2013-05-25 10:42:35

Papa atuma salam na matashi mema kwa wananchi wa Lebanon na Yordan


Kardinali Leonardo Sandri, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Makanisa ya Mashariki anafanya hija ya kichungaji nchini Lebanon na Yordan. Pamoja na mambo mengine Kardinali Sandri anashiriki katika Ibada na maadhimisho mbali mbali ya Kiliturujia pamoja na Maaskofu na Waamini wa Makanisa ya Mashariki. Ziara hii ambayo ameianza hapo tarehe 24 Mei, 2013 inatarajiwa kukamilika hapo tarehe 30 Mei 2013.

Lengo kuu la hija hii ya kichungaji ni kwa ajili ya kuombea amani nchini Syria, Lebanon na Mashariki ya Kati kwa ujumla. Kardinali Sandri anapenda kuwajulisha viongozi wa dini, waamini na watu wote wenye mapenzi mema kwamba, hija hii ya kichungaji inalenga zaidi kuonesha moyo wa mshikamano na upendo kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko na kwamba, anawaombea na kuwapatia baraka zake za kitume katika: matumaini, shida na mahangaiko yao ya kila siku.

Katika hija yake, Kardinali Sandri atapata pia fursa ya kuzungumza na viongozi wa Makanisa ya Mashariki, Jumuiya za Kitawa, lakini kwa namna ya pekee na vijana wanaoendelea kujitolea kwa ajili ya kuwahudumia wakimbizi kutoka Syria. Hawa ni wale vijana ambao wanashirikiana bega kwa bega na Caritas Lebanon.

Baba Mtakatifu Francisko akizungumzia kuhusu tatizo la wakimbizi anasema kwamba, Jumuiya ya Kimataifa haiwezi kuendelea kukaa kimya wakati watu wanateseka kiasi hiki kwa kupokonywa haki zao msingi. Wakimbizi wanalazimika kuyahama makazi yao kwa nguvu, changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa na Kanisa kuwasaidia kwa hali na mali.

Kardinali Sandri akiwa nchini Jordan atazungumza na viongozi pamoja na waamini waliko kwenye eneo hili. Alhamisi tarehe 30 Mei, Kardinali anatarajiwa kuhudhuria uzinduzi wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Madaba, kinachomilikiwa na kuendeshwa na Upatriaki wa Yerusalemu. Tukio hili la kihistoria linatarajiwa kuhudhuriwa na Mfalme Abdallah wa pili kutoka Yordan.

Kabla ya kurejea mjini Roma, Kardinali Sandri atatembelea kambi ya wakimbizi waliokimbia kutoka Syria na baadhi ya nchi zilizoko Mashariki ya Kati, ili kujionea mwenyewe hali halisi pamoja na kuwasilisha salam na matashi mema kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko anayeendelea kufuatilia kwa karibu zaidi hali ya wakimbizi huko Mashariki ya Kati.







All the contents on this site are copyrighted ©.