Ziara ya kikazi ya Rais Barack Obama Barani Afrika!
Taarifa kutoka Ikulu ya Marekani inaonesha kwamba, Rais Barack Obama wa Marekani kuanzia
tarehe 26 Juni hadi tarehe 3 Julai 2013 atakuwa na ziara rasmi ya kikazi Barani Afrika
na atapata fursa ya kutembelea Senegal, Afrika ya Kusini na Tanzania. Itakumbukwa
kwamba, kwa mara ya kwanza Rais Obama alitembelea Ghana kunako mwaka 2009, kwa kukazia
kwamba, Bara la Afrika litaendelezwa na Waafrika wenyewe! Misaada inayotolewa na Jumuiya
ya Kimataifa na Wahisani mbali mbali iwe ni kikolezo cha maendeleo ya Watu wa Bara
la Afrika, sanjari na kudumisha utawala bora. Katika ziara hii, Rais Obama atapata
fursa ya kukutana na viongozi wa Serikali, Wafanyabiashara na wadau mbali mbali. Ziara
ya Rais Obama nchini Afrika ya Kusini, inaweza kuwa ni fursa ya pekee kwake kuweza
kukutana na kuzungumza na Mzee Nelson Mandela, ambaye kwa siku za hivi karibuni afya
yake imekuwa na mgogoro. Wachunguzi wa mambo wanasema, Rais Obama kwa mara ya kwanza
alikutana na Mzee Madiba kunako mwaka 2005 wakati ambapo Obama alikuwa bado ni Seneta.
Ziara ya Rais Obama Barani Afrika, inasema Ikulu ya Marekani ni kuendeleza ushirikiano
wa kimataifa na nchi za Kiafrika, kwa kuwekeza zaidi katika masuala ya uchumi, biashara
na maendeleo endelevu ya watu hasa Kusini mwa Jangwa la Sahara, bila kusahau umuhimu
wa kudimisha demokrasia na utawala wa sheria. Ni wakati muafaka kwa nchi za Kiafrika
kuwekeza katika teknolojia rafiki pamoja na kuwajengea uwezo vijana ili kushiriki
katika mchakato wa kujiletea maendeleo yao. Uamuzi wa Rais Obama kutotembelea Kenya
kwa mara ya pili tangu achaguliwe, kumewafanya baadhi ya wananchi wa Kenya kujiuliza
maswali yasiyokuwa na majibu muafaka. Wanasema, pengine ni fursa kwa wanasiasa wa
Kenya kujichunguza zaidi ili kurekebisha kasoro zinazoifanya kutengwa katika matukio
kama haya. Rais Obama kabla ya kuanza ziara yake Barani Afrika, hapo tarehe 7
hadi tarehe 8 Juni, 2013 kwa mara ya kwanza atakutana na kuzungumza na Rais Xi Jinping
wa China ambaye amechaguliwa hivi karibuni. Inawezekana ziara hii ikawa ni jukwaa
la kuweza kubadilishana mawazo kuhusu masuala kadhaa kati ya Ulaya na Asia kabla ya
Wakuu wa G 20 kufanya mkutano wao huko Pitisburg. Wakati huo huo, Waziri wa Mambo
ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Tanzania, Bernard Membe amesema ujio wa Rais
wa Marekani Barack Obama ni wa umuhimu kwa nchi kwani utaipatia Tanzania zaidi ya
dola milioni 800 (sawa na Sh. Trilioni 1.3) kwa ajili ya kukamilisha Malengo ya Maendeleo
ya Milenia. Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe amesema
ujio wa Rais wa Marekani Barack Obama ni wa umuhimu kwa nchi kwani utaipatia Tanzania
zaidi ya dola milioni 800 (sawa na Sh. Trilioni 1.3) kwa ajili ya kukamilisha Malengo
ya Maendeleo ya Milenia ifikapo mwaka 2015. Membe alisema fedha hizo zitasaidia
kukamirisha miradi mbalimbali katika sekta za barabara, maji na elimu, akiwa nchini
Rais Obama ataongozana na ujumbe wa wafanyabiashara 700.