2013-05-27 09:15:58

Mshikamano ni fadhila yenye umuhimu wa pekee katika maisha ya Kijamii


Wajumbe wa Mfuko wa Kipapa unaojulikana kama “Centesimus Annus Pro Pontifice, uliozinduliwa na Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili yapata miaka ishirini iliyopita, kama kumbu kumbu endelevu ya Maadhimisho ya Miaka 100 tangu Waraka wa Rerum Novarum, yaani Mambo Mapya, ulipochapishwa wamehitimisha mkutano wao wa Mwaka uliokuwa unaongozwa na kauli mbiu “mshikamano katika ajira: changamoto katika karne ya 21”.

Kanisa kwa kipindi cha zaidi ya miaka 100 limeanzisha amana kubwa ya Mafundisho Jamii ya Kanisa ambayo yametajirishwa kwa namna ya pekee na Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili pamoja na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita kwa njia ya nyaraka na hotuba zao mbali mbali.

Baba Mtakatifu Francisko, amewashukuru wajumbe wa Mfuko huu kwa kulisaidia Kanisa kueneza Mafundisho Jamii ya Kanisa katika medani mbali mbali za maisha. Hii ni huduma makini kwa ajili ya Khalifa wa Mtakatifu Petro na changamoto kwa waamini walei kuendelea kuyatakatifuza malimwengu hasa kutokana na mchango wao katika Jamii, maeneo ya kazi na uchumi.

Kazi ni utimilifu wa maisha ya mwanadamu ambayo kwa sasa inakabiliwa na changamoto mbali mbali, jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, Jamii inajitahidi kujenga na kudumisha moyo wa upendo na mshikamano wa dhati unaopata chimbuko lake katika Injili ya Kristo, nguvu thabiti inayowawezesha waamini na watu wenye mapenzi mema kusonga mbele kwa moyo mkuu.

Madhara ya myumbo wa uchumi kimataifa ni changamoto na mwaliko kwa Jamii kufanya tafakari ya kina ili kufikia ukweli mkamilifu na utekelezaji wa Mafundisho Jamii ya Kanisa yanayotoa kipaumbele cha pekee katika kujenga mshikamano wa dhati wa matumizi ya rasilimali kwa ajili ya mafao ya wengi. Ukosefu wa fursa za ajira pamoja na tatizo la watu wengi kuendelea kupoteza fursa hizi ni jambo ambalo linatia simanzi kwani idadi ya watu wasiokuwa na fursa za ajira inaendelea kuongezeka maradufu kwa kuwatumbukiza watu wengi zaidi katika umaskini wa hali na kipato.

Ndiyo maana anasema Baba Mtakatifu Francisko kwamba, kuna haja ya kuonesha moyo wa mshikamano utakaosaidia kufanya upembuzi yakinifu, ili kubaini kasoro zilizojitokeza ili ziweze kubadilishwa, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa haki msingi za binadamu. Mshikamano ni fadhila yenye umuhimu wa pekee katika maisha ya Kijamii.

Athari za myumbo wa uchumi kimataifa zinagusa undani wa maisha ya mwanadamu, yaani katika msingi wa maisha adili na utu wema. Kuna baadhi ya watu wamekumbwa na uchu wa mali na madaraka; watu wanaotafuta faida kubwa, kiasi hata cha kubeza utu na heshima ya binadamu. Wachumi na watunga sera wanasahau kwamba, binadamu na utu wake ni tunu msingi zinazopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika: sera, malengo na mikakati ya maendeleo.

Binadamu anapaswa kupewa fursa itakayomshirikisha katika utafutaji wa mafao ya wengi kwa kuzingatia msingi wa utu na maadili mema mintarafu uhusiano wake na jirani zake. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko amewashukuru wajumbe hawa na kuwatakia kila la kheri na baraka tele katika maisha na utume wao.








All the contents on this site are copyrighted ©.