OAU inaadhimisha Jubilee ya Miaka 50 tangu ilipoanzishwa!
Maadhimisho ya Jubilee ya miaka 50 ya Umoja wa Nchi Huru za Kiafrika, OAU ambao kwa
sasa unajulikana kama Umoja wa Afrika yameanza kutimua vumbi mjini Addis Ababa, Jumatano
tarehe 22 Mei 2013 na kilele cha Maadhimisho haya ni Jumamosi, tarehe 25 Mei 2013.
OAU imetekeleza madhumuni yake kwani leo hii nchi zote Barani Afrika zimejipatia
uhuru wa bendera na zinaendelea kujikwamua katika masuala ya kiuchumi, kijamii na
kisiasa. Utawala wa ubaguzi wa rangi Afrika ya Kusini umeng'olewa, leo Afrika ya Kusini
ni kitovu cha maendeleo Kusini mwa Afrika.
Katika Maadhimisho haya, Wakuu
wa Umoja wa Afrika watajiwekea mikakati na maazimio kwa ajili ya utekelezaji katika
kipindi cha miaka mingine 50 ijayo katika masuala ya kiuchumi, kisiasa na kijamii.
Umoja wa Afrika una jumla ya wanachama 53 na umekuwa ni kiungo kikuu na sauti ya Bara
la Afrika katika masuala mbali mbali. Umaskini, ujinga na magonjwa; haki, amani na
maendeleo endelevu ni kati ya changamoto zinazoendelea kuzikumba nchi nyingi za Bara
la Afrika.
Uzalendo ukipewa kipaumbele cha kwanza, rasilimali na utajiri uliomo
Barani Afrika ukatumika kwa ajili ya mafao ya wengi, Waafrika wanaweza kucharuka katika
maendeleo! Vinginevyo, Bara la Afrika litaendelea kudidimia! Viongozi mbali mbali
wanashiriki katika Maadhimisho haya.