Yaliyojiri kwenye ziara ya Rais Kikwete nchini Japan
Japan imekubali kuangalia uwezekano wa kugharimia ukarabati na uboreshaji mkubwa wa
Reli ya Kati na pia imekubali kuwa mbia mkuu katika kuiwezesha Tanzania kuleta mageuzi
makubwa katika kilimo cha mpunga kwa nia ya kuzalisha mchele zaidi na kujitegemea
kwa zao hilo muhimu la chakula.
Serikali ya Japan imeeleza msimamo huo wa
kuisaidia Tanzania katika maeneo hayo baada ya kuombwa rasmi kufanya hivyo wakati
wa mazungumzo rasmi kati ya Tanzania na Japan kati ya Rais wa Jamhuri ya Muuungano
wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete na Waziri Mkuu wa Japan, Mheshimiwa Shinzo Abe.
Aidha,
Japan imeombwa na kukubali kuangalia uwezekano wa kugharimia ujenzi wa reli mpya kutoka
Tanzania kwenda nchi za Rwanda, Burundi na hatimaye Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo
(DRC). Tanzania pia imeiomba Japan kuwa mshirika kiongozi katika mageuzi ya kilimo
cha mpunga katika Tanzania ili kuwezesha kuongeza usalama wa chakula na hasa wa mchele
kwa Tanzania na majirani zake.
Tanzania vile vile imeiomba Serikali ya Japan
kuyashawishi makampuni makubwa ya nchi hiyo kuwekeza katika uchumi wa Afrika kwa sababu
Bara la Afrika linaendelea kuwa soko muhimu la bidhaa za viwandani za Japan. Maombi
hayo yametolewa Alhamisi, Mei 30, 2013 na Rais Kikwete wakati alipokutana na kufanya
mazungumzo rasmi na Mheshimiwa Abe, mjini Tokyo ikiwa sehemu ya shughuli za Rais Kikwete
katika ziara ya kikazi ya siku saba katika Japan.
Katika mazungumzo hayo ofisini
kwa Waziri Mkuu, Rais Kikwete ameiomba Japan kufikiria kuiunga mkono Tanzania kwa
kugharimia ukarabati na uboreshaji wa Reli ya Kati kutoka reli nyembamba ya sasa kuwa
reli ya kiwango kinachokubaliwa kimataifa. Aidha, Rais Kikwete ameiomba Japan kuangalia
uwezekano wa kugharimia ujenzi wa reli mpya kutoka Isaka, Tanzania kwenda Kigali,
Rwanda na hatimaye Burundi na DRC.
“Mheshimiwa Waziri Mkuu, reli yetu ya kati
ni nzee sana na tunataka kuboresha reli yenyewe kwa kuibadilisha na kuifikisha kiwango
cha kimataifa na pia kukarabati karakana zote muhimu za kuhudumia reli hiyo. Aidha,
tunashirikiana na Rwanda, Burundi na DRC kujenga reli mpya kwa sababu nchi zote hizi
zinategemea Bandari ya Dar es Salaam kupitisha mizigo yao,”
Ameongeza: “Tumekamilisha
upembuzi yakinifu na michoro kwa msaada wa Benki ya Maendeleo ya Afrika na kampuni
moja ya Barrington Santa Fe ya Marekani na sasa tunatafuta mbia wa kugharimia ujenzi
wake.”
Kuhusu uboreshaji wa kilimo cha mpunga, Rais Kikwete amemwomba Waziri
Mkuu Abe kuifanya Japan kuwa mbia kiongozi katika kilimo cha mpunga ili kuiwezesha
Tanzania kujitegemea kwa mchele na hata kuweza kulisha nchi za jirani. “Katika kilimo,
tunalenga kujitosheleza kwa mahindi na mchele. Tunao wabia wachache lakini tunataka
Japan iwe mbia kiongozi kwa sababu ya uzoefu wetu katika kilimo cha mpunga. Tunahitaj
kuongeza uzalishaji kwa sababu majirani zetu wanatutegemea.”
Kuhusu Serikali
ya Japan kuyashawishi makampuni binafsi ya nchi hiyo kuwekeza katika Afrika, Rais
Kikwete amesema: “Biashara kati ya Japan na Afrika inaongezeka na uwekezaji unaongezeka,
lakini tunaweza kufanya zaidi kwa sababu katika kila magari 10 kwenye barabara za
Afrika tisa yanatoka Japan. Maduka ya vifaa vya elekroniki yamejaa vifaa na vyombo
kutoka Japan – ziwe kamera, ziwe redio, ziwe televisheni lakini hayo makampuni mengi
ya Japan yanawekeza katika Afrika.”
Ameongeza Rais Kikwete: “Uwekezaji unatunufaisha
sana katika Afrika. Chukua mfano wa Kampuni ya Somitomo – imezalisha vyandarau
milioni 30 pale Arusha na ni vyandarua hivyo ambavyo vimepunguza malaria katika Afrika.
Tanzania kwenye malaria imepungua kwa kiasi cha asilimia 60 kwa sababu ya uwekezaji
huo.”
Rais pia ameiomba Serikali ya Japan kuisaidia kampuni hiyo ya Somitomo
kuwekeza zaidi katika uzalishaji umeme. Kwa sasa kampuni hiyo inashirikiana na Serikali
kuzalisha megawati 240 katika eneo la Kinyerezi, Dar Es Salaam.
Rais pia ameomba
Japan kuongeza nafasi za shahada ya juu ya PHD katika kufundisha madaktari wa Tanzania
na kusaidia kuongeza uwezo wa Tanzania katika matumizi ya mkongo wa taifa ambao Serikali
iliujenga.
Japan yatangaza mabilioni kusaidia Tanzania
Japan
imetangaza misaada na mikopo ya mabilioni ya fedha kusaidia uchumi na maendeleo
ya Tanzania ikiwa ni pamoja na kugharamia uboreshaji wa miundombinu, ujenzi wa miradi
ya barabara, ujenzi wa miradi ya maji, uanzishwaji wa skimu ndogo ndogo za umwagiliaji
na uboreshaji wa kilimo cha mpunga.
Waziri Mkuu wa Japan, Mheshimiwa Shinzo
Abe ametangaza hatua hizo za kuunga mkono jitihada za maendeleo za Tanzania wakati
alipokutana na kufanya mazungumzo rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jakaya Mrisho Kikwete.
Viongozi hao wawili wamekutana ofisini kwa Mheshimiwa
Abe, Alhamisi, Mei 30, 2013, mjini Tokyo kwenye siku ya pili ya ziara ya wiki moja
ya Rais Kikwete katika Japan ambako miongoni mwa mambo mengine amealikwa kuhudhuria
Mkutano wa Tano wa Kimataifa wa Kujadili Maendeleo ya Afrika wa Tokyo International
Conference on African Development (TICAD – V) unaoanza Yokohama, mji wa pili kwa ukubwa
katika Japan, Jumamosi, Juni Mosi hadi 3, 2013 na kuhudhuriwa na viongozi wa nchi
za Afrika na washirika wa maendeleo wa Bara hilo.
Miongoni mwa miradi ambayo
Japan imekubali kugharimia ambayo baadhi yake inaendelea kujengwa ama karibu inaanza
kutekelezwa ni pamoja na Mradi wa Maji wa Mkoa wa Tabora, Mradi wa Kuboresha Usafiri
katika Mkoa wa Dar Es Salaam ambao ni pamoja na kupanuliwa kwa Barabara ya Gerezani
na Ujenzi wa Daraja Jipya kwenye barabara hiyo, Mradi wa Kuendeleza Kilimo cha Mpunga
nchini na Mradi wa Awamu ya Pili ya Kuongeza Uwezo wa Serikali za Mitaa kwa Njia ya
Mafunzo.
Miradi mipya ambayo Japan itagharimia ni pamoja na Mradi wa Kuendeleza
Miundombinu, Mradi wa kujenga skimu ndogo za umwagiliaji, mradi wa ujenzi wa barabara
ikiwa ni pamoja na kugharimia ujenzi wa barabara katika milango ya kimataifa ya Mara,
Dodoma na Iringa na Mpango wa 10 wa Kuunga Jitihada za Kupunguza Umasikini.
Wakati
wa mazumgumzo hayo, Waziri Mkuu Abe pia ametangaza kuwa Japan itagharamia ujenzi wa
barabara za juu kwa juu (fly-overs) kwenye makutano ya barabara za TAZARA na Ubungo,
ujenzi wa mtambo wa kuchakata umeme wa Kinyerezi ambako unatekelezwa kwa mpango wa
Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPF).
Waziri Mkuu Abe pia ameitaka Tanzania
na Japan kukamilisha “haraka iwezekanavyo” majadiliano ya kufikiwa kwa makubaliano
ya kulinda uwekezaji kati ya nchi hizo mbili ili kufungua njia za uwekezaji zaidi
katika uchumi wa Tanzania kutoka Japan, moja ya mataifa tajiri zaidi duniani.
Mheshimiwa
Abe ameiomba Tanzania kuunga mkono jitihada za nchi hiyo kujiunga na Baraza la Usalama
la Umoja wa Mataifa (UN) chini ya mageuzi makubwa yanayotarajiwa kufanyika kwenye
mfumo wa Umoja huo.
Rais Kikwete alijibu ombi hilo la Mheshimiwa Abe kwa kusema:
“Mheshimiwa Waziri Mkuu tunaunga mkono moja kwa moja jitihada za Japan kujiunga na
Baraza la Usalama kama mwanachama mwenye kura ya turufu. Unajua msimamo wetu kuhusu
jambo hili siku nyingi.”
Tanzania yaunga mkono ombi la Japan kuhusu Olimpiki
Tanzania
imesema kuwa itaunga mkono ombi na jitihada za Jiji la Tokyo katika Japan kuwa
mwenyeji wa Michezo ya Olimpiki ya mwaka 2020. Msimamo huo wa Tanzania umetangazwa
Alhamisi, Mei 30, 2013 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete
wakati alipokutana na kufanya mazungumzo rasmi na Waziri Mkuu wa Japan, Mheshimiwa
Shinzo Abe.
Katika mazungumzo yaliyofanyika ofisini kwa Waziri Mkuu wa Japan,
Mheshimiwa Abe aliiomba Tanzania kuiunga mkono katika jitihada zake kadhaa za kimataifa
ikiwa ni pamoja na kupata nafasi ya kuandaa Michezo ya Olimpiki mwaka 2020.
“Nina
maombi mawili kwako Mheshimiwa Rais…moja ni kwamba Jiji la Tokyo ni moja ya miji ambayo
inawania kuwa mwenyeji wa Michezo ya Olimpiki ya mwaka 2020. Tunaomba kuungwa mkono
na Tanzania na tunaomba usaidie tuweze kuungwa mkono na Afrika,” Mheshimiwa Abe amemwambia
Rais Kikwete.
Baada ya Mheshimiwa Abe kutoa ombi hilo, Rais Kikwete amesema:
“Tutaiunga mkono nchi ya Japan na Jiji la Tokyo kuweza kuandaa Michezo ya Olimpiki
mwaka 2020. Aidha, nataka kukuhakikishia kuwa tutatumia mahusiano yetu katika Afrika
kuwezesha kuungwa mkono kwa ombi hilo la Japan.” Jiji la Tokyo ni miongoni mwa miji
mitatu duniani ambayo imevuka hatua ya kwanza kutoka mji iliyoomba (applicant cities)
na kuwa mji inayoweza kuandaa Michezo ya Olimpiki (candidate cities). Miji mingine
miwili ni Madrid (Hispania) na Istambul (Uturuki).
Kabla ya hatua hiyo, miji
mitano ikiwamo Tokyo, Madrid na Istambul pamoja na Baku (Azerbaijan) na Doha (Qatar)
ilikuwa imeomba kuandaa Michezo hiyo kabla ya idadi yao kupungua Mei 25, 2012. Uteuzi
wa mwisho wa Mji ambao utandaa Michezo hiyo utatangazwa kufuatia kikao cha 125 cha
Kamati ya Utendaji ya Kamati ya Olimpiki Duniani (IOC) kilichopangwa kufanyika Septemba
7, 2013 mjini Buenos Aires, Argentina. Tokyo mara ya mwisho iliandaa Michezo ya Olimpiki
mwaka 1964.