Mwenyeheri Don Giuseppe Puglisi alisimama kidete kupambana na Kikundi cha Mafia hata
akayamimina maisha yake kwa ujasiri mkuu!
Rais Giorgio Napolitano wa Italia amemwandikia barua Kardinali Paolo Romeo, Askofu
mkuu wa Jimbo kuu la Palermo, katika Maadhimisho ya Ibada ya kumtangaza Don Giuseppe
Puglisi kuwa mwenyeheri. Rais Napolitano anasema kwamba, anaungana na wote wanaoadhimisha
tukio hili la kihistoria ambalo Padre Puglisi alilionesha kwa njia ya ushuhuda wa
maisha yake ya Kikristo, kiasi hata cha kuyamimina maisha kama kielelezo cha ukarimu
na ujasiri wa hali ya juu.
Mauaji ya Don Puglisi yalisababisha majonzi na
masikitiko makubwa miongoni mwa wananchi wa Italia, lakini bado kuna kumbu kumbu hai
katika mawazo na mioyo ya wananchi wengi wa Italia kutokana na mchango wake mkubwa
katika shughuli za kichungaji huko Sicilia. Ni kielelezo makini cha mtu ambaye amesimama
kidete kupambana kufa na kupona na kikundi cha Mafia.
Itakumbukwa kwamba, Don
Puglisi aliuwawa kikatili na Kikundi cha Mafia kutokana na chuki za kiimani hapo tarehe
15 Septemba 1993. Ametangazwa kuwa Mwenyeheri tarehe 25 Mei 2013.