2013-05-24 08:43:19

Sherehe ya Fumbo la Utatu Mtakatifu


Mpendwa msilikilzaji wa Neno la Mungu, leo tunaadhimisha Fumbo la Utatu Mtakatifu. Ni sherehe kati ya sherehe za Bwana ambayo huadhimishwa Dominika inayofuata mara baada ya Pentekoste. RealAudioMP3

Mama Kanisa ameweka sherehe hii baada ya Pentekoste kwa sababu anajua tayari fumbo zima la Utatu Mtakatifu limekwishafunuliwa kwetu. Na kwa namna hiyo Mama Kanisa apenda kutuingiza furaha ijayo kwetu kila siku kwa njia ya Utatu Mtakatifu.

Anatushirikisha Fumbo la Mungu kukaa nasi daima mpaka mwisho wa maisha ya utume wetu hapa duniani. Kwa njia ya fumbo hili upendo wa Mungu kwa wanadamu unafunuliwa hatua kwa hatua tokea Agano la Kale hadi Agano Jipya. Basi, ninakualika kutafakari Neno la Mungu kwa furaha kuu ukitambua kuwa kwa njia ya Utatu Mtakatifu umekuwa mwana wa Mungu.

Kwa hakika Fumbo la Utatu Mtakatifu si fumbo rahisi kulielewa linadai imani kama ambavyo atatuambia Mtume Paulo katika somo la Pili na latudai Hekima kama ambavyo tutasikia katika somo la kwanza. Mmoja anaweza kukata tamaa akisikia habari ya fumbo hili kwa maana ya kuwa UMOJA usiogawanyika na wakati fulani kuonekana katika WINGI=Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Mpendwa kimahesabu mantiki haitupi jibu, kumbe yatupasa kwenda katika mantiki ya Kitaalilimungu na Kiimani zaidi.

Ndiyo kusema yatupasa kutosahau kabisa kuwa imani si kukubali kiurahisi habari ya ukweli wa kidini bali kuukumbatia na kuuishi ukweli huo katika ugumu wake. Mantiki hii ndiyo mantiki ya neno kuaamini kwa kiebrania. Kwa njia ya imani lazima kuweka akili zetu na maonjo yetu kwa Mwenyezi Mungu. Kwa mantiki hiyo kuwa na imani si kusadiki katika Utatu Mtakatifu tu bali kuambatana na Utatu Mtakatifu, kuishi katika Utatu na kujisalimisha na kujitumainisha katika fumbo hilo.

Tunasikia katika somo la kwanza, katika kitabu cha Mithali, 8:22-31 Mwandishi akitafakari uwepo wa Hekima ya Mungu kabla ya kuumbwa vitu vyote. Anatuambia kuwa kwa njia ya Hekima hiyo vitu vyote viliumbwa. Mwandishi anaweka sura ya mtu katika maneno akisema “wakati visipokuwako vilindi, nalizaliwa, na pia katika sura ya kwanza ya Mithali anaanza kwa kusema “sikilizeni hekima anaita, busara anapaaza sauti yake, enyi watu wangu nawaita ninyi, wito wangu ni kwa ajili ya binadamu” Kwa namna hii Hekima ya Mungu ni hai.

Kwa hakika mwandishi anataka kukuza maarifa akituelekeza katika hekima iliyo kuu yaani kumtambua na kumcha Mungu. Nasi tokea kuhuishwa kwa Hekima hiyo tunapata kufahamu na kutambua kuwa fumbo la Utatu Mtakatifu lilianza kudokezwa polepole katika maandiko ya Agano la Kale. Kristo ndiye Hekima ya Mungu ambaye katika Injili ya Yohane 1:1 na kuendelea tunasikia Bwana akisema hapo mwanzo alikuwako Neno na Neno alikuwa kwa Mungu na Neno huyo ni Mungu ambaye kwa njia yake vitu vyote viliumbwa. Kumbe kwa Hekima katika Agano la Kale vitu viliumbwa ni kwa Hekima hiyo katika Agano jipya vitu vimefanywa upya yaani kugeuzwa toka utumwa na kuwa wana wa Mungu.

Tukisoma katika Injili ya Matayo 11:19 tunaona jinsi Hekima ya Mungu hujidhirisha yenyewe kwa matendo yake. Ndiyo kusema ni njema na haihitaji kupigiwa mabango na kuitangaza kwa ushupavu bali upendo na Hekima yenyewe vinatosha. Katika Barua ya 1Kor, 1:24 Mtakatifu Paulo anasema, lakini kwa wale walioitwa, Wayahudi kwa Wagiriki, Kristo ni nguvu ya Mungu na Hekima ya Mungu. Kumbe ndugu yangu mpendwa, katika mantiki hii tunaweza kusema na tunaamini kuwa hekima tuisikiayo katika somo la I ni Kristu Mwenyewe katika matayarisho ya kufunua Utatu Mtakatifu.

Kama lilivyokuwa lengo la mafundisho ya hekima katika Agano la Kale na kama lilivyo lengo la Mithali katika makabila yetu mwaliko ni kumcha Bwana na hapo ndipo kuna kukua katika Hekima, na kutenda kinyume ni kupoteza dira ya maisha yako. Utajiri wote uko katika Neno la Mungu na Ekaristi Takatifu vitujiavyo kwa njia ya Kanisa. Basi ndugu yangu mpendwa, tukumbuke Mungu wetu ni upendo usio na mwisho, usio na ubaguzi bali mkamilifu.

Mtume Paulo anapowaandikia Warumi anawakumbusha zawadi ya Imani, inayotokana na mafundisho ya Bwana wetu Yesu Kristo akisema kwa njia ya imani sisi tunapata kuhesabiwa haki na amani kwa Mungu. Kumbe ni kwa njia ya Yesu Kristo tunapata kumwendea Mwenyezi Mungu.

Akitambua pia kwamba katika kutekeleza utume wake Bwana wetu Yesu Kristu aliteswa, anawakumbusha pia Warumi wanaoteswa watambue na kuvumilia mateso yao kwa maana katika dhiki kuna saburi na kazi ya saburi ni uthabiti wa moyo, na kazi ya uthabiti wa moyo ni tumaini. Mtume Paulo anasonga mbele akifundisha namna ambavyo tumepokea pendo la Mungu, anasema Roho Mtakatifu tuliyepewa amemimina pendo hilo katika mioyo na kwa namna hiyo tumefanywa wana wa Mungu.

Ewe rafiki yangu mpendwa oneni jinsi Roho Mtakatifu alivyochimbuko la kila aina ya zawadi za kimungu. Kumbe, tunaposhangilia na kusherehekea fumbo la Utatu Mtakatifu tunashangilia na kumshukuru Mungu kwa zawadi mbalimbali alizotujalia. Tunashangilia hasa lile fumbo la sisi kufanywa wana wana wa Mungu.

Mwinjili Yohane katika sehemu ya Injili yake anajenga polepole hoja ya Utatu Mtakatifu akinukuu maneno ya Bwana akisema kwa wanafunzi wake, ninayo mengi ya kuwaambia lakini hamtaweza kuyaelewa mpaka ajapo Roho wa kweli na kuwaongoza akiwatia kweli yote na kwa njia hiyo akinitukuza mimi. Na kisha mwishoni atatangaza kuwa yeye na Baba yake ni wamoja. Mwinjili Matayo katika Mwaka B anatangaza Utatu akimnukuu Bwana anayewaagiza wanafunzi wakaende duniani kote wakifundisha na na kubatiza katika Utatu Mtakatifu.

Mpendwa, Yohane atufundisha kuwa ukweli na ujuzi wa kumjua Mungu ni safari. Kwanza ametufunulia yote Yesu Kristu nafsi ya pili ya Mungu na kisha anatukabidhi kwa Roho Mtakatifu, Pentekoste mpya na yote yanakamilika katika Baba yake wa Mbinguni. Roho Mtakatifu anatumwa na Baba yake kama kumbukumbu hai ya Mwanaye mpenzi Yesu Kristo hapa duniani. Ni kwa njia ya Roho Mtakatifu Neno la Mungu huendelea kuwa hai kama ambavyo lilikusudiwa na Bwana mwenyewe.

Kwa njia ya Roho Mtakatifu Mungu huendelea kutenda kazi yake akiongoza taifa lake kuelekea Yerusalemu mpya. Ni kwa njia ya Roho wa Mungu Mungu hujionesha kwetu aliye zawadi hasa anapotuondolea dhambi.

Ni kwa njia ya Roho Mtakatifu Mungu Baba na Mwana kama tusikiavyo Mwinjili Matayo anavyomalizia Injili kwa ahadi ya Kristo kuwa pamoja nasi mpaka ukamilifu wa dahari. (Mt 28:20) Kwa habari hii njema ya furaha yakuwa Bwana yu pamoja nasi yatuonesha kuwa Utatu Mtakatifu ni upendo mkamilifu kwa wote na kwa vizazi vyote.

Mpendwa mwana wa Mungu katika utangulizi nilijaribu kujenga mantiki ya Utatu Mtakatifu sasa tunaliweka fumbo katika uhalisia wa maisha ya Kanisa. Kwa kawaida ni fumbo kuu kati ya mafumbo makuu matatu, yaani fumbo la Ekaristi Takatifu na umwilisho, fumbo la neema za Mungu na Utatu Mtakatifu ambao ndio tunasherehekea leo. Ni fumbo ambalo si rahisi kulielewa kwa undani na ukamilifu wake kwa maana ndiyo Mungu mwenyewe. Tunachotambua ni kuwa Mungu Baba ni muumbaji, na alipokwisha kuumba mbingu na nchi alimtuma Mwanae ili aokoe mwanadamu aliyepoteza uzuri aliokabidhiwa na Mungu Baba na hivi Mungu Mwana ni Mkombozi.

Mwana alipokwisha kufundisha na kumaliza kazi yake kabla ya kupaa mbinguni alihaidi kumpeleka Roho Mtakatifu mfariji na mwalimu atakayetukumbusha yote na tena hatafanya kinyume na yale yaliyofundishwa na Bwana. Kumbe mpendwa Utatu Mtakatifu ni Mungu mmoja lakini nafsi tatu zisizogawanyika, yaani Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Kutambua na kujaribu kuelewa tunahitaji kuwa na imani thabiti kama nilivyokwishadokeza hapo mwanzoni.

Ninakutakieni sherehe njema, ukajazwe imani, maisha yako yote katika Utatu Mtakatifu. Tumsifu Yesu Kristo.

Tafakari hii imeletwa kwako na Padre Richard Tiganya, C.PP.S.







All the contents on this site are copyrighted ©.