Makanisa Barani Afrika yana mchango mkubwa katika kudumisha demokrasia na utawala
bora
Baraza la Makanisa Ulimwenguni linasema, Makanisa Barani Afrika yana matumaini makubwa
kwamba, Serikali zitaweza kuendeleza mchakato wa utawala bora, misingi ya haki, amani,
demokrasia na utulivu kama kikolezo cha maendeleo endelevu ya binadamu kiroho na kimwili.
Hivi karibuni, wawakilishi wa Makanisa, Vyama vya Kiekumene pamoja na Vyama
vya kiraia walikusanyika nchini Zimbabwe ili kupembua kwa kina na mapana mchango wa
Makanisa katika kudumisha haki, amani, utulivu, utawala wa sheria na demokrasi ya
kweli Barani Afrika, kwa kuzingatia kwamba, katika miezi ya hivi karibuni kuna nchi
kadhaa Barani Afrika zitakuwa zinafanya uchaguzi mkuu, Zimbabwe ni kati ya nchi hizi.
Kwa pamoja wajumbe wamekazia umuhimu wa kuwa na Serikali imara itakayosimamia
kwa ukamilifu maendeleo ya wananchi wake badala ya kuendekeza migogoro na kinzani
ambayo imekuwa ni chanzo cha wananchi kukata tamaa na mkwamo wa maendeleo ya watu
katika sekta mbali mbali za maisha. Viongozi wa Makanisa wanasema, Kanisa linaweza
kuchangia kwa kiasi kikubwa kwa Jamii kuweza kukabiliana na changamoto mbali mbali
zinazoendelea kujitokeza nchini Zimbabwe.
Wananchi wa Bara la Afrika hawana
budi kushirikiana kwa pamoja katika kujenga na kudumisha misingi ya demokrasia na
utawala bora kama sehemu ya mchakato wa kuimarisha haki na amani Barani Afrika. Kutokana
na ukweli huu, Makanisa hayana budi kushirikiana kwa pamoja katika kutafuta na kudumisha
mafao ya wengi; pamoja na kuhakikisha kwamba, uongozi unakuwa ni kwa ajili ya huduma
kwa raia.
Kipindi cha mpito kuelekea kwenye demokrasi ya kweli, hakina budi
kupewa kipaumbele cha pekee kwani hapa kwa miaka mingi pamekuwa ni chanzo cha vurugu,
vita na kinzani za kijamii. Kwa hakika mchango wa Makanisa unafahamika katika harakati
za ukombozi Barani Afrika. Changamoto kwa Makanisa kwa wakati huu ni kuhakikisha kwamba,
yanakuwa ni vyombo vinavyowaunganisha watu kwa ajili ya mafao, ustawi na maendeleo
yao: kiroho na kimwili na kwamba, kila mwananchi ana haki ya kushiriki katika kudumisha
demokrasia na utawala bora.