2013-05-27 08:00:55

Mwenyezi Mungu bado anaendelea kufanya hija na waja wake!


Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, kwenye Sherehe za Fumbo la Utatu Mtakatifu aliwaambia waamini na mahujaji waliokuwa wamekusanyika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu petro mjini Vatican kwamba, alikuwa anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumwezesha kwa mara ya kwanza kufanya hija ya kichungaji katika Parokia ya Jimbo kuu la Roma. Anawaomba waamini kuendelea kumsindikiza katika utume wake kwa njia ya Sala.

Baba Mtakatifu anasema, Adhimisho la Mwanga wa Fumbo la Pasaka linapyaisha kila mwaka ile furaha inayobubujika kutoka katika imani, kwa kutambua kwamba, Mungu ni upendo na asili ya maisha; ni upendo ambao umejionesha kwa namna ya pekee kwa njia ya mateso na kifo cha Kristo Msalabani na kwamba, ni upendo huo unaomwezesha pia Roho Mtakatifu kuendelea kumgeuza mwanadamu na kuumba upya sura ya nchi.

Kwa kutambua kwamba, Mungu ni upendo, mwamini anachangamotishwa kupenda na kujitoa kwa ajili ya jirani zake, kama alivyofanya Yesu anayeendelea kufanya hija pamoja na wafuasi wake katika njia ya maisha. Fumbo la Utatu Mtakatifu ni ile sura ya Mwenyezi Mungu iliyofunuliwa na Yesu na kuahidiwa kwa Roho Mtakatifu. Mwenyezi Mungu katika Agano la Kale ametembea na Waisraeli na Yesu anaendeleza hija hii akiwa pamoja na wafuasi wake na kwamba, amewaahidia Roho Mtakatifu atakayewafundisha ukweli wote; anawaongoza na kuwakirimia mawazo mazuri. Kanisa linaadhimisha Fumbo la Utatu Mtakatifu kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, anayewapenda na kutaka waingie katika utawala wake ambao ni uzima wa milele.

Baba Mtakatifu aliwaweka waamini wote chini ya ulinzi na usimamizi wa Bikira Maria aliyeonesha unyenyekevu wa hali ya juu, kiasi kwamba, sasa amekwisha ingia katika hija ya uzima wa milele na utukufu wa Fumbo la Utatu Mtakatifu. Bikira Maria, Mama wa Kanisa ni kielelezo makini cha matumaini katika hija ya maisha ya imani. Ni Mama Mfariji.







All the contents on this site are copyrighted ©.