2013-05-30 11:05:24

Haki msingi za Wakristo Barani Ulaya zinapaswa kulindwa na kudumishwa!


Askofu mkuu Mario Toso, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Haki na Amani anasema, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete kulinda na kutetea haki msingi za Wakristo barani Ulaya ambao kwa sasa wanaonekana kuandamwa na matukio ya kibaguzi bila kuwasahau waamini wa dini nyingine pia.

Askofu mkuu Toso ameyasema hayo hivi karibuni wakati alipokuwa anashiriki kwenye Mkutano uliokuwa unajadili juu kuvumiliana na kutobaguana sanjari na haki msingi za vijana, uliohitimishwa hivi karibuni nchini Albania. Mkutano huu uliandaliwa na Shirika la Usalama na Ushirikiano Barani Ulaya, OSCE, unaofanyika kila baada ya miaka mitatu.

Baadhi ya Serikali za Nchi za Ulaya zimekuwa zikiendesha sera za kibaguzi, hali ya kutovumiliana na wakati mwingine kuwanyanyasa na kuwadhulumu Wakristo pamoja na Waamini wa dini nyingine, ambao wana idadi ndogo Barani Ulaya. Wakristo wamekuwa wakibaguliwa na Jamii nyingi Barani Ulaya na kwamba, hii ni hali inayoonesha kwamba, inaendelea kuongezeka maradufu miongoni mwa nchi wanachama wa OSCE, licha ya jitihada za makusudi zinazofanywa na Mashirika mbali mbali Barani Ulaya.

Imani ya Kikristo na Ibada zake imekuwa ni chanzo cha kinzani na migogoro ya Kijamii kana kwamba, Wakristo hawana haki ya kuungama na kuishuhudia imani yao katika maisha ya hadhara. Jambo hili linabainisha kwamba, hapa kunakosekana uhuru wa kidini na kuabudu kama ulivyobainishwa wakati wa kuasisi OSCE kunako mwaka 1957 pamoja na mapitio yaliyojionesha tangu wakati huo hadi mwaka 2010, Tamko la Astana lilipotolewa kama Kumbu kumbu endelevu ya mkutano huo.

Ni jukumu na dhamana kwa Nchi wanachama wa OSCE kuhakikisha kwamba, wanazuia na kudhibiti vitendo vya kibaguzi na dhuluma dhidi ya Wakristo, ili waweze kupata nafasi ya kukiri na kuishuhudia imani yao katika maisha ya hadhara. Kila mwamini anapaswa kutekeleza uhuru wake kwa kuongozwa na dhamiri nyofu. Madhulumu na nyanyaso dhidi ya Wakristo ni jambo tete linalohatarisha amani na utulivu, kumbe linapaswa kushughulikiwa kikamilifu pamoja na kuondokana na woga usiokuwa na msingi dhidi ya Waamini wa dini ya Kiislam.







All the contents on this site are copyrighted ©.