2013-05-31 08:42:18

Sinodi ya kwanza ya Jimbo kuu la Tabora inapania kuwaimarisha waamini katika Imani yao kwa Kristo na Kanisa lake!


Maadhimisho ya Mwaka wa Imani uliotangazwa na kuzinduliwa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, imekuwa ni fursa muhimu kwa Familia ya Mungu Jimbo kuu la Tabora, Tanzania, kuadhimisha Sinodi ya Jimbo kuu la Tabora itakayohitimishwa wakati wa Maadhimishoya Siku kuu ya Yesu Kristo Mfalme wa Ulimwengu sanjari na kufunga Mwaka wa Imani. RealAudioMP3

Katika mahojiano maalum na Radio Vatican, Askofu mkuu Paul Ruzoka wa Jimbo kuu la Tabora anafafanua kwamba, Jimbo kuu la Tabora linaendelea kufanya tafakari ya kina kuhusu misingi ya imani kwa kuchambua na kufanya tafakari ya kina kuhusu vipengele hivi katika maisha na utume wa Kanisa. Maadhimisho ya Mwaka wa Imani yanaboreshwa kwa kutembezwa Msalaba wa Jubilee Kuu, utakaoanza kuzungushwa Jimboni Tabora kuanzia tarehe 2 Juni 2013. Lengo la kutembeza Msalaba wa Jubilee kuu ni kuwawezesha waamini kumshuhudia Kristo katika maisha yao ya hadhara.

Askofu mkuu Ruzoka anabainisha kwamba, Yesu yuko tayari daima kuwavuta wote kwake kwa kufungua mikono yake; yuko tayari kuwaondolea dhambi zao kwa kuinamisha kichwa chake pembeni na yuko tayari kuwapokea na kuwahifadhi katika Moyo wake Mtakatifu. Pale ubavuni palipotobolewa kwa mkuki, hapo pamekuwa ni chemchemi ya Sakramenti za Kanisa na maisha mapya!

Wakati wote wa kutembeza Msalaba wa Jubilee kuu, waamini watapata nafasi ya kusali na kuungama imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Hivi ndivyo Familia ya Mungu Jimbo kuu la Tabora inavyoadhimisha Mwaka wa Imani!







All the contents on this site are copyrighted ©.