2013-05-31 11:33:09

Kanisa Katoliki linapenda kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kidini ili kujenga na kuimarisha urafiki, udugu na haki msingi za binadamu!


Padre Miguel Angel Ayuso Guixot, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini yuko nchini Uturuki ili kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kidini kati ya Wakristo na Waislam. Huu ni mwendelezo wa mkataba uliotiwa sahihi kunako mwaka 2002 kati ya Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini na Serikali ya Uturuki ili kuendeleza uhusiano mwema kati ya waamini wa dini hizi mbili.

Kwa pamoja waamini wanaalikwa kusimama kidete kulinda na kutetea uhuru wa kuabudu; Mafundisho tanzu ya imani zao, uhuru wa dhamiri pamoja na kukuza malezi na majiundo ya maisha ya kiroho na malezi kwa vijana. Ni mchakato unaopania kwa namna ya pekee, kuendeleza ushirikiano wa karibu katika sekta ya elimu kwa kuweka utaratibu na kanuni ambazo zitasaidia vyuo na taasisi za kidini kuweza kushirikiana.

Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, katika hija yake ya kichungaji nchini Uturuki kunako tarehe 28 Novemba 2006 alibainisha umuhimu wa nchi ya Uturuki katika maisha na utume wa Kanisa, kwani hapa ni mahali ambapo Jumuiya nyingi za Kanisa la mwanzo zilianzishwa; ni nchi ambayo ina utamaduni wa hali ya juu wa dini ya Kiislam unaojionesha katika: Fasihi, Sanaa pamoja na Taasisi mbali mbali zilizopo.

Itakumbukwa kwamba, Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili alitembelea nchini Uturuki kunako mwaka 1979. Majadiliano ya kidini ni muhimu sana miongoni mwa Wakristo na Waislam, ili kujenga na kudumisha urafiki; haki, amani, upendo na mshikamano miongoni mwa Jamii. Huu ndio msimamo unaofanyiwa kazi pia na Baba Mtakatifu Francisko, kama alivyobainisha wakati alipokutana na viongozi wawakilishi wa dini mbali mbali hapo tarehe 20 Machi 2013.







All the contents on this site are copyrighted ©.