Wakatoliki jitokezeni kwa wingi kushiriki katika Maadhimisho ya Siku kuu ya Ekaristi
Takatifu!
Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili aliokuwa anaanza utume wake, aliwaalika waamini pamoja
na watu wote wenye mapenzi mema kutoogopa kumfungulia Yesu Kristo malango ya maisha
yao. Askofu mkuu Paul Ruzoka, Mwenyekiti wa Tume ya Haki na Amani ya Baraza la Maaskofu
Katoliki Tanzania katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema kwamba, hii ni
changamoto endelevu inayopaswa kufanyiwa kazi na waamini wa nyakati zote.
Waamini wanapaswa
kujitokeza kifua mbele kumshuhudia Kristo kwa njia ya maisha yao, kwani Yesu mwenyewe
amewaahidia wafuasi wake kwamba, mara atakapokuwa ameinuliwa juu atawavuta wote kwake.
Askofu mkuu Ruzoka anayasema yote haya wakati huu wa Maadhimisho ya Siku kuu
ya Ekaristi takatifu, Wakatoliki wanapoandamana katika mitaa na viunga vya miji yao
wakiwa na Ekaristi Takatifu, ili kuwaonesha watu kwamba, Kristo ni Bwana na Mungu
anayefanya hija ya maisha akiandamana na wafuasi wake katika uhalisia wa maisha.
Askofu
mkuu Ruzoka anawataka Wakatoliki mahali popote pale walipo kujitokeza kwa wingi kushiriki
katika Ibada ya Maadhimisho ya Siku kuu ya Ekaristi Takatifu pamoja na Maandamano
ya Ekaristi Takatifu, wakiwa na imani na matumaini kwamba, hatima ya maisha yao iko
mikononi mwa Kristo mwenyewe. Yeye atawalinda. Anawataka waamini pia kuwa macho na
watu wenye nia mbaya wanaotaka kuvuruga amani, utulivu na uhuru wa kuabudu, kwa kuwajengea
waamini hofu isiyokuwa na msingi.
Askofu mkuu Ruzoka anaitaka Serikali ya Tanzania
kuwa macho na vitisho vinavyoashilia kuvunjika kwa misingi ya haki, amani na uhuru
wa kuabudu. Kamwe Serikali isiruhusu wala kufumbia macho watu wachache wanaotaka kuvuruga
misingi ya amani na utulivu nchini Tanzania. "Leo hii wanawajengea waamini hofu ili
wasiende Makanisani, lakini kesho na kesho kutwa watanzania watahofia pia kwenda kazini"
matoke yake yanaweza kuwa na athari kubwa katika maisha, maendeleo na ustawi wa Tanzania.