2013-05-30 10:12:03

Hakuna Ukristo Pasi na Kukumbatia Fumbo la Msalaba!


Ushindi wa maisha ya Kikristo unajionesha kwa namna ya pekee kwa njia ya Fumbo la Msalaba yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo, kumbe, waamini hawana sababu ya kuuogopa Msalaba kwani huu ndio ukweli ambao Yesu mwenyewe aliwafunulia wafuasi wake, alipokuwa anapanda kwenda Yerusalemu ili kukabiliana na mateso, kifo na hatimaye ufufuko siku ya tatu kama ilivyoandikwa.

Anakumbusha kwamba, ukubwa ni huduma kwa wanyonge na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Ni changamoto kwa waamini na viongozi wa Kanisa kushinda kishawishi cha uchu wa madaraka na badala yake wakumbatie Fumbo la Msalaba linaloonesha hekima, upendo na huruma ya Mungu kwa waja wake. Hakuna Ukristo pasi na Fumbo la Msalaba linalopaswa kufahamika katika maisha na utume wa Kanisa.

Ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano asubuhi, tarehe 29 Mei 2013, wakati wa Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kikanisa cha Domus Sanctae Marthae, kilichoko mjini Vatican. Baba Mtakatifu anasema, kuna kishawishi kikubwa cha Wakristo kutaka kupata mafanikio ya chapu chapu, pasi na kulikumbatia Fumbo la Msalaba. Mwenyezi Mungu anawakirimia waja wake yale wanayomwomba kwa imani na matumaini kadiri ya mpango wake na wala si kadiri ya vionjo na matamanio ya binadamu.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuendelea kuliombea Kanisa ili liweze kujikita katika fadhila ya unyenyekevu, likiandamana daima na Kristo katika maisha na utume wake. Ibada hii ya Misa Takatifu imehudhuriwa na wafanyakazi wa Kituo cha Televisheni cha Vatican, CTV pamoja na wafanyakazi wa maabara na mitambo kwenye Sekretarieti ya Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.