Yaliyojiri kwenye sakata la Bwana Absalom Kibanda!
Usiku wa Jumanne ya Machi 5 kuamkia Machi 6, 2013, Mhariri Mtendaji wa New Habari
(2006) Ltd, ambaye pia Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Absalom Kibanda
alivamiwa na kujeruhiwa vibaya akiwa nje ya lango la kuingilia nyumbani kwake Mbezi
Juu, Dar es Salaam.
Tukio hilo liliishtua na kutikisa taifa kwa kiwango kikubwa
si tu katika tasnia ya habari nchini, bali pia jamii kwa ujumla hasa baada ya aina
ya utekaji, utesaji na usiri uliotumika katika kufanikisha uhalifu huu kufanana kwa
karibu na tukio lilomkuta Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madkatari Tanzania, Dk. Stephen
Ulimboka lililotokea karibu miezi tisa kabla ya tukio la Kibanda yaani, usiku wa Juni
26, 2012.
Ukiacha matukio hayo, miezi sita kabla ya Kibanda kutekwa na kuteswa
Mwandishi Daudi Mwangosi, aliuawa akiwa mikononi mwa vyombo vya dola Septemba 2, 2012
huko Nyololo, Iringa akiwa kazini. Tukio la Kibanda limekuwa na sura ya mwendelezo
wa mauaji au utesaji wa wanahabari, hasa ikitiliwa maanani kuwa Mwandishi Issa Ngumba
(45) wa Radio Kwizera aliyekuwa anafanyia kazi zake katika Wilaya ya Kakonko, Kigoma,
Januari mwaka huu, alipigwa risasi na kuuawa katika mazingira ya kutatanisha.
Kama
hiyo haitoshi, tukio la kutekwa na kudhuriwa kwa Kibanda limetokea mwezi mmoja tu
baada ya Mwandishi wa Gazeti la Tanzania Daima, Shaaban Matutu kupigwa risasi na polisi
akiwa nyumbani kwake Dar es Salaam kwa maelezo kuwa kimakosa polisi walidhani Matutu
ni jambazi.
Mazingira ya kutekwa na kuumizwa kwa Kibanda yalitia wasiwasi kuwa
upo uwezekano, na dalili zilionyesha kwamba waliofanya kitendo hicho cha kinyama hawakuwa
wezi wala majambazi kutokana na ukweli kwamba licha ya kuwa na fedha zipatazo shilingi
milioni tatu taslimu ndani ya gari, laptop, simu tatu za gharama (ipad, iphone na
Blackberry), watekaji hawa hawakuchukua chochote baada ya kukamilisha uhalifu wao.
Kibanda
aliumizwa kwa kiwango kikubwa. Alitobolewa jicho la kushoto, akaumizwa vibaya kichwani
kiasi cha kusababisha kuvunjika kwa baadhi ya mifupa ya kichwa. Aling’olewa meno
mawili na kucha mbili, tena bila gazi. Watekaji hawa, katika unyama wa ajabu kabisa,
walimkata pingiri ya kidole cha pete chini ya kucha na kuondokana nayo.
Hali
hiyo iliibua maswali mengi, watu wengi wakajiuliza na kutafuta sababu za kutekwa na
kuumizwa kwa Kibanda kiasi hiki. Kutokana na kuwapo kwa maelezo mengi yanayotofautiana
kuhusu tukio hilo, ikabidi Jukwaa la Wahariri Tanzania lifanye uamuzi.
Katika
kikao cha Machi 8, 2013 Jukwaa la Wahariri Tanzania liliunda TIMU ya watu watano na
kuipa hadidu rejea za kufanya uchunguzi wa kihabari juu ya shambulio hilo kubaini
limetokana na nini. Timu hiyo iliundwa kufuatia uamuzi wa Jukwaa la Wahariri kufanya
uchunguzi huo na baada ya kukubalika kwa ombi la ruzuku ya kufanya uchunguzi huo wa
kihabari kutoka Mfuko wa Vyombo Vya Habari Tanzania (TMF).
Ruzuku ya TMF ililenga
kiujumla kutumia tukio la Kibanda kuwa chanzo cha kutengeneza mazingira salama zaidi
kwa waandishi na wahariri na kwamba kiwango cha matukio ya kuteswa, kupigwa na kuuawa
kwa waandishi yanapungua kila mwaka.
Timu hii imefanya kazi usiku na mchana
kwa kwa zaidi ya mwezi. Timu imezungumza na wadau 26. Kati ya hawa yumo Kibanda mwenyewe,
mke wake, ndugu zake, wasaidizi wake, waajiri wake wa zamani na wa sasa, viongozi
wa kisiasa na vyombo vya dola kutafuta ukweli wa jambo hili. Pia tumesoma matamko
na habari zilizochapishwa kwenye mitandao ya kijamii na magazeti ya kati ya Machi
5, 2012 na Aprili 5, 2012 kwa nia ya kufanya ulinganishi wa taarifa tulizozipata kutokana
na uchunguzi na habari zilizochapishwa baada ya kutekwa kwake. Vyombo vya dola
akiwamo Waziri mwenye dhamana walikataa kuhojiwa wakisema kuna tume ya serikali inayofanya
kazi hiyo na kwamba kuhojiwa kungeonyesha kutokuwa na imani na tume hiyo. Leo tunawasilisha
muhtasari wa ripoti hii. Ripoti kubwa pamoja na viambatanisho vyake, itachapishwa
na kuwekwa katika kitabu kimoja. Utaratibu mwingine wa kuchapisha habari ambazo hazijachapishwa
kuhusiana na tukio hili (untold stories) pia utaandaliwa kwa ushirikiano na Jukwaa
la Wahariri kwa nia ya kuieleza jamii maajabu juu ya kadhia hii.
Tulipewa Hadidu
Rejea ziafuatazo:-
HADIDU REJEA: 1. Kuchunguza mazingira ya kabla na
baada ya tukio la kushambuliwa kwake. Kabla ya kushambuliwa kwa maana ya kufahamu
kama kulikuwa na viashiria vyovyote vinavyoelekea kuwapo kwa mipango ya mashambulizi
dhidi yake.
2. Kuchunguza mazingira ya tukio lenyewe kwa kujikitika katika
mwenendo wake hasa siku nzima ya Jumanne Machi 5, 2013. 3. Kuangalia mazingira
ya kazi ndani ya Kampuni ya New Habari (2006), Ltd na nje ya kampuni hiyo kwa kumulika
sababu za kuhama kwake kutoka Free Media mwishoni mwa mwaka jana na kuhamia New Habari. 4.
Kuchunguza jambo jingine lolote linaloweza kutoa mwanga wa sababu za kuvamiwa na kupigwa
kwa Kibanda. 5. Kuchunguza mazingira ya sasa ya kazi kwa wanahabari na kupendekeza
hatua za kuchukua kutokana na kile kitakachobainika.
YALIYOJIRI KATIKA UCHUNGUZI:
Kuchunguza
mazingira ya kabla na baada ya tukio la kushambuliwa kwake. Kabla ya kushambuliwa
kwa maana ya kufahamu kama kulikuwa na viashiria vyovyote vinavyoelekea kuwapo kwa
mipango ya mashambulizi dhidi yake.
Timu ya uchunguzi ilitumia muda
mwingi katika eneo hili, kubaini iwapo kulikuwapo viashiria, sababu au matukio ya
wazi yenye mwelekeo wa kujitokeza kwa shambulio hili. Tuliangalia pia iwapo wapo watu
au makundi yaliyokwishapata kuonyesha ishara kwa matendo au kwa kauli juu ya uwapo
wa nia hii. Uchunguzi umebaini kuwa kuliwapo viashiria vingi, isipokuwa Kibanda au
watu wake wa karibu hawakupata kufikiri kuwa huenda vingeweza kuleta madhara makubwa
kiasi hiki kama ifuatayo:-
Wiki tatu kabla ya Kibanda kuvamiwa, kutekwa na
kuumizwa, gari la polisi aina ya gofu Na PT 180 liliwafuatilia kwa muda mrefu Absalom
Kibanda na Ofisa Mtendaji Mkuu wa New Habari (2006) Ltd, Hussein Bashe likiwa limeegeshwa
nje ya ofisi zao Sinza Kijiweni na baadaye likawafuatilia hadi Sinza Makaburini, ambapo
walisimamisha magari yao na kuzungumza na polisi hao waliosema walikuwa wanatilia
shaka magari yao. Baada ya kuzungumza kwa muda polisi waliondoka.
1.2. Usiku
wa Februari 25, mwaka huu majira ya saa 09:00 usiku, Kibanda walivamiwa na watu walioingia
kwenye uzio wa nyumba yao wakavunja kioo cha gari analotumia, lakini kioo kilipovunjwa
‘alarm’ ilipiga kelele, Kibanda akatoka nje na watu hao wakakimbia.
1.3. Kutokana
na uvamizi huo, Kibanda na wapangaji wengine katika nyumba zilizopo kwenye uzio mmoja,
waliona hatari ya kuvamiwa hivyo wakaanza mazungumzo na kampuni ya Ulinzi ya Kiwango,
iliyowataka kufunga kamera za usalama na kuweka walinzi watano. Hadi Kibanda anatekwa,
walikuwa hawajahitimisha mazungumzo na kampuni hii ya Kiwango.
1.4. Kuna askari
anayefanya kazi Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) miezi minane kabla alipata kumpa
Kibanda taarifa za kinteligensia, kuwa kulikuwapo mpango wa kumteka na kumuumiza.
Taarifa kama hizo pia alipewa na wasamaria wanaofanya kazi katika Jeshi la Polisi.
Kwa maneno yake Kibanda alisema:
“Kuna rafiki yangu askari wa Jeshi la Wananchi
Tanzania (JWTZ), kama miezi minane au tisa hivi aliwahi kuniambia ‘unaandika sana
usidhani kama watu wanakupenda. Chukua tahadhari hasa unapofika getini nyumbani kwako’.
Tangu wakati huo nimekuwa nikichukua tahadhari sana.
“Wiki mbili kabla ya tukio,
niliwahi kuhisi kitu kama hicho [cha kuvamiwa] nikiwa getini. Nilipiga honi wakachelewa
kuja kunifungulia, niliogopa sana. Hata nilipoingia ndani nilikuwa nimekosa raha kabisa.
“Pia
kuna rafiki zangu polisi waliwahi kuniambia kwamba ninatafutwa na kwamba watu wananifuatilia
na ikibidi wanitengenezee ajali au kunifanyia kama Ulimboka au Kubenea.”
1.5.
Ndani ya miezi mitatu mbele ya mlango wa ofisi yake Kibanda (Free Media Limited) ilikuwa
mara kwa mara muda wa asubuhi anapofika ofisini anakuta damu. Haikufahamika kama damu
hiyo ilikuwa ni ya binadamu, kuku, ng’ombe, kunguru au mbuzi, bali waliipuuza wakidhani
ni masuala ya ushirikina. Mhariri Mtendaji wa sasa, Ansbert Ngurumo, amethibitisha
kuwapo kwa tukio hilo.
1.6. Mfanyakazi mwandamizi wa Kampuni ya New Habari
anakofanya kazi sasa Kibanda ndani ya wiki mbili kabla ya kutekwa na kuumizwa kwake
alipata kumwabia Kibanda maneno mazito mara tatu, na hapa tunamnukuhu Kibanda:
“Aliniambia
Danny Mwakiteleko [aliyekuwa Naibu Mhariri Mtendaji wa New Habari] hakufa kwa ajali,
bali alikufa kutokana na blood clotting (kuganda kwa damu). Hivyo ikitokea mtu ukapata
ajali au ukapigwa na kuumizwa sana sehemu za kichwa hivi au tumbo, ni lazima madaktari
wadhibiti sana blood clotting.
“Na kweli, nilivyoletwa hapa Milpark hospitalini,
madaktari walikuwa wananidunga sindano sita kila siku kwenye kitovu kuzuia blood clotting.
.... (jina linahifadhiwa) aliniambia maneno haya mara tatu, katika mazingira yasiliyotarajiwa
na kwa msisitizo ambao sikujua maana yake. Nasema .... (jina linahifadhiwa) naye achunguzwe
kwa kina. Inawezekana kuna jambo analijua.”
Ofisa huyu, alipishana dakika chache
na Kibanda muda wa kutoka ofisini baada ya kipindi cha kwanza cha mechi kati ya Real
Madrid na Manchester united kumaliza nusu ya kwanza (half time). Dakika ishirini baadaye
Kibanda alishambuliwa.
2.0. Kuchunguza mazingira ya tukio lenyewe
kwa kujikitika katika mwenendo wake hasa siku nzima ya Jumanne Machi 5, 2013.
2.1.
Familia ya Kibanda na Kibanda Mwenyewe hawakuwa na wasiwasi wowote siku hiyo kwani
hawakuwa na hisia wala wazo kuwa ungetokea uvamizi huo.
2.2. Kibanda alipopiga
honi, mlinzi alisogea langoni kumfungulia. Ghafla akasikia kishindo kikubwa. Akasikia
kelele za Kibanda akiomba msaada. Kijana huyu Baraka Ibrahim mwenye umri wa miaka
27, aliogopa. Aliogopa kwa mana hakuwa na silaha yoyote mkononi. Hakuwa na panga,
kisu, rungu, wala filimbi. Kwa maneno yake anasema:
“Nilivyoona ningefungua
geti hata mimi ningekufa, nilikimbia kuwaamsha majirani. Sikuwa hata na namba ya simu
ya mtu yeyote kati ya mabosi wangu ninaowalinda. Nilikuwa mimi tu, imani yangu na
Mungu wangu.... kutokana na maisha naifanya hivyo hivyo tu. Vinginevyo milele nisingefanya
kazi hii ya ulinzi.”
Mlinzi huyo alikimbilia kwa majirani katika nyumba aliyoamini
yumo mwanaume, lakini akaanza kumwamsha House Girl, ili house girl amwamshe baba mwenyenyumba.
Kitendo cha kuamshana na kuwapa taarifa kilichukua dakika tano hadi saba, na ndani
ya muda huo, Mlinzi anasema watekaji wa Kibanda walifanyafanya unyama na uasi huo
na kuondoka ndani ya muda mfupi kiasi hicho. “Watu hawa wana mafunzo maalumu,” anahitimisha.
2.3.
Mke wake alikwenda kazini asubuhi na kurejea nyumbani jioni, lakini tofauti na utaratibu
wake wa kawaida ambapo huwa anaangalia televisheni sebuleni hadi Kibanda anaporejea
nyumbani, siku hiyo alikwenda kuangalia televisheni akiwa chumbani na usingizi ukampitia.
Anasema hakusikia honi wala tukio la Kibanda kutekwa. “Hii inanitesa sana moyoni.
Najiuliza kwa nini siku hiyo tu sikukaa sebuleni? Kwa nini siku hiyo tu nimelala mapema
kabla Baba Joshua hajarudi (machozi yanamlengalenga). Najiuliza sipati jibu.”
2.4.
Mmoja kati ya wasaidizi wawili wa nyumbani kwa Kibanda, alisikia kelele za Kibanda
akiomba msaada. Alimwamsha mwenzake na kumwambia. “Nasikia Baba Joshua anapiga kelele
kama amevamiwa hivi.” Mwenzake alimwambia “Unaota maana kuna kelele za mpira.” Siku
hiyo kulikuwa na mechi kati ya Real Madrid na Manchester United.
Ni kweli zilikuwapo
pia kelele za wanaoshangilia mpira siku hiyo, hivyo Kibanda alipoomba msaada, hata
waliosikia walidhani watu wanashangilia mpira. Binti aliwaamsha Angela na mwenzake,
wakaenda sebuleni, wakakaa na kuchungulia dirishani, wakaona mwanga wa gari getini,
lakini baada ya kutosikia kelele yoyote wakarejea kulala wakidhani siye. Lakini binti
mmoja alibaki sebuleni. Baada ya muda jirani mmoja akampigia simu Angela kumweleza
kuwa mumewe ameshambuliwa.
2.5. Kibanda kwa upande wake, anasema alipofika
getini, alipiga honi, ghafla akaona watu wawili wamesimama pembeni mwa gari lake na
mtu wa tatu akiwa kwa mbali. Kisha akasikia kishindo kikubwa, akidhani wanataka kuiba
gari, aliatokea mlango wa abiria na kuanza kukimbia huku akiita. “Mama Joshua nisaidieeeeee.”
Katika
kukimbia, aliteleza akaanguka. Huku watesaji wake wakisema mara tatu “Afande piga
risasi.” Kibanda alijaribu kupambana, akashika rungu, akawahoji amewakosea nini hadi
wampige kiasi hicho, lakini hawakumjibu lolote. Waliendelea kumpiga, hadi akapoteza
fahamu. Hakujua jicho limetobolewa saa ngapi, meno yameng’olewaje na wala pingiri
ya kidole chake imekatawaje. Ifuatayo ni sauti ya Kibanda mwenyewe. Inasikitisha
ila tuwe wavumilivu na tuisikilize.
3.0. Kuangalia mazingira
ya kazi ndani ya Kampuni ya New Habari (2006) Ltd na nje ya kampuni hiyo kwa kumulika
sababu za kuhama kwake kutoka Free Media mwishoni mwa mwaka jana na kuhamia New Habari.
3.1.
Mazingira ya kazi ndani ya New Habari (2006) Limited na Freemedia Limited, yanaacha
maswali kadhaa yenye kustahili majibu. Kama ilivyoelezwa kwenye Hadidu Rejea Na: 1,
ndani ya kampuni ya New Habari imekuwapo misuguano isiyo na afya kwa kazi ya Kibanda
kama mwandishi na tasnia ya habari kwa ujumla.
3.2. Mazingira ya kazi ndani
ya Kampuni ya New Habari (2006) Ltd ni utata. Uhusiano katika chumba cha habari si
mzuri. Ndani ya kampuni hawaaminiani na imefikia hatua wanatuhumiana kuwa huenda baadhi
ya viongozi ndani ya New Habari wamehusika kumteka na kumuumiza Kibanda. Haya yameandikwa
ndani ya mitandao ya kijamii, ikidai kwamba kiongozi mmoja ndani ya kampuni hiyo alihusika
na utekaji wa Kibanda.
Mkurugenzi wa Uhariri, Prince Bagenda anasema waliohusika
kusambaza taarifa chafu dhidi ya kiongozi huyo wa New Habari wanatoka ndani ya kampuni
hiyo.
3.3. Timu ya uchunguzi ilibaini kuwapo mgawanyiko mkubwa ndani ya New
Habari (2006) Ltd kwa kuwapo kundi la ‘Habari Wazawa’ na ‘Habari wa Kuja’. Malalamiko
mengi yanajikita katika msingi kuwa ajira hazitangazwi na watu wanaajiriwa bila kuzingatia
sifa za kitaaluma.
3.4. Kibanda hakuhama Free Media kwa amani. Uchunguzi unaonyesha
kuwa miezi kadhaa kabla ya kuondoka kwake alianza kupoteza mamlaka. Mwenyekiti wa
Kampuni ya Free Media Ltd, Freeman Mbowe alianza kumsikiliza zaidi msaidizi wake ambaye
alikuwa Naibu Mhariri Mtendaji, Ansbert Ngurumo kuliko yeye Kibanda. Kwa maneno yake,
anasema: “Nilihofu kuwa Mbowe anaweza kutugombanisha. Nikaona ni bora niondoke
nisije nikagombana na Mbowe au Ngurumo.”
Anasema alianza kupoteza mamlaka yake
na kutoaminika kwa mwajiri wake baada ya kuandika makala kuhusu Abdulrahman Kinana
ambayo kabla ya kuiandika hakuwa na wazo la kuondoka. Yaliyofuata baada ya makala
hiyo, yalimshukuma aondoke.
4.0. Kuchunguza jambo jingine lolote
linaloweza kutoa mwanga wa sababu za kuvamiwa na kupigwa kwa Kibanda.
4.1.
Uchunguzi ulifuatilia masuala mbalimbali ikiwamo miendendo ya watu waliotajwa kwa
njia moja au nyingine kuhusinaa na tukio hili. Hata hivyo, karibu watu wote waliohojiwa,
akiwamo Kibanda mwenyewe aliyeumizwa walimtaja kwa kutilia shaka mwenendo wa kijana
Joseph Ludovick. Hofu yao, iliongezwa nguvu na maandishi aliyoyachapisha Ludovick
kwenye mitandano ya kijamii siku ya Machi 6, 2013.
4.2. Usiku aliotekwa na
kuumizwa Kibanda, Ludovick katika naye alidai kuwa ametekwa katika eneo la Shekilango
na kupelekwa hadi Kigogo. Baada ya kutekwa aliibiwa kila kitu, ikiwamo begi, laptop,
simu mbili, fedha taslimu Sh 35,000, akavuliwa nguo na kubaki na chupi tu. Pia alieleza
kuwa alitoa taarifa hizo kituo cha polisi Mabibo.
4.3. Maelezo ya Ludovick
yalitiliwa shaka na watu wengi hasa baada ya kuleeza kuwa watekaji walitumia muda
wa saa mbili kumtoa Shekilango hadi Mabibo, umbali ambao kwa kiwaida mwendo wake hauwezi
kuzidi dakika 10. 4.4. Daniel Chongolo aliiambia timu kuwa alfajiri ya Machi 6,
siku anayodai kutekwa Ludovick yeye alimuona eneo la Mabibo wakati anatoka Muhimbili.
Taarifa za polisi Mabibo zinaonyesha kuwa Ludovick alitoa taarifa polisi kuwa alikuwa
ametekwa ila akarudishiwa mali zake zote. “Alipouliza amefuata nini polisi, akawambia
kama raia mwema amefika kuandikisha kumbukumbu kwa nia ya kuonyesha kiwango cha uhalifu
kinavyoongezeka nchini,” kilisema chanzo chetu kituoni hapo. Timu ya uchunguzi iliamua
kutafuta taarifa hizo baada ya uongozi wa kituo hicho kukataa kupitia leja ya ripoti
ya Ludovick. 4.5. Pia taarifa za uchunguzi wa timu hii zinathibitisha kuwapo kwa
utata juu ya madai ya kuibwa kwa simu za Joseph Ludovick, kwani simu yake ya tigo
(inayodaiwa kuibwa) ilitumika saa 01:21 asubuhi siku ya Machi 6, 2013. Muda huu ofisi
za Serikali na Kampuni ya Tigo zilikuwa hazijafunguliwa
5.0. Kuchunguza
mazingira ya sasa ya kazi kwa wanahabari na kupendekeza hatua za kuchukua kutokana
na kile kitakachobainika.
5.1. Uchunguzi umebaini kuwa maisha ya wanahabari
yapo hatarini. Hatari hii inatokana na makundi mengi yenye masilahi kuwaona wanahabari
wanaosimamia ukweli kuwa maadui wa masilahi yao haramu. Kuna hatari kubwa inayowakabili
waandishi wakati nchi inapoelekea kwenye uchaguzi wa mwaka 2015.
5.2. Uchunguzi
umebaini kuwa usiri umepungua katika vyombo vya habari. Tofauti na zamani ambapo habari
nyeti ziliandikwa kwa kuhifadhi majina ya waandishi wakitumia jina la MWANDISHI WETU.
Simu hizi hata habari za kutisha waandishi wanaweka majina yao na hata wasipoweka,
ndani ya vyumba vya habari vingi waandishi wapo tayari kutaja nani ameandika habari
fulani.
5.3. Usaliti miongoni mwa waandishi wenyewe ndani ya vyumba vya habari
unazidi kuongezeka na usipodhibitiwa hali itazidi kuwa mbaya zaidi. Mwenyekiti wa
MOAT, Dk. Reginald Mengi anasema: “Hili ni jambo muhimu sana. Tuache usaliti vinginevyo
wengi wataumia.”
5.4. Pia alishauri waandishi wa habari kurejea katika msingi
wa taaluma, ambayo inawataka wao kuwa ndio wenye kuendesha vyombo vya habari badala
ya kutegemea matakwa ya wamiliki au makundi yenye masilahi binafsi.
6.0.
KILICHOBAINIKA: 6.1. Uchambuzi uliofanywa ni timu hii umebaini kuwa hoja nne zinazungumzwa
kuhusiana na kutekwa na kuumizwa kwa Kibanda. Hoja hizi ni:- (i) Kazi yake ya uandishi
wa habari (ii) Uhusiano wa kisiasa na vyama au wanasiasa mbalimbali (iii)Uhusiano
wa kijamii ikiwamo mapenzi (iv) Vitendo vya rushwa.
6.2. Timu imejiridhisha
kutokana na majibu ya wengi kuwa dhana ya mapenzi na rushwa, havina nafasi yoyote
katika tukio hili. Wote waliohojiwa walieleza pasi na shaka kwamba suala hili la kushambuliwa
na kuumizwa kwa kiwango kikubwa kwa Kibanda, halina uhusiano wowote na rushwa au mapenzi.
6.3.
Kutokana na yaliyotajwa hapo juu kazi yake na siasa vikiunganishwa vimechangia kwa
kiasi kikubwa kuvamiwa kwa Kibanda. Timu imebaini kuwa kuna kutupiana mpira kati ya
vyombo vya dola na vyama vya siasa. Mchezo huu mchafu unaweza ukawa mwanzo wa kuumizwa
kwa Kibanda na waandishin wengine.
6.4. Baadhi ya waliohojiwa walidai kuwa
utekaji huu umefanywa na vyombo vya dola ukiwa sehemu ya mpango mkakati wa vyombo
hivi kukihusisha Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na vitendo vya ugaidi.
6.5.
Wanayataja matukio ya Uchaguzi Mdogo wa Igunga, maandamano ya Morogoro na Mkanda anaodaiwa
kurekodiwa Mkurugenzi wa Usalama wa CHADEMA, Wilfred Lwakatare kuwa vililenga kukifanya
CHADEMA kichukiwe na Watanzania kwa kukitaja kama chama cha kigaidi ambacho kinateka
watu na kinawaumiza.
6.6. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe anadai kwamba
mpango kama huo vyombo vya dola viliutumia kwa NCCR Mageuzi vikakisambaratisha, Chama
cha Wananchi (CUF) kilisingiziwa udini kikapoteza mwelekeo na sasa vyombo hivyo vililenga
kukifanya CHADEMA kionekane cha kigaidi mbele ya macho ya jamii ndiyo maana imerekodiwa
mikanda kwa nia ya kuitumia kujenga hoja hiyo.
6.7. Wakati Mbowe akisema hayo,
baadhi ya watu waliohojiwa wanadai kuwa CHADEMA kimepewa mafunzo na ushauri kutoka
nje ya nchi kuwa kikitumia baadhi ya watumishi wa vyombo vya dola wasiokuwa waaminifu
kuteka, kuumiza na hata kuua baadhi ya watu maarufu nchini wakiwamo waandishi na wanasiasa,
basi wananchi wataamini kuwa Chama Cha Mapinduzi na Serikali yake kimeshindwa uongozi
na sasa kimeanza kazi ya kuua wanaowapinga.
6.8. Kwa njia hiyo, inaelezwa kuwa
hesabu za Chadema ni kuwa wananchi wataichukia CCM na Serikali yake na kukipa nafasi
ya kuingia madarakani. Hapa kauli ya Chadema kuwa NCHI HAITATAWALIKA itakuwa imetimia.
6.9.
Dhana nyingine iliyojitokeza ni kuwa wapo wafanyabiashara ambao wana vita binafsi,
hivyo wanaamua kuumiza watu wasiowaunga mkono katika mipango yao na hilo ndilo limemkumba
Kibanda, baada ya kuwa ameepusha mauaji ya mwandishi mmoja na aliyekuwa ameandaa mpango
wa kuua mwandishi huyo hakuridhika hivyo akaamua amshughulikie Kibanda.
7.0.
MAPENDEKEZO:
Baada ya Timu kupata taarifa hizi na nyingine nyingi, inapendekeza
yafuatayo:- 7.1. Taarifa hii ichukuliwe kama chanzo cha uchunguzi zaidi wa vyombo
husika. 7.2. Yanahitajika marekebisho makubwa na ya haraka katika mifumo ya uendeshaji
wa vyumba vya habari kwa nia ya kurejesha misingi ya uandishi wa habari inayokubalika.
7.3.
Usalama wa wanahabari unapaswa kupewa kipaumbele na wamiliki, wanahabari wenyewe na
jamii kwa ujumla. Hapa Timu inapendekeza yawepo mafunzo ya kuwawezesha wanahabari
kutambua viashiria vya hatari na kuchukua hatua mara moja.
7.4. Kwa kiwango
alichoumizwa Kibanda iwapo mwajiri wake asingejitolea kugharamia matibabu, hatujui
hatima yake ingekuwaje leo hii. Tunapendekeza taasisi na mifuko mbalimbali inayojihusisha
na masuala ya wanahabari kama Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) , Baraza la Habari
Tanzania (MCT), Mfuko wa Vyombo vya Habari Tanzania (TMF) na Umoja wa Klabu za Waandishi
wa Habari Tanzania (UTPC) kuanzisha mfuko wa pamoja utakaotumika kugharamia matibabu
ya waandishi watakaoumia wakiwa kazini.
7.5. Tukio la kutekwa kwa Kibanda limeonyesha
mwanga kuwa wahariri tumegawanyika mno. Habari zilizochapishwa katika magazeti mbalimbali
na mitandao ya kijamii zimeonyesha haja ya kuwafanya wahariri kuwa kitu kimoja kwa
kuondoa tofauti zao zisizo na masilahi kwa tasnia ya habari.
7.6. Kuna viashiria
vingi kuwa kuelekea mwaka 2015 matukio ya waandishi kuumizwa au kutekwa yanaweza kuongezeka
kutokana na wanasiasa na vyama kuwania madaraka huku wakitumia baadhi ya watumishi
katika vyombo vya dola. Kwa mantiki hiyo, vyombo vya habari na waandishi wa habari
wachukue tahadhari kuanzia sasa. 7.7. Taasisi za habari zifanye juhudi za makusudi
kukutana na vyama viwili vya siasa vya CCM na CHADEMA haraka iwezekanavyo, kuzungumzia
viashiria hivi vya hatari vinavyoelekea kuvuruga amani ya Tanzania.
8.0.
HITIMISHO:
Ni dhahiri kuwa kupigwa na kuteswa kwa Kibanda kumejiegemeza katika
siasa na kazi yake, hali inayofanya makundi muhimu kuchukua wajibu wa msingi. Kwa
upande wa Serikali ni muhimu kufuatilia viashiria katika taarifa hii kwa nia ya kupata
ukweli zaidi na kuchukua hatua stahiki za kisheria dhidi ya wahusika.
Na
kwa upande wa vyombo vya habari na taasisi za kihabari zinapaswa kutambua viashiria
vinavyohatarisha usalama wa waandishi wa habari na wahariri na kutengeneza mazingira
yatayokuwa salama zaidi kwa waandishi kufanya kazi zao.
9.0. SHUKRANI: 9.1.
Tunapenda kulishukuru Jukwaa la Wahariri Tanzania, kwa kufanya uamuzi sahihi wa kuwezesha
kufanyika kwa uchunguzi huu ulioanza kuonyesha mwanga wa nini kilitokea. 9.2. Tunapenda
kulishukuru Baraza la Habari Tanzania (MCT) kwa kushiriki kikamilifu na kuiwezesha
timu hii kwa Rasilimali Watu na Mali kufanikisha kazi hii.
9.3. Tunapenda kuwashukuru
Mfuko wa Vyombo vya Habari Tanzania (TMF) kwa uwezeshaji wa ruzuku, uliofanikisha
kufanya uchunguzi wa kihabari uliohusisha kwenda nchini Afrika Kusini kufanya mahojiano
na Kibanda. Uwezeshaji huo pia unahusisha kutengeneza mwongozo kwa waandishi wenye
lengo la kuwaepusha na hatari za kiusalama.
9.4. Tunawashukuru Kibanda, mkewe
Angela, wanafamilia, ndugu na jamaa wa Kibanda na wanahabari wote waliohojiwa kwa
ushirikiano mkubwa walioutoa kwa Timu hii.
9.5. Tunawashukuru wahariri wote
kila mtu kwa nafasi yake, kutokana na ushauri wa mara kwa mara mliotupatia katika
kufanikisha uchunguzi huu.
10.0. WAJUMBE WA TIMU: Timu hii iliundwa
na wajumbe watano ambalo ni: 1. Deodatus Balile – Mwenyekiti 2. Pili
Mtambalike – Mjumbe 3. Jane Mihanji – Mjumbe 4. Tumaini Mwailenge
– Mjumbe 5. Rashid Kejo – Katibu Mwisho.....