2013-05-25 11:40:38

Kigoda cha Kardinali Bernardini Gantini chaanzishwa Roma ili kuwafunda viongozi wa Afrika!


Chuo Kikuu cha Kipapa cha Laterani kilichoko mjini Roma, kimeanzisha Kigoda cha Kardinali Bernardini Gantini, kutoka Benin, Kardinali wa kwanza mwafrika kupewa dhamana ya kushiriki kuliongoza Kanisa la Kiulimwengu akiwa mjini Vatican. Kigoda cha Kardinali Gantini kitajihusisha zaidi na masuala ya Siasa za Kijamii Barani Afrika.

Tamko hilo limetolewa na Kardinali Robert Sarah, Rais wa Baraza la Kipapa linaloratibu misaada ya Kanisa Katoliki "Cor Unum"; hafla ambayo imehudhuriwa pia na Dr. Thomas Yayi Boni, Rais wa Benin pamoja na viongozi wengine kutoka Vatican na Chuo Kikuu cha Kipapa cha Lateran.

Kardinali Bernardini Gantini alizaliwa kunako mwaka 1922 nchini Benin. Mara baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi akapewa Daraja Takatifu la Upadre mwaka 1951. Baada ya miaka miwili ya utume nchini Benin, aliondoka na kuelekea mjini Roma kuendelea na masomo zaidi kwenye Chuo Kikuu cha Kipapa cha Laterani, ambako alijipatia shahada ya uzamili katika masuala ya Taalimungu na Sheria za Kanisa.

Kunako mwaka 1956 aliwekwa wakfu kuwa Askofu na mwaka 1960 akateuliwa kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Cotonou, Benin. Akiwa Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Benin alishiriki vikao vitatu vya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Kardinali Gantini alibahatika pia kushiriki katika Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu iliyofanyika kunako mwaka 1967. Baba Mtakatifu Paulo wa sita akamteuwa kuwa Kardinali kunako mwaka 1977 na hapo akapewa dhamana ya kuwa ni Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Maaskofu.

Kunako mwaka 1993 alichaguliwa kuwa ni Dekano wa Makardinali. Alipofikisha umri wa miaka 80 aling'atuka kutoka madarakani na kuamua kurudi nchini mwake Benin. Kunako mwaka 2008 Kardinali Gantini alifariki dunia akiwa mjini Paris, Ufaransa alikokuwa amekwenda kwa ajili ya kupata matibabu. Akazikwa mjini Ouidah.

Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita alipotembelea nchini Benin kunako mwaka 2011, ili kuwasilisha matunda ya Maadhimisho ya Awamu ya Pili ya Sinodi ya Maaskofu wa Afrika, alipata pia fursa ya kutembelea kaburi la Kardinali Bernardini Gantini ambaye walifanya kazi kwa pamoja kwa miaka kadhaa mjini Vatican.

Kardinali Robert Sarah anasema uamuzi wa Chuo Kikuu cha Kipapa cha Lateran kuanzisha kigoda cha Kardinali Bernardini Gantini kuna maanisha kufanya rejea ya maisha, utume na vipaumbele vya Hayati Kardinali Gantini kwa Benin, Afrika na kwa Kanisa la Kiulimwengu. Ni matumaini ya Kardinali Sarah kwamba, Kigoda cha Kardinali Bernardini Gantini kitasaidia kuanzisha mchakato wa masuala ya kisiasa Barani Afrika, kama sehemu ya maandalizi ya viongozi wa baadaye wa Bara la Afrika, wataongozwa na Mafundisho Jamii ya Kanisa.

Dr. Martin Nkafu Nkemkia kutoka Dawati la Afrika anasema, Kigoda hiki kinapania kuendesha kozi, semina, warsha na makongamano. Kitashirikiana na Taasisi pamoja na watu mbali mbali ili kuthaminisha zaidi utamaduni na siasa za Bara la Afrika. Kigoda hiki kitakuwa ni mahali pa kuwafunda viongozi wa Bara la Afrika kwa siku za usoni; kwa kuzingatia maadili yatayosaidia kupambana na mmong'onyoko wa kimaadili na utu wema; rushwa na ufisadi, ili kujenga tena matumaini mapya kwa wananchi Barani Afrika.

Watakaofundwa kwenye Kigoda cha Kardinali Bernardini Gantini wanapaswa kuwa kweli ni watu wa huduma, watakaosimama kidete kutetea mafao ya wengi.







All the contents on this site are copyrighted ©.