Mapadre wa Jimbo Katoliki Embu, wanahamasishwa kujenga ari na moyo wa kimissionari
tayari kuhudumia Majimbo mengine hitaji!
Askofu Paul Kariuki Njiru wa Jimbo Katoliki Embu, Kenya, anawaalika Mapadre wa Jimbo
nchini Kenya kujenga na kuimarisha ari na moyo wa kimissionari, tayari kujitosa bila
ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza Habari Njema ya Wokovu katika maeneo ambayo yanakabiliwa
na upungufu mkubwa wa wahudumu wa Injili na Mafumbo ya Kanisa.
Askofu Njiru
ameyasema hayo Jumatatu tarehe 27 Mei 2013 wakati alipokuwa anazungumza kwenye mkutano
wa Mapadre wa Jimbo Katoliki la Embu. Takwimu zinaonesha kwamba, kila Parokia ya Jimbo
Katoliki Embu ina wastani wa Mapadre watatu wanaohudumia Parokia, wakati ambapo kuna
baadhi ya Majimbo nchini Kenya, parokia zinahudumiwa na Padre mmoja au wakati mwingine
hazina hapa Padre, hali inayowafanya waamini kuadhimisha Ibada bila Padre.
Jimbo
Katoliki Embu linawahamasisha mapadre wake kujitoa kwenda Majimbo mengine kutangaza
Habari Njema ya Wokovu kama alama ya mshikamano wa kichungaji na Majimbo ambayo bado
yana upungufu wa wahudumu na wala si kwamba, Jimbo Katoliki la Embu lina Mapadre wengi
zaidi. Hadi sasa kuna Mapadre wawili wanaotoa huduma ya kichungaji nje ya Jimbo hili.