2013-05-25 07:36:25

Mwaka wa Imani: Fumbo la Utatu Mtakatifu


Maadhimisho ya Mwaka wa Imani ni fursa makini kwa waamini kukiri, kuadhimisha, kumwilisha na kusali imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Leo katika studio za Radio Vatican tunaye Padre Simoni Masondole anayetutafakarisha kuhusu Fumbo la Utatu Mtakatifu. RealAudioMP3
Mpendwa msikilizaji, leo kanisa linaadhimisha Sherehe ya Utatu Mtakatifu «Baba, Mwana na Roho Mtakatifu», Mungu mmoja katika nafsi tatu. Sherehe hii ilianza kuadhimishwa katika liturujia toka zama za kati za kukua na kuenea kwa ukristo duniani. Neno au jina «Utatu Mtakatifu» linatumika katika liturujia kuonesha imani yetu katika ukweli kuwa: «Mungu mmoja (Warumi 3:30) amegawanyika katika nafsi tatu», yaani Mungu Baba (1 Wakorintho 8: 6), Mungu Mwana (Yohane 1:1) na Mungu Roho Mtakatifu (1 Wakorintho 6: 19), kama tusomavyo na kukiri katika Mafundisho na imani ya Kanisa letu.
Ushuhuda wa Fumbo hili la «Utatu Mtakatifu» katika historia ya liturujia ya kanisa, umewekwa bayana na kwa msisitizo mkubwa kabisa katika Kanuni ya Kiriimani yaani Nasadiki tusaliyo kila mara, lakini pia katika Kiriimani ya zamani kabisa ya Mtakatifu Athanasio, ambayo inaweka bayana kuwa Baba ni Mungu, Mwana ni Mungu na Roho Mtakatifu ni Mungu. Na bado hawa si miungu watatu bali Mungu mmoja katika nafsi tayu au Utatu Mtakatifu.
Katika Utatu huu Mtakatifu, Yesu ni mwana wa pekee wa Mungu bila kuumbwa na Roho Mtakatifu ni zao (tunda) la upendobadilishana wa milele kati ya Mungu Baba na Mungu Mwana. Nafsi zote hizi tatu za Mungu ni za milele na zote ni sawa. Hazijaumbwa na zote zina uwezayote, ujuayote na pia ujuakabla ulio sawasawa.
Mpendwa msikilizaji, katika Maandiko Matakatifu, hakuna hata kifungu kimoja kinacho taja, au kutamka waziwazi jina au neno «Utatu Mtakatifu». Hakuna pia kifungu kinacho onesha waziwazi kuwa Mungu mmoja yuko katika nafsi tatu kwa kuandika, isipokuwa baadhi ya vifungu fulanifulani tu katika maagano yote mawili vina dokeza au kuonesha juu ya Utatu Mtakatifu bila kusema kuwa Mungu ni «Mtatu». Mfano mzuri ni Mwanzo 1: 26- «na tufanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyana na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa [...]», Pia Matayo 28:19 «Basi nendeni mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu [...]».
Katika historia ya liturujia ya Kanisa, hulka hii ya Mungu mmoja katika nafsi tatu na jina hili la Mungu mmoja katika «Utatu Mtakatifu» linanza kutumiwa na mababa wa kanisa toka zama za awali kabisa za historia ya liturjia yetu. Theophilius wa Antiokia kati ya mwaka 180 B.K anafundisha juu ya Utatu Mtakatifu yaani «Mungu Baba, Neno wake na Hekima wake». Baadaye neno «Utatu Mtakatifu» linatumiwa na Tertuliano katika mafundisho yake. Hulka hii pia ya Mungu mmoja katika Nafsi tatu tunaikuta katika kazi na Mafundisho ya kiibada ya Origeni na ya Gregori Thaumaturgus.
Mpendwa msikilizaji, inatulazimu kukiri wazi, jinsi ilivyo vigumu kulieleza kinagaubaga, kwa uwazi na uhakika, au kulifafanua kwa ufasaha kabisa fumbo hili la «Utatu Mtakatifu», hadi likaeleweka kama tujuwavyo kuwa 1+1+1 = 3 au 1+1 = 2, au 2+1 = 3. Kwa fumbo hili akili yetu hubaki nyembamba bila kujua maana yote ya Utatu Mtakatifu. Padre Malema Lui Mwanampepo anafundisha kuwa kazi zote endanje za Mungu ni tunda la Utatu Mtakatifu. Hii inamaanisha kuwa uumbaji ni kazi ya nafsi zote tatu, ukombozi ni kazi ya nafsi zote tatu na hata msamaha wa dhambi ni kazi ya Utatu Mtakatifu.
Lakini Professa Mwanampepo anakiri kuwa hatuwezi kuuelewa bayana utatu Mtakatifu na siri zake zote. Anapofikia katika hatua hii ambapo akili haiwezi tena kwenda mbele, anasema ni sharti tuiachie imani ili iweze kufanya kazi yake, kama wimbo huu ulio tunda la mafundisho yake usemavyo na kuimbwa: «pendo lako Bwana Yesu ni hazina ya uwema wote. Washuka kutoka juu, waniijia hapa duniani, imani tu, imani tu, imani tu yaelewa». Hakika ni imani tu, ndiyo iwezayo kushamiri katika fumbo hili na siyo akili, fahamu wala kufikiri sana kwetu.
Simulizi nzuri na ya kusisimua, inasimuliwa juu ya jitihada za kutaka kulielewa na kulifundisha Fumbo la «Utatu Mtakatifu» alizokuwa nazo Mtakatifu Agostino wa Hippo, na jinsi ambavyo hazikuweza kufua dafu kwa kulifumbua Fumbo hili: Asubuhi moja huku akiwa katika tafakari zake za kitaaluma juu ya Utatu Mtakatifu, Agostino alifika baharini akitembea ufukweni. Mbele yake kwa mbali aliona mtoto aliyekuwa ameshikilia kopo lake mkononi huku mara kadhaa akiwa anakimbia baharini na kuchota maji kwa kopo hilo, kisha kuyamwaga katika kishimo kidogo alichokuwa amekichimba ufukweni mwa bahari.
Agostino alivuta hisia na subira ili apate kuona. Baada ya kuona na kushangazwa na kazi ya mtoto huyo, alivunja ukimya, kwa kumwuliza:«mtoto unafanya nini?» na yeye alijibu kwa nidhamu:«ninajaribu kuihamishia bahari yote hii katika kishimo changu hiki nilicho kichimba hapa». Agostino kwa mshangao alicheka na kumwambia: «mtoto kitu hiki hakiwezekaniki». Kwa mshituko na mshangao pia, mtoto alimwambia «na wewe ni waajabu sana kufikiri kuwa ukweli juu ya Mungu katika Utatu Mtakakatifu utaumalizia katika kichwa chako hichi kidogo!» kisha mtoto yule alitoweka kwa miujiza, na Agostino akabaki bila kulijua kwa undani wote Fumbo hili la Utatu Mtakatifu.
Mpendwa msikilizaji, Je, kuna namna yoyote ile ambayo sisi leo twaweza itumia kulijua au kulieleza Fumbo hili la Utatu Mtakatifu kwa mapana na marefu yake? Kwa hakika jibu ni hapana hatuwezi kumjua Mungu kama alivyo kabisa katika fumbo hili. Ila mifano mbalimbali kutoka katika maumbile yatuzungukayo inatusaidia walau kupata picha au wazo fulani juu ya Utatu Utakatifu na hivyo kujibu shaka na dukuduku tulizonazo juu ya Fumbo hili.
Hebu angalia mkono wako! Ni wazi kuwa kwa kawaida una vidole vitano kila mmoja; lakini ukweli ni kuwa vidole hivi vyote ni tofauti, ila vinaishia kuwa mkono mmoja. Je, Umewahi kuangalia pua yako? Ina matundu au matobo mawili, lakini yote yanaishia kuwa upenyo/mlango/ au uwazi mmoja kwa ndani na kufanya kazi kama kiungo kimoja. Na midomo yako je? Japo ipo juu na chini yote inaishia kuwa kinywa kimoja.
Mpendwa msikilizaji, Mtakatifu Patrick wa kisiwa cha Ireland, wakati wa Uinjilishaji wake kisiwani huko, huku akitamani kulielezea Fumbo la Utatu Mtakatifu alitumia jani lenye vitanga 3 (Shamrock leaf/au trifolium dubium) ili kutoa picha na taswira, jinsi ambavyo Utatu Mtakatifu unafanana katika umoja, upendo na kazi yake. Matokeo yake, hadi leo Wakristo wa Ireland wana desturi ya kubeba jani hilo, siku ya tarehe 17 Machi huku wakimkumbuka Mtakatifu Patrick na fundisho lake hilo maridhawa juu ya Fumbo la Utatu Mtakatifu.
Sisi leo tunajifunza kuwa Mungu mmoja katika nafsi tatu hufanya kwa shirika kazi zote endanje za ukombozi wa mwanadamu bila kubaguana wala kutegeana. Je, sherehe hii inatufundisha nini zaidi? Inafundisha kujua kuwa Mungu ni upendo na kuwa yeye ndiye familia ya kwanza kabisa ya kuigwa na watu wote. Ni lazima pia sisi tujifunze kupendana, kuheshimiana, kama ndugu na marafiki katika familia na mitaani tuishiko. Tijibidishe kupendana sote kila wakati kwani tumekombolewa kwa Damu Azizi ya Yesu Kristo na kutakatifuzwa na Roho Mtakatifu anayeendelea kuliongoza Kanisa.
Maadhimisho ya Mwaka wa Imani yawe ni fursa makini ya kujifunza ili kuifahamu imani ambayo tunapaswa kuikiri kwa vinywa vyetu; kuiadhimisha katika Sakramenti za Kanisa; kuimwilisha katika matendo mema na adili pamoja ns kuisali.
Kutoka Studio za Radio Vatican, mimi ni Padre Simon Masondole kutoka Jimbo Katoliki la Bunda, Tanzania.








All the contents on this site are copyrighted ©.