Tahadhari ya ugonjwa wa Nimonia inayotokana na Corona Virus
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii nchini Tanzania, imepokea taarifa kutoka Shirika
la Afya Duniani (WHO) mnamo tarehe 22 Mei 2013, kuhusu kuwepo kwa ugonjwa wa Nimonia
unaosababishwa na kirusi cha “Novel Coronavirus”.Taarifa hiyo inaeleza kuwa,tangu
ugonjwa huo utokee mwishoni wa mwaka 2012 hadi tarehe 23 Mei 2013 idadi ya wagonjwa
wapatao 44 na vifo 22 viliripotiwa
Shirika la Afya Duniani limethibitisha ugonjwa
huu kuwepo katika nchi za Mashariki ya Kati yaani Jordan, Qatar, Saudi Arabi na Falme
za Kiarabu (UAE). Katika bara la Ulaya, ugonjwa huu umethibitishwa kutokea nchi za
Ujerumani, Ufaransa, na Uingereza. Katika bara la Afrika, ugonjwa huu umetokea Tunisia.
Wizara
ya Afya na Ustawi wa Jamii inapenda kutoa tahadhari ya Ugonjwa huu kwa wananchi wote,
katika mikoa yote ya Tanzania na hasa wale wanaosafiri kuelekea maeneo tajwa yenye
uthibitisho wa ugonjwa huu.
Ugonjwa huu unaenezwa na kirusi kiitwacho “novel
coronavirus (nCoV).”. Dalili kuu za ugonjwa huu ni kushindwa kupumua kwa ghafla, homa
kali, kukohoa, na kubanwa na mbavu na hatimaye kupata Nimonia. Dalili nyingine ambazo
zinaweza kutokea ni pamoja na kupata maumivu makali ya tumbo pamoja na kuharisha.Vile
vile ugonjwa huu unaweza kupelekea figo kushindwa kufanya kazi na hata kusababisha
kifo. Kipindi cha kuonekana kwa dalili za ugonjwa huu ni kati ya siku 2 hadi 10 baada
ya kupata maambukizi. Ugonjwa huu hauna tiba wala chanjo.
Ugonjwa huu unaweza
kuambukizwa kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine. Njia za maambukizo bado hazijajulikana
ingawa uwezekano mkubwa wa maambukizo ni kwa kwa njia ya hewa (kukohoa/kupiga chafya)
au kwa kugusa majimaji/makamasi kutoka kwa mgonjwa aliyethibitishwa kuwa na ugonjwa
huo.
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, imechukua hatua zifuatazo katika kukabiliana
na tishio la ugonjwa huu:
·Kutoa taarifa ya tahadhari ya ugonjwa huu kupitia
kwa Waganga Wakuu wote wa Mikoa na Wilaya kwa Tanzania bara. Aidha, taarifa hii pia
imejumuisha namna mgonjwa anavyoweza kutambuliwa (Ainisho la Ugonjwa), “Fact sheet”
ya ugonjwa, Mwongozo kwa watumishi wa afya wa namna ya kuchukua sampuli ikiwa ni pamoja
na vipeperushi vinavyoelezea jinsi ya kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huu.
· Kuimarisha ufuatiliaji wa ugonjwa huu kupitia kwa Wataalamu wa Afya katika
Mikoa, Wilaya na maeneo ya mipakani. Aidha watalaamu hawa pia wanatoa elimu kwa wananchi
kuhusu dalili za ugonjwa huu na jinsi ya kujikinga na maambukizi ili endapo ugonjwa
huo utatokea uweze kutolewa taarifa mapema.
·Wizara inasisitiza kuwa hakuna
vikwazo vyovyote vilivyowekwa kwa ajili kwa wasafiri watakaokwenda au kurudi katika
maeneo tajwa yaliyothibitishwa kuwa na ugonjwa huu. Vipeperushi vya ugonjwa huu vimetumwa
katika maeneo ya mipakani ili iwapo msafiri anayeondoka au kurudi nchini akiwa na
dalili tajwa atoe taarifa kwa watumishi wa afya wa mpakani ili hatua stahili ziweze
kuchukuliwa.
·Kutoa mafunzo kwa watumishi wa afya na mipakani wa namna ya
kutambua na kujikinga dhidi ya maambukizo ya ugonjwa huu pamoja na uchukuaji wa sampuli
iwapo mgonjwa atapatikana
·Kupeleka vifaa kinga kwa ajili ya watumishi
wa afya
Wananchi wanashauriwa kutokuwa na hofu kwani mpaka sasa hakuna mgonjwa
yeyote aliyeripotiwa nchini. Wizara inapenda kutoa tahadhari kwa wananchi juu ya umuhimu
wa KUNAWA MIKONO VIZURI KWA SABUNI NA MAJI MARA KWA MARA na pia KUZUIA MDOMO NA PUA
KWA KITAMBAA AU KARATASI LAINI WAKATI WA KUKOHOA AU KUPIGA CHAFYA.
Pia wananchi
wanashauriwa kutoa taarifa kwenye kituo cha kutolea huduma za afya kilicho karibu
mara watakapoona mgonjwa yeyote atakayehisiwa kuwa na dalili za ugonjwa huu.
Imetolewa
na; Nsachris Mwamwaja Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali 30/05/2013