Wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume wamehitimisha mkutano wao wa themanini
na moja, uliopembua pamoja na mambo mengine, umuhimu wa huduma ya uongozi katika hija
ya maisha ya kitawa kwa nyakati hizi. Ni tafakari iliyokuwa inaangalia dhamana ya
uongozi mintarafu maisha ya kitawa, miaka hamsini ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican.
Wajumbe wameshirikishana: mawazo, mang'amuzi na changamoto wanazokabiliana nazo katika
maisha na utume wao.
Wajumbe kwa namna ya pekee wamekumbushana kwamba, mmomonyoko
wa maadili na utu wema bila kusahau athari za myumbo wa uchumi kimataifa ni mambo
yanayoukumba ulimwengu, Jamii na hata Kanisa, bila kusahau Mashirika ya Kitawa na
Kazi za Kitume, changamoto kwa watawa kujikita zaidi na zaidi katika: mang'amuzi,
uwajibikaji wa pamoja na uaminifu.
Mkutano huu umehudhuriwa pia na viongozi
wakuu wa Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume. Wajumbe wamekumbushwa
kwamba, uongozi katika maisha ya kitawa na kazi za kitume ni muhimu sana unaohitaji
fadhila ya unyenyekevu na mabadiliko ya mawazo. Aishangazi kuona kwamba, kuna mgogoro
wa uongozi katika Mashirika ya Kitawa kuanzia kwenye Jumuiya, hali ambayo inatishia
umoja, upendo, mshikamano na uaminifu wa karama miongoni mwa watawa.
Kuna haja
kwa wakuu wa mashirika ya kitawa na kazi za kitume kutambua kwamba, kuna tatizo la
uongozi, linalohitaji watawa kuliangalia kwa mtazamo mpya, licha ya kukazia utii,
uwajibikaji pamoja na utii wa kiimani ambao ni muhimu sana katika mchakato wa maisha
miongoni mwa watawa. Viongozi wamehamasishwa kujenga na kukuza uhusiano fungamanishi
miongoni mwao, ili kwa pamoja waweze kufanya hija ya maisha ya kitawa inayofumbata
utu na ubinadamu unaopaswa kuinjilishwa.
Jumuiya iwe ni mahali pa majadiliano
ya kina na uwajibikaji; pawe ni mahali ambapo upendo na huruma ya Mungu unamwilishwa
miongoni mwa wanajumuiya. Watawa watambue kwamba, wao ni zawadi kwa jirani zao wanaotembea
kwa pamoja katika kutekeleza mpango wa Mungu kwa mwanadamu katika uhalisia wa maisha
yake.
Watawa watambue kwamba, wako duniani na wanakabiliwa na athari za myumbo
wa maadili ya uongozi kama inavyojionesha katika Jamii na Familia kwa ujumla. Watawa
wanaalikwa kuwa ni kielelezo cha matumaini kadiri ya Mpango wa Mungu. Baba Mtakatifu
mstaafu Benedikto wa kumi na sita ni mfano wa kuigwa aliyetambua kwamba, uongozi ni
huduma. Papa Francisko anaendelea kutoa mwelekeo mpya wa uongozi kama huduma, kwa
kuwa karibu zaidi na Familia ya Mungu pamoja na Watu wote wenye mapenzi mema.