2013-05-25 11:58:17

Yaliojiri katika uzinduzi wa Sinodi ya Jimbo Katoliki Musoma, Tanzania


Tarehe 19 Mei, 2013 Kanisa liliadhimisha Sherehe ya Pentekoste. Kwa wanajimbo la Musoma, siku hii ilikuwa na upekee zaidi. Ilikuwa ni siku ya Uzinduzi Rasmi wa Sinodi ya Jimbo. Uzinduzi huo ulifanyika kwa adhimisho la Misa Takatifu iliyoongozwa na Askofu Michael Msonganzila wa Jimbo la Musoma na kuhudhuriwa kwa wingi na Mapadre, Watawa na Waamini toka pembe zote za Jimbo.

Adhimisho la Misa Takatifu lililoanza majira ya saa 4:00 asubuhi, lilifanyika katika Viwanja vya Matumaini Katika Vijana, vinavyopakana na Kanisa Kuu la Jimbo. Hii ilikuwa ni Misa pekee iliyoadhimishwa kwa Jimbo zima siku hiyo ili kuwapa nafasi mapadre wote, watawa na waamini jimboni kushiriki pamoja katika tukio hilo muhimu sana katika historia ya Jimbo. Watu walianza kukusanyika viwanjani hapo kuanzia saa moja asubuhi na kufikia majira ya saa tatu sehemu kubwa ya viwanja hivyo ilikuwa tayari imeshafurika watu. Wengi walifika kivikundi: kiparokia na vyama vya kitume wakiwa na sare zao.

Maandamano yalitanguliwa na tukio la Askofu kugonga kengele ya Kanisa Kuu la Jimbo. Tendo hili lilimaanisha kuwa yeye akiwa mchungaji mkuu wa Jimbo anaitisha kusanyiko la Kijimbo kwa ajili ya kuadhimisha Sinodi na anawaalika kondoo wake kushiriki. Kisha maandamano yalianza kuelekea eneo la Ibada, eneo lililopampwa kifani kwa rangi nyekundu na nyeupe kuakisi sherehe ya Kiliturujia ya Pentekoste iliyoadhimishwa siku hiyo.

Mwanzoni mwa Misa, Padre Robert Luvakubandi, Paroko wa Parokia ya Musoma Mjini alipata nafasi ya kutoa neno la utangulizi na kumkaribisha Baba Askofu kuongoza adhimisho.

Katika neno lake, Pd. Luvakubandi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Sinodi alimjulisha Baba Askofu kuwa shughuli nzima ya maandalizi imekamilika. “Shughuli hiyo imechukua takribani miezi kumi tangu Julai mwaka jana ulipounda Kamati Kuu ya Maandalizi ya Sinodi” alieleza Pd. Luvakubandi. Alifafanua kuwa maandalizi hayo yalijumuisha vikao vya Kamati kupanga ratiba na picha nzima Maadhimisho yatakavyokuwa, kukusanya maoni toka kwa wanajimbo, kuandaa Sala ya Sinodi, kuandaa Kauli Mbiu na wajumbe wa vikao. “Maandalizi hayo” aliendelea kufafanua “yalijumlisha pia semina elekezi iliyotolewa tarehe 21 na 22 Januari kwa wajumbe wote wa sinodi uliowaalika wewe Baba Askofu”.

Katika adhimisho hilo la Misa, lililofanyika kwa uchangamfu na ushiriki hai wa waamini wote katika nyimbo na matendo mengine ya kiibada, Askofu aliwaapisha wajumbe wote wa vikao vya Sinodi waliokuwapo. Wajumbe hawa ni Mapadre wote wanaofanya utume Jimboni Musoma, wawakilishi wa mashirika ya Kitawa yaliyoko Jimboni na wawakilishi kutoka parokia na taasisi zote za Jimbo. Kiapo walichokula, kwa sehemu kubwa, kilikuwa ni ungamo la Imani. Hii ni kwa sababu maadhimisho ya Sinodi ni tendo la Imani na kwa namna ya pekee yanafanyika katika Mwaka wa Imani.

Mahubiri ya Askofu Msonganzila katika Ibada hii ya Misa, yaligusa dhamira zote za siku hiyo, yaani Sherehe ya Pentekoste, Sikukuu ya Walei na Uzinduzi wa Sinodi. “Wapendwa wanafamilia ya Mungu wa Jimbo la Musoma” ndivyo alivyoanza Askofu na kuendelea “leo ni Sherehe ya Pentekoste; sherehe ambayo inahitimisha Kipindi cha Pasaka… Kwa namna ya pekee leo tunasherehekea utimilifu wa Ahadi ya Bwana Yesu kwa Mitume kabla ya kupaa kwake mbinguni, yaani ujio wa Roho Mtakatifu. Pia tunakumbuka kuzaliwa kwa Kanisa na mwanzo wa Utume wa Kanisa. Siku hii pia imewekwa na Kanisa kama sherehe ya Waamini walei”.

Askofu alieleza kuwa kwa wanajimbo la Musoma kusanyiko kubwa la wanajimbo katika Sherehe hii katika Viwanja vya Matumaini katika Vijana lina umuhimu wa kipekee katika historia ya Jimbo kwa sababu ni kusanyiko pia la Uzinduzi wa Sinodi. “Kwa sababu hii twaweza kupaita mahala hapa Viwanja vya Matumaini katika Sinodi!”

Masomo ya liturjia ya siku yalitoka Mdo. 2:1 – 11; 1Kor. 12:3b – 7, 12 – 13; na Yn. 20:19 – 23. Akifanua masomo hayo, Askofu alieleza kuwa Roho Mtakatifu waliyempokea Mitume, aliwapa ujasiri mkubwa wa kulihubiri Neno la Mungu. Roho huyo alikuwa ndio sababu ya Umoja na Uelewano uliokuwa umepotea kati ya Mataifa kwa sababu ya dhambi.

Aliendelea na kusema kuwa Roho Mtakatifu ndiye msingi wa karama na huduma mbalimbali katika Kanisa na ndiye anayefanya karama hizo zilete faida na umoja katika Kanisa. Aliongeza kuwa Roho huyu aliyefanya kazi ya kuwaunganisha mitume na Yesu, sasa anawaunganisha watu na Mungu kwa kuwaondolea dhambi zao. Na matunda yake makuu ni Amani kati ya Mungu na watu.

“Roho huyu tunayempokea katika maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa” alisisitiza “anatuwajibisha tumshuhudie kwa maneno na maisha yetu”. Alionya kuwa “Tunapomtambua Roho Mtakatifu kati yetu, tunalazimika tusiwe na Majivuno na Dharau kwa wengine. Roho tuliyepewa si kwa ajili ya utukufu wetu wenyewe bali ni kwa ajili ya kuujenga mwili wa Yesu yaani Kanisa”

Katika mahubiri hayo Baba Askofu aliwaalika waamini wote kumpa Roho Mtakatifu nafasi katika maisha yao ili atende kazi ndani yao. “Jenga mazingira ya Roho Mtakatifu kutenda kazi ndani yako” alisisitiza.

Baba Askofu alihitimisha mahubiri yake kwa kueleza ratiba na mada kuu za Vikao vya Sinodi. Mintarafu ratiba, alieleza kuwa maadhimisho yote ya Sinodi yanategemea kuchukua takribani Miaka Miwili hadi kuhitimishwa kwake tarehe 03 Oktoba 2014. Na ndani ya kipindi hicho matukio makuu yafuatayo yataadhimishwa. Baada ya Uzinduzi kutakuwa na vikao vikuu vine. Kikao cha Kwanza (03 – 07 Juni 2013), kikao cha Pili (09 – 13 Desemba 2013), kikao cha Tatu (28 Aprili – 02 Mei 2014) na kikao cha nne (04 – 08 Agosti 2014).

Mada kuu zitakazojadiliwa ni mosi; UINJILISHAJI WA IMANI NA CHANGAMOTO ZA NYAKATI ZETU, MIITO NA CHANGAMOTO ZA WAKATI, pili; LITURJIA YA KANISA NA MAISHA YA SAKRAMENTI, tatu; UTUME WA HAKI, AMANI NA UPATANISHO na nne; MAENDELEO NA KUJITEGEMEA. Kisha hayo Askofu alitoa tamko kuwa Sinodi Imezinduliwa.

Ilikuwa ni siku nzuri na iliyosubiriwa kwa hamu sana na wanajimbo wote. Ikizingatiwa kuwa hii ndiyo Sinodi ya Kwanza ya Jimbo wengi wana hamasa ya kuwa washiriki katika tukio hili kubwa la kihistoria katika Jimbo. Kote jimboni sasa salamu inayotawala ni: Sinodi Musoma: Imani na Matendo, ndiyo salamu ya Sinodi.

Baadhi ya waamini waliopata nafasi ya kuzungumza na mwandishi wa makala hii hawakusita kuonesha hisia zao za furaha na matumaini makubwa kuwa adhimisho la Sinodi litafanikiwa kuliongezea jimbo uhai na ustawi.

SINODI MUSOMA: IMANI NA MATENDO.
Waweza kupata habari zaidi kuhusu Sinodi kwa kutembelea blogu: au kwa kujiunga ukurasa wa Facebook:

Imeandaliwa na Padre Alfred Kwene,
Jimbo Katoliki la Musoma.








All the contents on this site are copyrighted ©.