2013-05-22 07:35:21

Jimbo Katoliki Musoma linaadhimisha Sinodi ya Jimbo! Matendo makuu ya Mungu


Maadhimisho ya Sherehe ya Pentekoste kwa Mwaka 2013 yamekuwa ni fursa ya pekee kwa Jimbo Katoliki Musoma, Tanzania kufungua Maadhimisho ya Sinodi ya Jimbo. Askofu Michael Msonganzila wa Jimbo Katoliki Musoma katika mahojiano maalum na Radio Vatican anabainisha mambo msingi yaliyopelekea Familia ya Mungu Jimbo Katoliki Musoma kuwa na Maadhimisho ya Sinodi kuanzia mwaka 2013 hadi Mwaka 2014. RealAudioMP3

Jimbo Katoliki Musoma lilianzishwa kunako tarehe 3 Oktoba 1957 na hayati Askofu John Rudin aliyeliongoza hadi kunako mwaka 1978. Mwaka 1979 Jimbo la Musoma likampata Askofu wa kwanza Mzalendo, Jubilee ya miaka 50 ya Jimbo Katoliki Musoma, Jubilee ya miaka 100 ya Ukristo Musoma, Jubilee ya Miaka 50 ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, Miaka 20 ya Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki, Sheria za Kanisa, Maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu wa Afrika sanjari na Maadhimisho ya Mwaka wa Imani ni sababu msingi za kuadhimisha Sinodi ya Jimbo Katoliki Musoma.

Sehemu ya kwanza ya malengo ya Sinodi inahusisha masuala ya maisha yetu kama Wakristo, yaani, wafuasi wa Kristo, na washiriki katika Ujenzi wa Ufalme wa Mungu mioyoni mwa ndugu zetu, ambayo ni pamoja na: kusali pamoja, kutafakari pamoja, kupanga pamoja, kutathimini pamoja.



Kuibua mawazo, kuyajadili na kuyatolea mapendekezo yenye mwelekeo wa kiutendaji katika utume wa Kanisa Jimboni Musoma. Kutazama tulikotokea, tulipo na tunapoelekea kiuchungaji, ki-uchumi, kiutendaji na maadhimisho ya Liturujia ili kukirithisha kizazi kijacho katika Imani ya Kikristo. Kujitengenezea “METANOIA”, yaani, mabadiliko ya kina, ya ndani kabisa kadiri ya Neno la Mungu na taratibu za Kanisa – kujiwekea MOYO WA NYAMA.

SABABU ZA KUWA NA SINODI YA JIMBO LA MUSOMA: 2013/ 2014
Miaka zaidi ya 100 ya Uinjilishaji: Nawaalika wote tuliomo kwenye ukumbi huu, tuendelee kumshukuru Mungu kwa zawadi ya UHAI NA IMANI YA KIKRISTO. Katika Jimbo la Musoma, Imani ya Kikristo imekuwepo humu tangu mwaka 1911. Ni mwaka 2011 tumeadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu habari njema kuhubiriwa katika eneo hili.
Mwaka 2007 tuliadhimisha Jubilei ya Miaka 50 ya uwepo wa Jimbo Katoliki la Musoma. Matukio yote haya mawili yanatupatia fursa ya kujiandaa kikamilifu kuitafiti kwa kina Historia ya Jimbo letu tukianzia na Shirika la Wamisionari wa Afrika (White Fathers) waliofika kwanza eneo hili, na baadaye kufuatiwa na Shirika la Wamisionari wa Maryknoll. Iko haja ya kutamani sana kwa macho, masikio na kiimani kurithisha na kuendeleza jitihada za mwanzo za uinjilishaji wa wamisionari wa Afrika na pia wamisionari wa Maryknoll.
Miaka 50 ya Mtaguso wa Mkuu wa II wa Vatican: Historia ya Kanisa miaka 50 iliyopita inatufundisha kuwa mnamo tarehe 11 Oktoba,1962, Baba Mtakatifu Yohane wa XXIII, aliitisha MTAGUSO MKUU WA PILI WA VATICAN ambao ulisisitiza sana kuwa KANISA LIJITATHIMINI UPYA, LIJIREKEBISHE UPYA, LIJITAZAME UPYA, LIJICHUNGUZE, LIFANYE MAREKEBISHO NA MAGEUZI HALALI KUENDANA NA HALI HALISI YA ULIMWENGU WETU WA LEO.
Kutokana na umuhimu wake nitaieleza kirefu:
Ili kukidhi adhima hiyo, Mtaguso wa Pili wa Vaticano katika majadiliano yake ulifanikiwa kuchapisha na kusambaza HATI 16 za Mafundisho yaliyojaa utajiri kwa kiimani, maadili na nidhamu ndani ya Kanisa lote. Hati hizi zimegawanyika kama ifuatavyo:

1) Hati Nne za kwanza za Mtaguso wa Vatican II zinaitwa KATIBA ZA MAFUNDISHO MUHIMU YA KANISA (CONSTITUTION):

(i) LUMEN GENTIUM: - “Mwanga wa Mataifa” – yaani, Kanisa Katoliki linajitambulisha kuwa ni Mwanga wa Mataifa.

(ii) DEI VERUBUM: - “Neno la Mungu” – yaani, Kanisa ni Jumuiya inayosimikwa katika Ufunuo wa Neno la Mungu.

(iii) SACROSANCTUM CONCILLIUM: - yaani, Kanisa ni Jumuiya inayoabudu hasa kwa adhimisho la Sakramenti ya EKARISTI TAKATIFU. Hati hii inatufundisha daima kutambua kuwa LITURUJIA NI NIDHAMU YA UTARATIBU MAALUM WA KANISA KATIKA IBADA NA MAADHIMISHO YAKE MBALIMBALI.

(iv) GAUDIUM ET SPES: - yaani, FURAHA NA MATUMANI: Hati hii inalitambulisha Kanisa kuwa ni chombo cha wokovu chenye kuleta furaha na matumaini kwa wanadamu ulimwenguni.

Wapendwa wajumbe, hati hizi nne zinaeleza kwa kina na mapana katika lugha nyepesi juu ya NIA NA LENGO la Utashi wa Yesu Kristo kwa Kanisa lake.

Hati hizi nne za Kikatiba, zinatualika na kutuagiza kuondoa kabisa yale mambo yasiyo ya lazima katika Ukristo wetu kusudi UINJILISHAJI UONEKANE WAZI KATIKA JAMII YETU INAYOKUWA KATIKA MAZINGIRA NA MABADILIKO MENGI YA KILA WAKATI.

2) Kundi la Pili la Hati hizi linaitwa MAAZIMIO MATATU YA MTAGUSO WA PILI WA VATICAN:

(i) Azimio la Kwanza linahusu: “UMUHIMU WA ELIMU” – “Gravissimum Educationis”
(ii) Azimio la Pili linahusu: “UHUSIANO WA KANISA NA DINI ZINGINE ZISIZO ZA KIKRISTO” – “NOSTRA AETATE”
(iii) Azimio la Tatu linahusu: “UHURU WA MTU KATIKA SWALA JUU YA KUABUDU” – “DIGNITATIS HUMANAE”

3) Kundi la Tatu la hati hizi ni MATAMKO MATATU JUU YA KUBADILI MIOYO YETU: Matamko haya yanatutayarisha na kutusaidia kuweka tayari mioyo yetu ili tuweze kweli kupokea mafundisho ya Kanisa.

(i) Vyombo vya Upashanaji Habari: - “INTER MIRIFICA” Kanisa lipinge mila na desturi potovu za giza zinazoweza kusambazwa na vyombo vya mawasiliano na upashanaji habari na badala yake vyombo hivyo hivyo vitumike katika kueneza UFALME WA MWANGA.

(ii) Makanisa ya Mashariki – “ORIENTALIUM ECCLESIARUM” Jitihada njema za Makanisa ya Mashariki katika kuboresha Liturujia na kuendeleza Elimu ya Teolojia tangu mwanzo wa Ukristo ziendelezwe. Makanisa haya ni sehemu ya ya Kanisa Katoliki. Jitihada za kuyafikia makanisa mengine ya mashariki ziendelezwe.

(iii) UHUSIANO WA KIDUGU WA MAKANISA MENGINE YA KIKRISTO AMBAYO SI YA KIKATOLIKI – “UNITATIS REDINTEGRATIO” – EKUMENE. Kuimarisha mahusiano mema kati yetu wakristo na kuudumisha.

4) MATAMKO SITA YA MTAGUSO JUU YA MAENEO MAALUM YA KUREKEBISHWA: Lengo ni kuleta mageuzi, mabadiliko katika Kanisa kadiri ya majukumu ya wanakanisa wote.

(i) WAJIBU WA MAASKOFU – “CHRISTUS DOMINUS”
(ii) KUHUSU MALEZI YA SEMINARI – “OPTATAM TOTIUS” Malezi bora katika Seminari zetu na jinsi ambavyo kila mmoja anaalikwa kushiriki.

(iii) KUHUSU MAISHA YA HUDUMA YA MAPADRE: - “PRESBYTERORUM ORDINIS”:- Malezi bora ya upadre – kielimu na kimaadili Kukuza ushirikiano katika huduma yao ya kichungaji.

(iv) MAISHA YA WAKFU KATIKA KANISA:- “PERFECTAE CARITATIS” Nafasi ya Watawa katika Kanisa tuifahamu vema ushirikiano wetu na Watawa uongozwe na taratibu zilizowekwa na Kanisa.

(v) UMISIONARI WA KANISA:-“AD GENTES” Mwaliko wa Mtaguso wa Pili wa Vatikani kwa kila mbatizwa kuwa mmisionari. Tutolee nguvu zetu zote kwa ajili ya maendeleo ya ustawi wa Kanisa. Tujitoe sadaka sisi wenyewe.

(vi)UTUME WA WALEI: Nafasi ya Walei ndani ya Kanisa Kusimika familia za kikristo zilizo misingi ya Jumuiya Ndogondogo za Kikristo. Kutakatifuza ulimwengu kwa kuonesha ushuhuda wa kina katika nyanja mbalimbali. Kuiga mfano wa familia ya NAZARETI.

SINODI MBILI ZA MAASKOFU KWA AJILI YA BARA LA AFRIKA NA MADAGASCAR:

Kati ya miaka ya 1994 na 2009, pamekuwepo na Sinodi mbili za Maaskofu zilizojadili mambo muhimu yanayolihusu Kanisa la Afrika na Madagascar.
Mambo yaliyoongelewa na kuamuliwa katika Sinodi hizi ni mengi na ya maana sana kwa Kanisa letu la Afrika – Jimbo la Musoma likiwemo.

MWAKA WA IMANI:

Mwaka 2012/13 umetangazwa kuwa Mwaka wa Imani – ambao rasmi unaadhimishwa kuanzia tarehe 11 Oktoba 2012 hadi 24 Novemba, 2013. Lengo Kuu ni kuamsha katika kila muumini hamu ya KUKIRI IMANI KIKAMILIFU NA KWA UTHABITI MPYA, KWA KUJIAMINI NA KWA MATUMAINI. Mwaka unaotupatia fursa kubwa sisi sote kukuza ushuhuda wa maisha yetu katika IMANI tunayosadiki katika mazingira yetu. Tuamini kwa moyo, na tukiri kwa kinywa.

KATEKISIMU YA KANISA KATOLIKI:
Ni miaka ISHIRINI sasa imetimia tangu itangazwe rasmi na Mwenyeheri Yohane Paulo II (11 Oktoba, 1992) Katekisimu hii ni tunda kuu la pili la Mtaguso wa Pili wa Vatican.

SHERIA ZA KANISA – C.I.C. (1983 – 2013)
Imetimiza miaka 30 tangu itangazwe rasmi tarehe 25 Januari, 1983.

MIAKA MITANO (5) YA UASKOFU:
Tarehe 20 Januari, 2013 nimetimiza rasmi miaka mitano ya uaskofu. Kipindi hiki kimenifundisha mengi juu ya Uchungaji na Maendeleo ya Jimbo letu.
Ni vizuri tushirikishane hayo na hatimaye kuyaweka kama sehemu ya maazimio yetu.











All the contents on this site are copyrighted ©.