2013-05-29 09:33:26

Mwaka wa Imani: Maadhimisho ya Injili ya Uhai: tarehe 15-16 Juni 2013


Askofu mkuu Rino Fisichella, Rais wa Baraza la Kipapa la kuhamasisha Uinjilishaji Mpya anabainisha kwamba, Maadhimisho ya Mwaka wa Imani yanaendelea kushika kasi na kwamba, kwa mwezi Juni, tarehe 15 hadi tarehe 16 Juni 2013, Mama Kanisa ataadhimisha Siku ya Injili ya Uhai kama inavyojulikana kwa lugha ya Kilatini kwamba, "Evangelium Vitae". Kauli mbiu inayoongoza maadhimisho haya ni "Kwa kuamini wawe na maisha tele!"

Lengo kuu ni kuwahamasisha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusimama kidete kulinda na kutetea Injili ya Uhai tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake hadi mauti ya kawaida yanapomfika kadiri ya mpango na mapenzi ya Mungu mwenyewe ambaye kwa asili ni chemchemi ya maisha. Wakristo wanaendelea kuhamsishwa kulinda na kutetea utu na heshima ya mwanadamu. Tukio hili linatarajiwa pia kuwa na uwakilishi mkubwa ili waamini watambue kwamba, wao wanahamasishwa kuwa ni watangazaji wa Injili ya Uhai.

Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa Jumapili tarehe 16 Juni 2013, Saa 4:30 Asubuhi kwa saa za Ulaya, Kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu na kuwamegea waamini na watu wote wenye mapenzi mema, Injili ya Maisha sanjari na kuwatia moyo wagonjwa na wale wote wanaoteseka kutokana na sababu mbali mbali katika maisha yao.

Askofu mkuu Fisichella anaendelea kufafanua kwamba, wale wote watakaoshiriki katika Maadhimisho ya Tukio hili la Kikanisa, mara baada ya Katekesi, watapata fursa ya kufanya Maandamano hadi kwenye Kaburi la Mtakatifu Petro, ili kuungama Imani yao. Maandamano haya yataanza saa 8:00 mchana hadi saa 11:00 Jioni, Siku ya Jumamosi ya tarehe 15 Juni 2013. Waamini watapata fursa ya Kuabudu Ekaristi Takatifu pamoja na kushiriki Sakramenti ya Upatanisho, ili kujipatia rehema zinazotolewa na Mama Kanisa katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani.

Kitakuwa ni Kipindi cha Katekesi kuhusu Injili ya Uhai na kwamba, Katekesi hii itatolewa kwenye Makanisa mbali mbali yaliyoko mjini Roma kadiri ya lugha za watu husika. Baadhi ya viongozi wakuu wa Kanisa watashiriki katika kuwapatia waamini Katekesi ya kina. Taasisi ya Maisha itakuwa mstari wa mbele kwani wao ndio wadau wakuu katika Maadhimisho haya.

Jumamosi ya tarehe 15 Juni, kuanzia saa 2:30 Usiku, kutafanyika Maandamano ya kimya, huku waamini wakiwa wameshika mienge mikononi mwao kuelekea kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro. Hapo baadhi ya waamini watashirikisha ushuhuda wa maisha yao jinsi ambavyo wamesimama kidete kulinda na kutetea zawadi ya uhai au jinsi ambavyo wameonja huruma na upendo wa Mungu katika hija ya maisha yao hapa duniani.

Waamini kutoka sehemu mbali mbali za dunia tayari wamekwisha onesha nia ya kushiriki katika tukio hili. Huu ni mwaliko kwa waamini na wale wote ambao wamekuwa mstari wa mbele kutetea Injili ya Uhai, kujitokeza kama njia ya ushuhuda wa imani yao katika matendo.







All the contents on this site are copyrighted ©.