2013-05-27 10:55:02

Mshikamano wa upendo na ushuhuda wa Kikristo ni njia makini ya kuwaimarisha Wakristo Imani huko Mashariki


Baraza la Makanisa Ulimwenguni linayataka Makanisa wanachama huko Mashariki ya Kati kuendelea kusoma alama za nyakati kutokana na mabadiliko makubwa yanayoendelea kujitokeza katika medani mbali mbali za maisha ya watu, jambo ambalo linahitaji kuwepo na mshikamano na ushuhuda wa Kikristo, kama njia ya kuwaimarisha Wakristo katika imani.

Haya ni baadhi ya maoni yaliyotolewa na wajumbe 150 waliokuwa wanashiriki katika mkutano wa kiekumene ulioandaliwa na Baraza la Makanisa Ulimwenguni kwa kushirikiana na Baraza la Makanisa Mashariki ya Kati, kuanzia tarehe 21 Mei na umehitimishwa hapo tarehe 25 Mei, 2013. Wakristo huko Mashariki ya Kati wanatambua fika kwamba, hatima ya uhuru wa kuabudu na kushuhudia imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, iko mikononi mwa Wanasiasa na Viongozi wa Serikali. Kumbe, kuna haja kwa viongozi wa Makanisa Mashariki ya Kati kudai haki hii msingi kwa ajili ya waamini wao.

Wajumbe wanasema, kuwatenga Wakristo wanaoishi katika Nchi za Kiarabu si suluhu, bali jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, Wakristo wanashikamana kwa udi na uvumba, huku wakionesha ushuhuda wa imani yao kwa Kristo na Kanisa lake; ushuhuda unaoleta mvuto na mguso. Kanisa linapenda kutekeleza dhamana na wajibu wake kwa kuzingatia misingi ya ukweli, uwazi, uwajibikaji na mafao ya wengi na wala halitaki kupewa upendeleo wa pekee. Kanisa litaendelea kupinga utawala unaowagandamiza na kuwanyanyasa wananchi wake kutokana na ubinafsi pamoja na kulinda masilahi yao binafsi.

Wajumbe wa mkutano huu wamekumbushwa kwamba, wanakutanika katika majadiliano ya kiekumene yanayofumbatwa katika mateso na mahangaiko ya watu, changamoto ya kila mwamini kutekeleza dhamana na wajibu wake katika mchakato unaopania kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano wa dhati miongoni mwa Wakristo. Mshikamano huu unapaswa pia kujionesha katika msingi wa imani. Wakristo Mashariki ya Kati wanauyashukuru Makanisa kwa kuonesha umoja na mshikamano wakati wa Maadhimisho ya Kiimani na pale ambapo Maaskofu wawili walipotekwa nyara, Makanisa yamelaani na kukemea sana vitendo hivi vinavyodhalilisha utu na heshima ya binadamu.

Ni mwaliko kwa Makanisa Mashariki ya Kati kushirikiana na kufanya kazi kwa pamoja, kwani wanatambua kwamba, wanawajibu wa kuendelea kuishi katika nchi zao pamoja na kushirikiana na Waamini wa dini nyingine ili kujenga na kuimarisha misingi ya haki, amani, utulivu pamoja na kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya kila mwanadamu. Msalaba wa Kristo uwaongoze waamini kuchuchumilia misingi ya haki na amani kwa ajili ya Jamii nzima.

Wajumbe wanaendelea kuwatia moyo Wakristo huko Mashariki ya kati ili kusimama kidete katika misingi na maisha yao ya Kikristo, huku wakiendelea kushikamana na vijana ili kukabiliana na changamoto za maisha pasi na kukata wala kukatishwa tama, wasimame imara kulinda na kudumisha: misingi ya haki, amani na upatanisho wa kweli.

Wakristo wanaendelea kuhamasishwa ili waweze kuwa kweli ni chachu ya maendeleo endelevu na mabadiliko ya kijamii. Vijana kwa hakika ni jeuri ya Jamii na Kanisa katika ujumla wake. Hawa ndio wale walioleta mageuzi na mwanzo mpya kwa Nchi nyingi za Kiarabu katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni. Vijana wakiwezeshwa kimaadili, kiutu na kiuchumi wanaweza kuleta mabadiliko makubwa kwa Jamii inayowazunguka.








All the contents on this site are copyrighted ©.