Siku kuu ya Ekaristi Takatifu iwe ni fursa ya kuonesha imani ya Kanisa katika uwepo
wa Mwili na Damu ya Kristo katika Sakramenti hii!
Katika Maadhimisho ya Sherehe ya Ekaristi Takatifu, Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi,
tarehe 30 Mei 2013, Saa 1:00 za Usiku, anatarajiwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu
kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano na baadaye kufuatia Maandamano
ya Ekaristi Takatifu kuzunguka mitaa na viunga vya mji wa Roma.
Kardinali Agostino
Vallini, Makamu Askofu Jimbo kuu la Roma anawakumbusha Mapadre na Waamini kwa jumla
kwamba, Maadhimisho ya Sherehe ya Ekaristi Takatifu kwa Mwaka huu, yanabeba uzito
wa pekee kwani yanafanyika katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, changamoto kwa waamini
kutolea ushuhuda wa imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, wakionesha kwa namna ya pekee
uwepo wa Kristo anaye andamana na wafuasi wake katika hija ya maisha yao ya kila siku.
Ile ni nafasi kwa waamini kuonesha imani yao kwa uwepo wa Kristo katika Sakramenti
ya Ekaristi Takatifu.
Kardinali Agostino Vallini anachukua fursa hii kuwaalika
waamini kujitokeza kwa wingi ili kushiriki katika Ibada ya Misa Takatifu na baadaye
katika Maandamano ya Ekaristi Takatifu.