2013-05-31 08:45:37

Ekaristi Takatifu ni kielelezo makini cha ufuasi wa Kristo, Umoja na Mshikamano wa upendo!


Ufuasi, umoja na kushirikishana ni maneno makuu matatu yaliyoongoza mahubiri ya Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Maadhimisho ya Siku kuu ya Ekaristi Takatifu mjini Roma; ibada ambayo imefanyika kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano na kuhudhuriwa na bahari ya watu, iliyoshiriki pia katika Maandamano ya Ekaristi Takatifu, hadi kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu, lililoko mjini Roma.

Baba Mtakatifu anasema kwamba, Yesu alikuwa kati kati ya umati mkubwa watu waliokuwa wamemzunguka, akiwakaribisha na kuzungumza nao; akiwatibu na kuganga matatizo yao, kwa njia hii aliowafunulia huruma ya Mungu. Kati ya kundi kubwa hili la wafuasi wake, Yesu aliamua kuchagua wafuasi kumi na wawili kuwa ni mitume wake, ambao wangeshiriki kwa ukaribu zaidi katika kumwilisha mafundisho yake katika uhalisia wa maisha ya watu duniani. Yesu alikuwa anazungumza na kutenda katika mwelekeo mpya; akionesha ukweli, mamlaka pamoja na kuwamegea watu matumaini yaliyokuwa yanabubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu, wakamshukuru Mungu kwa matendo haya makuu.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, bahari ya watu iliyofurika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano ni kielelezo cha watu wanaotaka kumfuasa Yesu, ili kumsikiliza na hatimaye, kujenga umoja kwa njia ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, ili kusindikizana katika hija ya maisha, kwa kutambua kwamba, Yesu ni mwenza amini wa safari ya maisha.

Katika ukimya unaojionesha kwenye Sakramenti Kuu, Yesu anaendelea kuzungumza na wafuasi wake, akiwachangamotisha kutoka katika ubinafsi wao na kuanza safari ya kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya wengine.

Baba Mtakatifu anasema kwamba, kutokana na uwepo wa umati mkubwa wa watu na mazingira yaliyokuwepo, Mitume waliingiwa na hofu kiasi cha kumwomba Yesu aweze kuwatawanya watu waliokuwa wamemzunguka ili waende mjini kujitafutia mahitaji yao msingi. Kwa mitume hii ndiyo iliyokuwa njia ya mkato kwa matatizo ambayo yangeweza kujitokeza, kishawishi ambacho kimeendelea pia kujionesha katika maisha ya wakristo.

Lakini, Yesu hakatishwi tamaa na mawazo yanayotolewa na Mitume wake, anawataka wao wenyewe kuwapatia chakula, jambo ambalo liliwashangaza kwani pale kulikuwa na mikate mitano na samaki wawili tu! Baada ya kuwateketisha watu, akachukua mikate na wale samaki wawili akainua macho yake juu mbinguni, akashukuru, akawabariki na kuwapatia Mitume ili waweze kuwaandalia watu. Hiki kikawa ni kipindi kilichoonesha umoja kati yao na watu wakashibishwa kwa Neno la Mungu kwani walikuwa wamelishwa ule Mkate wa Uzima wa Milele.

Baba Mtakatifu Francisko amewakumbusha waamini waliokuwa wanashiriki Ibada ya Misa Takatifu katika Maadhimisho ya Siku kuu ya Ekaristi Takatifu kwamba, hata wao waliokuwa wamekusanyika kuzunguka meza ya Bwana, Sadaka ya Fumbo la Ekaristi Takatifu inayoendelea kutolewa Altareni, wakati wa Maadhimisho ya Sadaka ya Misa Takatifu.

Kwa kusikiliza Neno la Mungu na kulishwa kwa Mwili na Damu yake Azizi, anawajalia waamini kuwa kweli ni Jumuiya inayojitambulisha katika Umoja, kwani Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya Umoja, inayowawezesha waamini kutoka katika ubinafsi wao ili kuishi na kushiriki kikamilifu ule ufuasi na imani kwa Kristo. Huu ni mwaliko kwa waamini kujiuliza swali la msingi jinsi ambavyo wanajitahidi kuliishi Fumbo la Ekaristi Takatifu kwa kushikamana na Kristo pamoja na jirani zao.

Baba Mtakatifu Francisko akigusia kuhusu umuhimu wa kushirikishana anabainisha kwamba, unatokana na mahitaji yaliyojionesha kwa wakati ule, kwa kugawana hata kile kidogo walichokuwa nacho na kwa njia hii, Yesu mwenyewe aliweza kutenda miujiza, licha ya kuonesha umaskini na utupu wao wa ndani.

Neno la msingi linalopaswa kuzingatiwa ni mshikamano wa upendo unaowawezesha watu kutoa kile walichokirimiwa na Mungu kwa kugawana na wengine, kwani kwa kutekeleza zawadi hii, maisha yao yatauhishwa na kuzaa matunda. Inasikitisha kuona kwamba, neno mshikamano linaangaliwa kwa "makengeza" na baadhi ya watu katika Jamii.

Baba Mtakatifu anasema, Yesu anaendelea kugawa Fumbo la Mwili na Damu yake Azizi, ili kuonja mshikamano endelevu wa Mungu na binadamu; mshikamano ambao unaendelea kuwashangaza watu. Mwenyezi Mungu amejifanya kuwa mwenza wa maisha kwa njia ya Sadaka yake Msalabani; akawakirimia wafuasi wake zawadi ya maisha inayovuka na kushinda ubaya, ubinafsi na kifo.

Yesu anaendelea kujitoa katika Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, akishirikiana na wafuasi wake hija ya maisha, hata pale safari hii inapokuwa ni ngumu pamoja na kuwa na vikwazo vinavyowafanya kupunguza mwendo.

Ekaristi inawachangamotishwa waamini kufuata nyayo za Yesu kwa njia ya huduma shirikishi hata kwa kile kidogo walicho nacho kinachogeuka na kuwa ni utajiri mkubwa kwani nguvu ya Mungu ambayo ni upendo inawashukia katika umaskini wao na kuwageuza.

Hii ni changamoto ya kumpatia Yesu nafasi ya kuweza kuwaletea wafuasi wake mabadiliko katika maisha kwa kujikita zaidi na zaidi katika ufuasi, umoja na kushirikishana.

Mara baada ya Ibada ya Misa Takatifu yalifuatia Maandamano ya Ekaristi Takatifu hadi kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu. Hapo waamini walipata nafasi ya kuabudu Sakramenti kuu na baadaye Baba Mtakatifu Francisko akawapatia baraka ya Ekaristi Takatifu.







All the contents on this site are copyrighted ©.