2013-05-22 08:12:03

Watoto wa Bara la Afrika wanakoseshwa haki zao msingi


Wajumbe wa mkutano wa Umoja wa Afrika katika kikao chao cha ishirini na moja, kilichokuwa kinafanyika mjini Addis Ababa wanasema kwamba, kuna idadi kubwa ya watoto Barani Afrika ambayo haijulikani iliko kutokana na Jamii nyingi za Kiafrika kutokuwa na utamduni wa kuandikisha watoto wao wanapozaliwa. Takwimu za Shirika la Watoto la Umoja wa Mataifa zinaonesha kwamba, ni asilimia 44% tu ya watoto wenye umri chini ya miaka mitano wanaoandikishwa katika serikali zao.

Wajumbe hao wanabainisha kwamba, bila ya kuwa na takwimu kisheria, watoto wengi Barani Afrika wataendelea kukosa haki zao msingi sanjari na huduma za kijamii kama vile afya, elimu na kinga dhidi ya kazi za suluba na nyanyaso kwa watoto wadogo. Watoto wasipolindwa watapelekwa mstari wa mbele, wataweza kutumbukizwa kwenye biashara haramu ya binadamu na mifumo mbali mbali ya dhuluma na unyonyaji.

Hayo yamebainishwa wakati wa Maadhimisho ya Jubilee ya miaka 50 tangu Umoja wa Nchi Huru za Kiafrika, OAU ulipoanzishwa, changamoto kwa nchi za Kiafrika kuendelea kuwekeza zaidi katika ustawi na maendeleo ya watoto ambao ni taifa la leo na kesho yenye matumaini. UNICEF inasema, watoto wanapaswa kutambuliwa kisheria pamoja na kuandikishwa. Kusini mwa Jangwa la Sahara watoto wengi wanafanyishwa kazi za suluba.







All the contents on this site are copyrighted ©.