Changamoto ya maisha na utume wa Kanisa nchini Madagascar
Wananchi wa Madagascar wanaendelea kuishi katika umaskini wa kipato licha ya kuwa
na utajiri mkubwa wa maliasili, madini na nishati ambayo ingetumika kwa ajili ya mafao
na maendeleo ya wengi.
Hali hii
inakuzwa pia na migogoro, kinzani na machafuko ya kisiasa ambayo yamekuwa yakijirudia
rudia nchini humo kwa miaka kadhaa kiasi kwamba, wananchi wameanza kukosa imani na
wanasiasa ambao kimsingi wamekuwa wakijali zaidi masilahi binafsi kuliko hata ustawi
na maendeleo ya wananchi wa Madagscar.
Uchaguzi mkuu ambao umekuwa ukifikiriwa
na wengi kuwa ni mkombozi wa hali ya kisiasa nchini Madagascar umekuwa ukihairishwa
mara kwa mara kutokana na ukata na hali ngumu ya uchumi. Lakini jambo la kushangaza
ni kuona kwamba, Makampuni ya Kimataifa yanaendelea kuwekeza na kupata faida kubwa
katika vitega uchumi vyao, wakati ambapo wananchi wa Madagascar wanaendelea kuogelea
katika dimbwi la umaskini wa hali na kipato.
Kuna huduma duni za afya na elimu
zinazotolewa na Serikali na kwamba, haki msingi za binadamu ziko mashakani. Hali ya
maisha ni mbaya zaidi vijijini ambako kuna idadi kubwa ya watoto wanaopoteza maisha
kwa magonjwa ambayo yangeweza kupatiwa kinga na tiba.
Katika mazingira kama
haya anasema Askofu Rosario Vella kutoka Madascar wakati wa mahojiano maalum na Shirika
la Kipapa la Misaada kwa Kanisa hitaji kwamba, Kanisa nchini humo limejikuta likibeba
dhamana kubwa katika utoaji wa huduma ya elimu, afya na maendeleo endelevu, kwa kutumia
kwa ukamilifu rasilimali iliyopo.
Wananchi wengi wa Madagascar kama hata ilivyo
sehemu nyingine za Bara la Afrika, wanaendelea kuathirika na utandawazi na maendeleo
ya sayansi na teknolojia kiasi kwamba, wanajikuta wakipoteza tunu msingi za maisha
ya kifamilia, kijamii na kiutu; Upendo, mshikamano pamoja na thamani yautu wa mwanadamu
si kati ya mambo yanayopewa msukumo wa pekee nchini humo. Watu wanajikuta wakielemewa
na ubinafsi, uchu wa mali na madaraka hata kwa njia za mkato na kwamba, wazazi na
walezi wanaanza kukosa dira na mwelekeo katika makuzi na elimu kwa watoto wao!
Kanisa
Katoliki nchini Madagascar linaziona changamoto hizi na linazifanyia kazi katika maisha
na utume wake, kwa kuwekeza katika majiundo ya vijana kwa njia ya elimu makini, kwani
kutokana na umaskini wa kipato, vijana wakiwa bado na umri mdogo wanajikuta wakilazimika
kuzikimbia familia zao hasa kwa wale wanaoishi vijijini ili kwenda mijini kutafuta
nafuu na uhakika wa maisha, jambo ambalo linawanyima haki ya kuendelea na masomo pamoja
na uwezekano wa kupata malezi bora kutoka katika familia husika. Vijana hawa wanajikuta
wakiishi katika mazingira magumu hali inayowapelekea kujiingiza katika matumizi haramu
ya dawa za kulevya, biashara ya ngono, wizi na ujambazi. Wakati mwingine, wazazi wasiokuwa
na soni wamejikuta wakiwatumbukiza watoto wao hata katika utalii wa ngono nchini Madagascar,
jambo ambalo linadhalilisha utu na heshima ya wasichana na wavulana hao.