Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anaichangamotisha Msumbiji kupambana na umaskini pamoja
na magonjwa!
Umaskini wa hali na kipato na magonjwa ni kati ya changamoto kubwa zinazoikabili Msumbiji
katika kipindi, hata kama kuna utashi na mikakati ya kupambana na hali hii nchini
Msumbiji, kwani kuna dalili za maboresho ya hali ya kiuchumi na kijamii.
Ni
maneno ya Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Ban Ki-Moon mapema juma hili alipokuwa
anafanya ziara ya kikazi ya siku mbili nchini Msumbiji kabla ya kujiunga na Umoja
wa Afrika katika Maadhimisho ya Jubilee ya miaka 50 tangu Umoja wa Nchi Huru za Kiafrika
ulipoanzishwa.
Msumbiji imeonesha utashi wa kisiasa na kiuchumi katika kuwaletea
watu wake maendeleo endelevu mara baada ya vita ya wenyewe kwa wenyewe ambayo kimsingi
imekuwa ni kikwazo kikubwa cha maendeleo nchini Msumbiji. Kuna dalili za maendeleo
makubwa Barani Afrika yanayokwenda sanjari na uhru pamoja na utawala bora na watu
wanaonesha imani kubwa kwa Afrika iliyo bora kwa siku za usoni. Msumbiji ni mfano
na kielelezo cha kuigwa anasema, Bwana Ban Ki- Moon.
Hata hivyo bado kuna idadi
kubwa ya wananchi wengi Barani Afrika wanaoendelea kuogelea katika dimbwi la umaskini
na magonjwa, changamoto ya kuweka mikakati makini katika utekelezaji wa Malengo ya
Maendeleo ya Millenia ifikapo mwaka 2015. Bado Umoja wa Mataifa unaonesha wasi wasi
wa kuweza kufikiwa kwa Malengo haya lakini, umedhamiria kutekeleza mikakati hii ka
hali na mali. Athari za mabadiliko ya tabianchi bado zinaendelea kuleta maafa makubwa
sehemu mbali mbali dunia na Msumbiji imekuwa ikiathirika mara kwa mara.