2013-05-21 08:46:59

Vatican na FAO kushirikiana katika mapambano dhidi ya baa la njaa na utapiamlo wa kutisha duniani


Bwana Josè Graziano da Silva, Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO anasema anapenda kushirikiana na Vatican katika mapambano dhidi ya baa la njaa na utapiamlo unaoendelea kusababisha maafa makubwa sehemu mbali mbali za dunia, lakini kwa namna ya pekee Barani Afrika. Kutokana na changamoto hii, Baba Mtakatifu Francisko amekubali kukutana na kuzungumza na ujumbe wa FAO mwezi Juni, 2013.

Baa la njaa si tu ni suala la kiuchumi lakini pia linagusa maadili na utu wema, mshikamano na upendo. Ni jambo ambalo haliwezi kukubalika kwamba, kuna baadhi ya watu duniani wanakula na kusaza kiasi cha kutupa chakula na wakati huo huo kuna watoto wanaoendelea kuteseka kutokana na utapiamlo.

Uchoyo na ubinafsi ni kielelezo makini cha kumong'onyoka kwa misingi na maadili na utu wema. Kama watu wangejenga moyo wa upendo, urafiki na udugu, watu zaidi ya billioni mbili wasingeteseka kutokana na baala njaa. Bwana Graziano katika mahojiano maalum na Shirika la Habari la Zenit anasema kwamba, Kanisa kwa miaka mingi limekuwa likijihusisha na mchakato wa maendeleo endelevu miongoni mwa watu wa Mataifa. Limejitahidi kuwajengea watu uwezo wa kupambana na hali ya maisha. FAO na Kanisa wanaweza kushirikiana katika mapambano dhidi ya baa la njaa duniani.

Bwana Graziano anasema kwamba, gharama za uzalishaji, utunzaji na usafirishaji wa mazao ya chakula ni kubwa mno kwa mwananchi wa kawaida. Kumbe, Jumuiya ya Kimataifa inakabiliwa na changamoto ya kuhakikisha kwamba, inaongeza uzalishaji na tija katika sekta ya kilimo; kunakuwepo na sera makini za utunzaji bora wa mazingira na matumizi sahihi ya maji pamoja na kuhakikisha kwamba, wakulima wadogo wadogo wanawezeshwa ili kupata pembejeo za kilimo.







All the contents on this site are copyrighted ©.