Mchakato wa haki na amani upewe msukumo wa pekee katika maisha na vipaumbele vya Kanisa!
Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la Haki na Amani anapenda kuwaalika
waamini na watu wpte wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, wanajitahidi kuwa ni wahudumu
na wajenzi wa haki na amani mahali wanapoishi na kufanya kazi, hasa wakati huu Kanisa
linapomshukuru Mungu kwa Jubilee ya miaka 25 tangu Mtandao wa Imani na Haki kati ya
Afrika na Ulaya ulipozinduliwa rasmi.
Kardinali Turkson ameyasema hayo wakati
wa Ibada ya Misa Takatifu iliyofanyika mjini Roma, kama sehemu ya Maadhimisho ya Jubilee
ya Miaka 25 tangu Mtandao huu ulipoanzishwa kunako mwaka 1988. Ni mtandao unaoyashirikisha
Mashirika 44 ya kitawa na kazi za kitume yanayotekeleza utume wake Barani Afrika na
Ulaya kama sehemu ya mchakato unaopania kuhamasisha uwiano sawa katika uhusiano wa
kiuchumi baina ya Afrika na Ulaya, ili wananchi wa Bara la Afrika waweze kufaidika
na matunda ya jasho lao.
Mtandao huu unatarajiwa kufanya kilele cha Maadhimisho
ya Jubilee ya miaka 25, Mwezi Novemba 2013 hapa mjini Roma kwa kuadhimisha Mkutano
mkuu unaotarajiwa kutoa msukumo na ari mpya ya matumaini miongoni mwa wananchi wa
Bara la Afrika.