Mafanikio ya Kijiji cha Matumaini, Jimboni Dodoma, Tanzania
Padre Vincent Boselli, Muasisi wa Kijiji cha Matumaini kinachomilikiwa na kuendeshwa
na Masista Waabuduo Damu Takatifu ya Yesu, kilichoko Jimbo Katoliki Dodoma anasema,
Kijiji cha Matumaini kimepata mafanikio makubwa katika utoaji wa huduma kwa watoto
walioathirika na ugonjwa wa Ukimwi kanda ya Kati, nchini Tanzania. Katika kipindi
cha zaidi ya miaka kumi, watoto waliofariki dunia ni kidogo sana, ikilinganishwa na
hali halisi ya athari za ugonjwa wa Ukimwi.
Watoto wanaohudumiwa
kwenye Kijiji cha Matumaini afya zao zimeendelea kuboreka na sasa wako Kidato cha
Nne, wako kifua mbele wanajiandaa kufanya mitihani ya Kidato cha Nne kwa Mwaka 2013.
Idadi ya watu wanaohudumiwa kwenye Kijiji cha Matumaini imeendelea kuongezeka maradufu,
hii inatokana na ukweli kwamba, watu wanathamini na kupenda huduma ya tiba na kinga
inayotolewa kwenye Kijiji cha Matumaini.
Huduma ya kuzuia maambukizi ya virusi
vya Ukimwi kutoka kwa Mama mjamzito kwenda kwa Mtoto zinazidi kuboreka mwaka hadi
mwaka, hadi sasa takwimu zinaonesha kwamba, kuna watoto 400 wamezaliwa na wanawake
waliokuwa na Ukimwi, lakini watoto ni salama salimini. Kuna zaidi ya watu 2,900 wanaohudumiwa
kwenye Kijiji cha Matumaini.