2013-05-29 14:34:20

Asasi, Vyama na Makundi sasa ruksa kuunda Mabaraza ya Katiba nchini Tanzania



Tume ya Mabadiliko ya Katiba imetoa Mwongozo unaoruhusu kuanza rasmi kwa uundwaji wa Mabaraza ya Katiba ya asasi, taasisi na makundi mbalimbali kwa lengo la kujadili na kutoa maoni kuhusu rasimu ya katiba inayotarajiwa kutolewa na Tume hiyo hivi karibuni.

Kwa mujibu wa mwongozo ulitolewa na Tume hiyo Jumatano, 29 Mei, 2013 na kusainiwa na Mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji Joseph Warioba, mwongozo utatumika kwa miezi mitatu kuanzia, Juni 1 hadi Agosti 31, 2013.

“Mabaraza haya ya Katiba ya Asasi, Taasisi na Makundi ya Watu wenye malengo yanayofanana yatajadili na kutoa maoni kuhusu Rasimu ya Katiba,” amesema Jaji Warioba na kuongeza kuwa maoni hayo yanaweza kuwasilishwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwa njia ya randama, barua, andiko, muhtasari wa makubaliano.

Mwongozo huo, ambao utachapishwa katika magazeti mbalimbali ya siku ya Alhamisi (Mei 30, 2013) na kurudiwa tena Jumatatu (Juni 3, 2013), pia unapatikana katika tovuti mbalimbali ikiwemo ya Tume hiyo () na ukurasa wa facebook wa Tume hiyo (Tume ya Mabadiliko ya Katiba Tanzania).

Kwa mujibu wa maelezo ya Jaji Warioba katika mwongozo huo, mabaraza hayo ya taasisi yanaundwa kwa mujibu wa kifungu cha 18 (6) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83 kinachoitaka Tume kuruhusu Asasi, Taasisi na Makundi ya Watu wenye malengo yanayofanana kuandaa mikutano kwa ajili ya kutoa fursa kwa wanachama wao kutoa maoni yao juu ya Rasimu ya Katiba na kisha kuwasilisha maoni hayo kwa Tume.

Katika mwongozo huo, Jaji Warioba ametaja taasisi zinazoweza kuunda Mabaraza hayo kuwa ni pamoja na Jumuiya ya Kidini, Chama cha Siasa, Asasi ya Kiraia, Taasisi ya Elimu ya Juu, Chama cha Wafanyakazi, Chama cha Wakulima, Chama cha Wafugaji, Chama cha Wanahabari na Baraza la Watoto.

Taasisi nyingine zinazoweza kuunda mabaraza hayo ni taasisi ya Wafanyabiashara, Mabaraza ya Wanawake, Taasisi ya Kitaaluma, Baraza la Vijana, Baraza la Wazee, Jumuiya ya Kijamii (CBO) na Chama cha Waajiri. Nyingine ni Chama cha Wanasheria, Umoja wa Watanzania waishio Nchi za Nje, Wizara, Idara na Taasisi za Serikali, na Kundi au makundi ya watu wenye malengo yanayofanana au wale wenye mahitaji maalum katika jamii.
Kuhusu gharama za uendeshaji, mwongozo huo unaelekeza kuwa Mabaraza ya Katiba ya Asasi, Taasisi na Makundi ya Watu wenye Malengo Yanayofanana, yatagharimia taratibu zote za uendeshaji wa Mabaraza ya Katiba hayo.

Kwa mujibu wa Jaji Warioba katika mwongozo huo, ili kuiwezesha kuratibu kwa ufanisi mchakato wa kukusanya maoni kuhusu Rasimu ya Katiba, kila Asasi, Taasisi na Makundi ya Watu wenye malengo yanayofanana yatakayounda Mabaraza ya Katiba itatoa taarifa ya maandishi ya kusudio la kuunda, kuendesha na kusimamia Mabaraza ya Katiba.

Taarifa hiyo itawasilishwa katika Ofisi za Tume ya Mabadiliko ya Katiba moja kwa moja – Makao Makuu, Mtaa wa Ohio - Dar es salaam au Ofisi Ndogo Mtaa wa Kikwajuni Gofu Jengo la Mfuko wa Barabara Zanzibar. Taarifa pia inaweza kutolewa kwa Tume kupitia S.L.P. 1681, Dar es Salaam au S.L.P. 2775, Zanzibar.








All the contents on this site are copyrighted ©.