2013-05-31 14:53:31

Umoja wa Mataifa waipongeza Vatican kwa kusimama kidete kulinda na kutetea mafao ya wengi, utu na heshima ya binadamu!


Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 31 Mei 2013 amekutana na kuzungumza na Rais wa Baraza la Umoja wa Mataifa Bwana Vuk Jeremic, ambaye alikutana pia na Kardinali Tarcisio Bertone, Katibu mkuu wa Vatican na Askofu mkuu Dominique Mambert, katibu mkuu wa mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican.

Baba Mtakatifu pamoja na mgeni wake wamejadili mambo yenye uzito wa juu katika medani za kimataifa hasa jitihada za kutafuta suluhu ya migogoro na kinzani za kimataifa kwa njia ya amani badala ya kukimbilia kwenye mtutu wa bunduki kama hali inavyojionesha Mashariki ya Kati. Eneo hili kwa sasa linakabiliwa na hali tete pamoja na mahangaiko ya watu wasiokuwa na hatia, changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika kuanzisha mchakato wa upatanisho miongoni mwa jamii sanjari na majadiliano ya kidini.

Viongozi hawa wawili wamejadili kwa kina na mapana kuhusu biashara haramu ya binadamu na hali tete inayoendelea kuwakabili wakimbizi na watu wasiokuwa na makazi huko Mashariki ya Kati. Baraza la Umoja wa Mataifa linaweza kutoa mchango mkubwa katika kukabiliana na athari za myumbo wa uchumi kimataifa sanjari na utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Millenia ifikapo mwaka 2015 kwa kukazia utunzaji bora wa mazingira pamoja na kupunguza pengo kati ya maskini na matajiri.

Umoja wa Mataifa umeipongeza Vatican kutokana na mchango wake katika Jumuiya ya Kimataifa kwa kusimama kidete kutafuta kwanza kabisa mafao ya wengi na kwamba, Kanisa limechangia kwa kiasi kikubwa katika ustawi na maendeleo ya watu sehemu mbali mbali za dunia. Huu umekuwa ni utambulisho wa Kanisa Katoliki katika utoaji wa huduma zinazopania kumwendeleza mwanadamu; kwa kulinda na kutetea utu na heshima yake; kwa kusimama kidete kulinda na kutetea amani bila kusahau kujenga utamaduni wa majadiliano; tunu msingi katika mikutano ya Baraza la Umoja wa Mataifa.







All the contents on this site are copyrighted ©.