2013-05-31 11:08:12

Zaidi ya Wakristo 1,000 wanauwawa kila Mwaka sehemu mbali mbali za dunia!


Askofu mkuu Silvano Maria Tomasi Mwakilishi wa kudumu wa vatican kwenye Ofisi za Umoja wa Mataifa zilizoko mjini Geneva hivi karibuni ameonesha masikitiko na wasi wasi wa vatican kutokana na uvunjifu wa misingi ya uhuru wa kuabudu pamoja na madhulumu ya kidini wanayofanyiwa Wakristo: Barani Afrika, Asia na Mashariki ya Kati.

Tafiti za kuaminika zilizofanywa hivi karibuni zinabainisha kwamba, zaidi ya Wakristo 1,000 wanauwawa kila mwaka kutokana na chuki za kidini. Baadhi ya wakristo wamejikuta wananyanyasika kiasi cha kulazimika kuyakimbia makazi yao, hii inatokana na mashambulizi ya mara kwa mara pamoja na vitendo vya utekaji nyara wa viongozi wa Makanisa kama inavyojidhihirisha huko Mashariki ya Kati. Haya ni matokeo ya misimamo mikali ya kiimani, hali ya kutovumiliana, vitendo vya kigaidi na vile vya kibaguzi.

Askofu mkuu Tomasi anasema, katika Nchi za Bara la Ulaya ambamo Ukristo uliota mizizi na kukomaa kwa miaka mingi, sasa Wakristo wanabaguliwa na wala hawapewi tena fursa katika maisha ya hadhara kwa kubeza mchango mkubwa uliotolewa na Kanisa katika medani mbali mbali mbali za kijamii kiasi kwamba, hata huduma za Kijamii zilizokuwa zinatolewa na Kanisa kwa sasa zinaonekana hazifai tena!

Askofu mkuu Tomasi ameonesha masikitiko yake mbele ya Baraza la Haki Msingi za binadamu katika mkutano wake wa hivi karibuni. Umoja wa Mataifa unatambua na kuthamini mchango wa dini na tasaufi, mambo yanayochangia kwa namna ya pekee katika kulinda na kukuza utu na heshima ya binadamu, bila kusahau huduma ya upendo inayotolewa kwa watu mbali mbali, kwa ajili ya mafao ya wengi.

Kanisa Katoliki limekuwa mstari wa mbele katika utoaji wa huduma za kijamii katika sekta ya: elimu, afya, maendeleo, huduma kwa wakimbizi na watu wasiokuwa na makazi na kwamba, utu na heshima ya binadamu ni sehemu ya Mafundisho Jamii ya Kanisa, kwa kutambua kwamba, mwanadamu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na kwamba, huduma za kijamii zinatolewa bila ubaguzi wa kidini, kikabila au rangi ya mtu!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuheshimu uhuru wa kuabudu na kwamba, kila mtu anayo haki ya kushuhudia imani yake katika maisha ya hadhara. Mchango wa Kanisa katika maendeleo endelevu yanayomgusa mtu mzima: kiroho na kimwili hauna budi kuheshimiwa na kuthaminiwa.









All the contents on this site are copyrighted ©.