Mshahara wa ufuasi wa Kristo ni Msalaba na Madhulumu!
Mateso na mahangaiko ni kati ya changamoto ambazo Wafuasi wa Kristo wanaalikwa kuzimwilisha
katika maisha yao kama kielelezo cha ufuasi wa Kristo bila ya kukata tamaa, Kama ilivyokuwa
kwa Kristo mwenyewe, wafuasi wake wataendelea kukabiliana na madhulumu na nyanyaso,
lakini watambue kwamba, Kristo ameshinda yote.
Ni sehemu ya mahubiri ya Baba
Mtakatifu Francisko wakati wa Maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kikanisa
cha Domus Sanctae Marthae, kilichoko hapa mjini Vatican siku ya Jumanne, tarehe 28
Mei 2013. Baada ya Yesu kuainisha jinsi itakavyokuwa vigumu kwa matajiri kuingia kwenye
Ufalme wa Mungu, mitume walishikwa na bumbuwazi na kumuuliza, Je, wao ambao wameacha
yote, watapata faida gani? Yesu anawajibu kwa macho makavu kabisa kwamba, watapata
yote kwa ziada, lakini pia watakabiliwa na madhulumu, huu ndio utakaokuwa mshahara
wao mkubwa zaidi.
Wakristo sehemu mbali mbali za dunia wanaendelea kukabiliana
na madhulumu na taabu za maisha, changamoto kwa wafuasi wa Kristo kuibeba vyema Misalaba
yao na kumfuasa Kristo aliyejinyenyekesha hata akateswa na kufa Msalabani, kielelezo
cha unyenyekevu wa hali ya juu kabisa. Wakristo wanapaswa kujitoa kimaso maso wakitambua
kile wanachofanya katika maisha yao.
Kuna baadhi ya watu wenye majina na sifa
kemkem ambao walidhani kwamba, kumfuasa Kristo ni kujijengea jina na hatimaye, kupata
marupu rupu kibao! Watu wa namna hii anasema Baba Mtakatifu wamemezwa na malimwengu
na wanasahau kwamba, mateso na madhulumu yatawaandama katika hija ya maisha yao, kama
ilivyokuwa kwa Mtakatifu Petro na mitume wengine.
Baba Mtakatifu anawaalika
Wakristo kumshuhudia Kristo kwa maisha na matendo yao, kwa njia ya huduma kwa maskini
na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii kama alivyofanya Mama Theresa wa Calcutta.
Ni Mtawa ambaye alitumia muda wake mwingi kwa ajili ya Kuabudu Ekaristi Takatifu,
humo akajichotea nguvu ya kuwahudumia maskini na wanyonge wa dunia hii kwa upendo
wa Kikristo, akithamini utu na heshima yao kama watoto wa Mungu.
Wakristo
waguswe na ujumbe wa Neno la Mungu litakalowawezesha kufanya mabadiliko katika maisha
sanjari na kuwapatia nguvu ya kuweza kukabiliana na madhulumu katika hija ya maisha
yao hapa duniani. Ufuasi wa Kristo unaambatana na upendo wa kweli, hatua kwa hatua.
Baba Mtakatifu anawaalika waamini kumwomba Kristo neema na ujasiri wa kutolea ushuhuda
amini, kwani Kristo yuko pamoja nao katika shida na magumu ya maisha.
Ibada
hii ya Misa takatifu imehudhuriwa na viongozi waandamizi kutoka Baraza la Kipapa la
Uhamasishaji wa Uinjilishaji Mpya, Wafanyakazi wa kitengo cha umeme na useremala kutoka
Sekretarieti ya Vatican.