Chuo Kikuu cha Madaba ni jukwaa la majadiliano ya kidini; mahali pa kutafuta ukweli
na mafao ya wengi!
Mto Yordani una umuhimu wa pekee katika historia na maisha ya Kikristo. Hapa ni mahali
ambapo Yesu alibatizwa na ubatizo ni mlango wa Imani na Maisha ya Kikristo. Ni maneno
ya Kardinali Leonardo Sandri, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Makanisa ya Mashariki
wakati wa ufunguzi wa Chuo Kikuu cha Madaba nchini Yordani pamoja na kuwasilisha salam
na mateshi mema kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko kwa viongozi na wananchi wa Yordani.
Katika salam hizi, Baba Mtakatifu Francisko amewaahidia sala na sadaka yake kwa ajili
ya kulinda na kudumisha msingi wa haki na amani huko Mashariki ya Kati.
Baba
Mtakatifu anatambua na kuthamini mchango unaoendelea kutolewa na viongozi wa Yordan
katika mchakato wa ujenzi wa mshikamano na uelewano wa kimataifa. Anawaombea wanafunzi
wa Chuo Kikuu cha Madaba ambacho kimefunguliwa rasmi Alhamisi, tarehe 30 Mei 2013,
tukio ambalo limehudhuriwa na viongozi mbali mbali wa Kanisa na Serikali. Chuo hiki
anasema Kardinali Sandri ni matokeo ya sadaka ya Wakristo huko Mashariki ya Kati pamoja
na mchango uliotolewa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, tangu Chuo
hiki kilipoasisiwa!
Kardinali Sandri anasema, Chuo Kikuu cha Madaba ni kielelezo
makini cha vipaumbele vya Kanisa na Serikali katika maboresho ya sekta ya elimu kwa
vijana wa kizazi kipya ambao kimsingi ni tumaini la Taifa na Jeuri ya Kanisa. Kwa
njia ya elimu makini: umaskini, ujinga, shida pamoja na mahangaiko ya mwanadamu yanaweza
kupatiwa ufumbuzi wa kudumu. Elimu hii haina budi kukamilishwa kwa kuzingatia kanuni
maadili na utu wema unaopaswa kuundwa kwa njia ya dhamiri nyofu mintarafu imani za
vijana husika ili kutafuta mafao ya wengi.
Chuo Kikuu ni jukwaa makini la
majadiliano ya kidini miongoni mwa waamini wa dini mbali mbali nchini Yordani; ni
mahali pa kutafuta ukweli na mafao ya wengi huku wananchi wakiheshimiana na kuthaminiana
kwa kutambua kwamba, wote ni watoto wa Mwenyezi Mungu, changamoto endelevu kwa Wanajumuiya
wa Chuo Kikuu cha Madaba, ili kuponya makovu ya utengano na chuki miongoni mwa Jamii.
Kanisa linapenda kuchangia katika mchakato wa maendeleo bila ya kuhatarisha utamaduni
na mapokeo ya wananchi husika.