini kwa niaba ya Serikali ya Tanzania wakati Ofisa Mtendaji
wa Kampuni Sumitomo Bwana Msayuki Hyodo ametia saini kwa niaba ya kampuni hiyo, moja
ya makampuni makubwa zaidi katika Japan.
Kwa upande wa Sumitomo Corporation,
Rais na Mtendaji Mkuu wa Kampuni hiyo, Bwana Kanuharu Nakamura ameshuhudia utiaji
saini mkataba huo ambako kituo cha kuzalisha megawati 240 zitajengwa katika eneo la
Kinyerezi mjini Dar es Salaam kwa gharama ya sh. bilioni 675.
Katika mradi
huo mkubwa, Sumitomo Corporation inashirikiana na makampuni mengine ya Japan ambayo
ni pamoja na Benki ya Maendeleo ya Japan (JBIC), Kampuni ya Bima ya Nippon (NEXI)
na Benki ya Sumitomo Mitsui Banking Corporation (SMBC), moja ya makampuni tanzu ya
Sumitomo.
Akizungumza katika sherehe hiyo, Rais Kikwete ameishukuru Kampuni
ya Sumitomo kwa kuonyesha imani yake kwa Tanzania kwa kuwekeza katika uchumi wake.
Pia ameeleza jinsi gani Sumitomo ilivyochangia katika kuokoa maisha ya Waafrika kwa
kuwekeza katika Kiwanda cha Kutengeneza Nguo za A-Z mjini Arusha ambako mpaka sasa
vyandarua milioni 30 vimetengenezwa na kusambazwa katika Afrika nzima.
Kwenye
sherehe hiyo pia Rais Kikwete ameshuhudia utiaji saini wa Makubaliano ya Ushirikiano
kati ya Sumitomo Corporation na Kampuni binafsi ya Tanzania, Quality Garage Limited.
Mwenyekiti na Mtendaji Mkuu wa Quality Garage, Bwana Yusuf Manji ametia saini kwa
niaba ya kampuni yake wakati Meneja Mkuu wa Mikakati ya Kimataifa na Uratibu, Bwana
Takechiyo Tanaka ametia saini kwa niaba ya Sumitomo.
Sumitomo imekuwa inafanya
biashara kwa miaka 400 tokea ilipoanzishwa katika miaka 1600 kabla ya kuundwa rasmi
kwa Sumitomo Corporation mwaka 1919 na katika Afrika ina ofisi na shughuli katika
Tanzania, Afrika Kusini, Angola, Kenya, Madagascar na Ghana.
Wakati huo huo,
Rais amekutana na kufanya mazungumzo na uongozi wa Kampuni ya Biashara ya Marubeni,
kampuni nyingine kubwa ya Japan. Ujumbe wa Marubeni katika mazungumzo hayo kwenye
Hoteli ya Intercontinental mjini Yokohama umeongozwa na Bwana Akihiko Sagara, Mtendaji
wa Kampuni hiyo.
Marubeni ambayo ilianzishwa mwaka 1858 inafanya biashara ya
kiasi cha dola za Marekani bilioni 112 kwa mwaka ikiwa na mali zenye thamani ya dola
bilioni 63 na faida ya bilioni 2.2 kwa mwaka. Ina ofisi 120 nje ya Japan katika nchi
65.
Rais ambaye yuko Japan katika ziara ya kikazi ya siku saba ni mmoja wa
viongozi wengi za Afrika ambako wamealikwa kuhudhuria Mkutano wa Tano wa Tokyo Kuhusu
Maendeleo ya Afrika (TICAD – V) huko mjini Yokohama.