2013-05-30 09:21:47

Ufunguzi wa Chuo Kikuu cha Madaba ni matunda ya mchakato wa maboresho ya sekta ya elimu Mashariki ya Kati


Kardinali Leonardo Sandri, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Makanisa ya Mashariki, kwa kushirikiana na viongozi wa Kanisa na Serikali ya Yordan, wanatarajia Siku ya Alhamis, tarehe 30 Mei 2013 majira ya jioni kufungua rasmi Chuo Kikuu cha Kikatoliki nchini Yordan kitakachojulikana kama "The American University of Madaba" na kitakuwa ni Chuo Kikuu Kishiriki cha Upatriaki wa Yerusalem.

Kukamilika na hatimaye kufunguliwa kwa Chuo Kikuu cha Madaba ni matunda ya harakati za kutaka kuboresha hali ya maisha ya wananchi huko Mashariki ya Kati kwa kuwekeza zaidi katika sekta ya elimu. Hizi ni juhudi za mchakato ulioanza takribani miaka 160 iliyopita, leo hii matunda yake yanaonekana. Ni Chuo Kikuu ambacho kina hadhi na ubora wa kimataifa unaopania kuwekeza miongoni mwa vijana kutoka Yordan kama kielelezo makini cha ujenzi wa majadiliano ya kidini katika uhalisia wa maisha, ili kudumisha misingi ya haki, amani na mshikamano kwa ajili ya mafao ya wengi.

Chuo Kikuu cha Madaba kilizindua majengo yake kunako mwezi Oktoba 2011. Hadi sasa kadiri ya taarifa iliyotolewa na Shirika la Habari za Kimissionari, FIDES zinaonesha kwamba, kuna jumla ya wanachuo 800 na kwamba, Chuo hiki kina uwezo wa kuchukua wanafunzi 8,000 kwa mkupuo. Upatriaki wa Yerusalem umechangia kwa kiasi kikubwa ujenzi wa Chuo Kikuu cha Madaba nchini Yordan.







All the contents on this site are copyrighted ©.